Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo akifungua warsha
ya kujadili changamoto za Uendeshaji wa Mabaraza ya Biashara Tanzania
inayofanyika kwa siku mbili Jijini Dodoma.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Dkt.
Bilinith Mahenge akizungumza na wadau wa baraza la biashara kabla ya
kumkaribisha mgeni rasmi kufungua warsha hiyo.
Kaimu Mkurugenzi wa Tawala za
Mikoa OR-TAMISEMI Beatrice Kimoleta(kwanza Kushoto) akiwa na Mkurugenzi
Msaidizi wa Utawala bora na Huduma OR-TAMISEMI Angelista Kihaga (kwanza
kulia) pamoja na wadau wa Baraza la Biashara katika warsha ya kujadili
uendeshaji wa Mabaraza ya Biashara.
Mshauri wa Majadiliano baina ya
Sekta Umma na Binafsi wa LIC Bw. Donald Liya (Kwanza kushoto) akifuatiwa
na Kiongozi Msaidizi wa Timu ya LIC Bw. Peter Laizer, Mshauri wa Mradi
wa LIC toka Taasisi ya Sekta Binafsi Bi. Rehema Mbugi pamoja na
Kaimu Mkurugenzi wa TCCIA Bw. Gotfried Muganda wakifuatilia warsha ya
kujadili changamoto ya Uendeshaji wa Mabraza ya Biashara.
Mkurugenzi Msaidia wa Utawala toka OR-TAMISEMI Bw. Mrisho Mrisho akiongoza warsha ya Mabaraza ya Biashara Tanzania.
………………..
Nteghenjwa Hosseah, OR-TAMISEMI.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo amewataka Wakuu
wote wa Mikoa na Wilaya Nchini kuhakikisha wanaanzisha kituoa kimoja cha
huduma ‘One Stop Center’ kwa ajili ya wawekezaji.
Mhe. Jafo ameyasema hayo wakati wa
ufunguzi wa Warsha ya namna ya Uendeshaji wa Mabaraza ya Biashara kwa
Mikoa na Halmashauri zote Nchini iliyoandaliwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI
kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Mradi wa Local Investiment Climate (LIC) inayofanyika kwa siku mbili Jijini Dodoma.
Katika Warsha hiyo inayowajumuisha
viongozi wa Ngazi za Mkoa na Wilaya Mhe. Jafo amesema mazingira magumu
ya upatikanaji wa taarifa za uwekezaji na urasimu uliopo katika Mikoa na
Wilaya ndio unaowakwaza Wawekezaji katika harakati zao za kutaka
kuwekeza katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.
“Imekuwa ni vigumu sana kwa
Muwekezaji kupata taarifa sahihi na kwa wakati katika maeneo yetu na hii
imekua ikiwakatisha moyo na kupelekea hata kusitisha mpango mzima na
nia yao ya kuwekeza katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, inatakiwa
tubadilike na tuweke mazingira rahisi yatakayomuweza kila mdau anayetaka
kuwekez kupata taarifa anazozihitaji kwa urahisi.
Hali hii inarudisha nyuma juhudi
zetu za kuhamasisha uwekezaji sasa basi kila kiongozi wa Mkoa na Wilaya
kuhakikisha wanaanzisha kituo kimoja “One Stop Center” ambacho
kitatoa huduma zote kwa Wawekezaji kama vile upatikanaji wa maeneo ya
uwekezaji, Leseni za biashara, Hati miliki, usajili wa kampuni, namna ya
ulipaji wa kodi nk” alisema Jafo.
Aliongeza kuwa warsha hii
imewakutanisha wadau kutoka Sekta ya umma na binafsi katika kila ngazi
ya utawala ili kujadiliana namna bora ya kuboresha mazingira ya biashara
na uwekezaji Nchini na hivyo basi ni wakati wa kukubaliana kwa pamoja
namna mabaraza ya Biashara yatakavyosaidia katika kukuza Uchumi wa
Viwanda ambao ndio muelekeo wetu kama Taifa kwa hivi sasa.
Sambamba na hilo Jafo
aliwakumbusha viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuwa pamoja na
majukumu mengine wanapaswa kutengeneza mazingira bora ya kufanyia
biashara na uwekezaji, kuibua fursa za uwekezaji, kuzinadi fursa
zilizoibuliwa kupitia Makongamano ya uwekezaji na kuandaa midahalo
mahususi.
Pia Mhe. Jafo alisisitiza kuwa
mara baada ya kikao hiki kila kiongozi akahakikishe kuwa Vikao vya
mabaraza ya Biashara vinafanyika kwa mujibu wa Sheria na viongozi
washiriki katika vikao hivyo na maazimio ya vikao hivyo yakashughulikiwe
kwa wakati na kutoa mrejesho kwa upande wa sekta za umma na binafsi.
Aidha kila Halmashauri zikatenge
bajeti kwa ajili ya uendeshaji wa Mabaraza ya biashara na kwa upande wa
Sekta binafsia ziandae utaratibu mzuri wa kuchangia gharama za
uendeshaji wa vikao hivyo.
Alimalizia kuwa Mradi wa LIC kwa
kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI pamoja na Baraza la Taifa la
Biashara kuandaa utaratibu wa kueneza uzoefu uliopatikana katika Mikoa
miwli ya Dodoma na Kigoma ambapo mradi huu umetekelezwa ili mikoa
mingine iweze kujifunza na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.
Mabaraza ya Biashara Tanzania
yameanzishwa kwa mujibu wa Waraka wa Rais Na. 1 wa mwaka 2001 na
kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali Na. 691 la tarehe 28 Seot,2001.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni