Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisoma hotuba ya kuahirisha Mkutano wa 11 wa Bunge, jijini Dodoma Juni 29, 2018.
Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
………………….
*Ni baada ya Serikali na wananchi kulinda rasilimali za nchi
IMEELEZWA kuwa jitihada za
Serikali za kulinda rasilimali za nchi na ushirikiano kutoka kwa
wananchi zimesababisha ongezeko kubwa la idadi ya wanyama pori, hivyo
kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye wanyama wengi barani Afrika.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
ameyasema hayo leo (Ijumaa, Juni 29, 2018) katika hotuba yake aliyoitoa
bungeni wakati wakuahirisha Mkutano wa 11 wa Bunge jijini Dodoma.
Amesema ili kuitumia vema fursa ya
kuwa na vivutio vingi ikiwemo wanyamapori wengi na kuleta tija kwa
nchi, Serikali imeendelea kuandaa utambulisho wa Tanzania Kimataifa
(Destination Branding), lengo likiwa ni kuitambulisha Tanzania kama
kituo mahsusi cha utalii duniani.
“Tunalenga kuvutia wageni wa
kimataifa waje kuitembelea Tanzania, kuongeza wigo wa kutangaza vivutio
na kufanya vivutio vya utalii vifahamike duniani. Pia, Serikali
inakamilisha mchakato wa kuanzisha Channelmaalum katika Television ya Taifa (TBC1) kwa ajili ya kutangaza utalii,” amesema.
Waziri Mkuu amesema maandalizi ya
kuanzisha studio ya kutangaza utalii kwa njia ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano (TEHAMA) yanaendelea vizuri, ambapo studio hiyo itawezesha
kutambua, kufuatilia na kuwasiliana moja kwa moja na watu wanaofuatilia
Tanzania na vivutio vyake.
Pia, Serikali inakusudia kuanzisha
chombo kitakacho simamia fukwe za bahari, mito na maziwa lengo la hatua
hiyo ni kuimarisha utalii wa fukwe Bara na Visiwani kwa kujenga hoteli,
maeneo ya mapumziko na michezo mbalimbali.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu
amezungumzia jitihada zinazofanywa na Serikali katika kukabiliana na
changamoto ya migogoro ya matumizi ya ardhi miongoni mwa watumiaji kwa
kuunda timu ya kisekta ikijumuisha watendaji wa sekta mbalimbali
zinazohusika kwenye masuala hayo.
Sambamba na hilo, Waziri Mkuu
amesema Serikali imeandaa mipango ya matumizi ya ardhi, kupima mipaka ya
vijiji, kutunga na kurekebisha sera, sheria na kuandaa mipango
mbalimbali ya kuboresha matumizi na utawala wa ardhi.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema
Serikali imeandaa mipango ya kupanga, kupima na kumilikisha kila kipande
cha ardhi nchini. “Ni matumaini yangu kwamba programu hii ikitekelezwa,
ardhi itatoa mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii na
pia kudhibiti migogoro ya ardhi,”.
Waziri Mkuu amesema katika mwaka
wa fedha 2018/19, Serikali itaendelea kutatua migogoro inayojitokeza na
pia kutoa elimu kwa umma ili watumiaji wote wa ardhi waweze kuzingatia
mipango ya matumizi ya ardhi inayoandaliwa katika vijiji.
Amesema katika juhudi za kudhibiti
migogoro kwenye maeneo mbalimbali ya utawala, jumla ya vijiji 11,256
kati ya vijiji 12,545 vilivyopo nchini vimepimwa, hiyo ni sawa na
asilimia 90 ya vijiji vyote, huku lengo likiwa ni kupima mipaka ya
vijiji vyote na kuvipatia vyeti vya kijiji kwa kushirikiana na wadau wa
maendeleo.
“Hatua hii itasaidia kwa kiwango
kikubwa kutatua migogoro ya mipaka kati ya vijiji. Ili kuharakisha kasi
ya upimaji nchini, Serikali itaendelea kutumia makampuni binafsi ya
upimaji na upangaji makazi kwa vibali maalum,”.
Akizungumzia kuhusu hifadhi ya
mazingira, Waziri Mkuu amesema misitu inaendelea kukatwa hovyo kwa
sababu mbalimbali ikiwemo matumizi ya nishati ya mkaa na kuni, ili
kukabiliana na tatizo hilo Serikali itaendelea kuhamasisha matumizi ya
nishati mbadala kote nchini.
Amesema Serikali itashirikiana na
sekta binafsi kuweka utaratibu mahsusi wa kuwawezesha na kuwaratibu
wajasiramali wanaojishughulisha na nishati mbadala ili kuwa na
uzalishaji wa kutosha wa nishati hiyo na iweze kusambazwa katika maeneo
yote nchini.
Aidha, Serikali itaendelea
kuboresha na kukamilisha Mkakati wa Tungamotaka (National Biomass Energy
Strategy) na kusambaza kwa wadau nchini ili kuratibu vyema upatikanaji
na matumizi ya nishati hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni