HOTUBA YA WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO MHE. DKT. MPANGO,AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO KWA MWAKA 2018/19


1
DODOMA                                
  1. UTANGULIZI
  • Mheshimiwa Spika, kutokana na taarifa iliyowasilishwa ndani ya Bunge lako Tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, naomba kutoa Hoja kwamba, Bunge lako sasa lipokee na kujadili mapitio ya utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa mwaka wa fedha 2017/18 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka ujao wa fedha 2018/19.
  • Mheshimiwa Spika, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu, kwa kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kuwasilisha bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa mwaka wa fedha 2018/19. Aidha, napenda nitumie fursa hii kuwapongeza Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Kassim M. Majaliwa (Mb.), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuliongoza Taifa letu kwa ujasiri na uzalendo wa hali ya juu. Mwenyezi Mungu azidi kuwapa afya njema, hekima na busara katika kuliongoza Taifa letu.
  • Mheshimiwa Spika, napenda pia kukushukuru wewe binafsi, Naibu Spika na Wenyeviti wote wa Bunge kwa kuendesha vema majadiliano ya mapendekezo ya bajeti za Wizara mbalimbali kwa mwaka 2018/19. Aidha, napenda kumpongeza Mhe. Hawa Abdulrahman Ghasia, (Mb.) kwa kuchaguliwa tena pamoja na Makamu Mwenyekiti mpya Mhe. Jitu Vrajlal Soni (Mb.). Aidha, nawapongeza na kuwashukuru wajumbe wote wa Kamati ya Bajeti kwa maoni, ushauri na mapendekezo waliyotoa ambayo yamesaidia sana katika kuboresha Mpango na Bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka 2018/19.
  • Mheshimiwa Spika, nitumie pia fursa hii kuwapongeza Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro – Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini, Mhe. Justin Monko – Mbunge wa Singida Kaskazini, Mhe. Dkt. Stephen Kiruswa – Mbunge wa Jimbo la Longido, Mhe. Dkt. Godwin Mollel – Mbunge wa Jimbo la Siha na Mhe. Maulid Mtulia – Mbunge wa Jimbo la Kinondoni kwa kuchaguliwa kuwakilisha Wananchi wa majimbo yao katika Bunge lako Tukufu. Aidha, natoa pole kwa Bunge lako Tukufu kwa kuwapoteza Mhe. Leonidas Gama aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini na Mhe. Kasuku Samson Bilago aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Buyungu. Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi, Amina.
  • Mheshimiwa Spika, naomba pia nitoe shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kachwamba Kijaji – Mbunge wa Kondoa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, kwa ushirikiano anaonipatia katika  kuhakikisha utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Fedha na Mipango unafanikiwa. Aidha, nawashukuru Bw. Doto James – Katibu Mkuu na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Naibu Makatibu Wakuu Bibi Amina Kh. Shaaban, Dkt. Khatibu M. Kazungu na Bi. Susan Mkapa kwa kusimamia vizuri shughuli za kila siku za kiutendaji za Wizara yangu. Pia napenda kumpongeza kwa dhati Prof. Florens Luoga – Gavana mpya wa Benki Kuu ya Tanzania na kumshukuru yeye pamoja na Bw. Charles Kichere – Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania na Dkt. Albina Chuwa – Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, kwa kusimamia kwa weledi taasisi nyeti walizokabidhiwa. Nawashukuru pia, Makamishna, Wakurugenzi, Wakuu wa Taasisi zote zilizoko chini ya Wizara, Wakuu wa Vitengo na wafanyakazi wote wa Wizara, kwa kutimiza wajibu wao vema wa kuwatumikia Watanzania.
  • Mheshimiwa Spika, hotuba yangu imejikita katika maeneo makuu mawili yafuatayo: Kwanza, ni Mapitio ya utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka 2017/18 na pili, Malengo na Maombi ya fedha kwa mwaka wa fedha 2018/19.
  1. MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI KWA MWAKA 2017/18
  • Mheshimiwa Spika, Wizara imetekeleza majukumu yake kupitia mafungu tisa ya kibajeti pamoja na Taasisi na Mashirika 36 yaliyo chini yake (Jedwali Na. 1 ukurasa 136). Mafungu hayo ni Fungu 50-Wizara ya Fedha na Mipango, Fungu 21-Hazina, Fungu 22-Deni la Taifa, Fungu 23-Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali, Fungu 10-Tume ya Pamoja ya Fedha, Fungu 13-Kitengo cha Udhibiti wa Fedha Haramu, Fungu 7- Ofisi ya Msajili wa Hazina, Fungu 66-Tume ya Mipango na Fungu 45-Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi.
  • Mheshimiwa Spika, majukumu ya Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na muhtasari wa mapato na matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2017/18 ni kama inavyooneshwa kwenye kitabu cha hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 4 hadi ukurasa wa 9.
    1. UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU KWA MWAKA 2017/18
  • Mheshimiwa Spika, naomba sasa kutoa taarifa mbele ya Bunge lako Tukufu kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa mwaka 2017/18 ambayo yameainishwa katika hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 10 hadi ukurasa wa 81.
  • Utekelezaji wa Sera za Uchumi Jumla
  • Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza jukumu hili, Wizara imejikita katika kuhakikisha kuwa malengo ya ukuaji wa uchumi, mfumuko wa bei, na mapato na matumizi ya Serikali yanafanikiwa. Katika mwaka 2017, kasi ya ukuaji wa uchumi imeendelea kuwa ya kuridhisha na kufikia wastani wa asilimia 7.1 ikilinganishwa na ukuaji wa wastani wa asilimia 7.0 mwaka 2016. Ukuaji huo ulichangiwa na kasi kubwa ya ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika sekta ya madini na uchimbaji mawe (asilimia 17.5), sekta ya maji (asilimia 16.7), sekta ya uchukuzi na uhifadhi mizigo (asilimia 16.6) na sekta ya habari na mawasiliano ambayo ilikua kwa asilimia 14.7.
  • Mheshimiwa Spika, wastani wa mfumuko wa bei kwa mwaka 2017 ulikuwa asilimia 5.3 na umeendelea kupungua hadi kufikia asilimia 3.8 mwezi Aprili, 2018. Kupungua kwa mfumuko wa bei kulichangiwa zaidi na kuongezeka kwa uzalishaji wa chakula, utulivu wa thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya sarafu za kigeni, kuimarika kwa uzalishaji wa umeme, utekelezaji thabiti wa sera za fedha, urari wa malipo, kuongezeka kwa akiba ya fedha za kigeni pamoja na usimamizi wa bajeti ya Serikali. Mapato ya kodi kwa mwaka 2017/18 yanatarajia kufikia asilimia 13.0 ya Pato la Taifa ikilinganishwa na asilimia 13.3 mwaka 2016/17. Aidha, nakisi ya bajeti inatarajia kufikia asilimia 2.1 mwaka 2017/18 ikilinganishwa na asilimia 1.5 mwaka 2016/17.
  • Uratibu wa Mipango ya Maendeleo ya Taifa
  • Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18, Wizara imeandaa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2018/19. Mpango huu ni wa tatu katika kutekeleza Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2016/17-2020/21). Utekelezaji wa Mpango utasaidia Taifa kujenga msingi wa uchumi wa viwanda ili kukuza uchumi na kuondoa umaskini. Hivyo, Serikali inaendelea kuandaa mazingira wezeshi ili kuhuisha ushiriki wa sekta binafsi katika kugharamia utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo. Aidha, Wizara imekamilisha na kuchapisha Mkakati wa Utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano, 2016/17-2020/21. Mkakati huo unatoa mwongozo wa utekelezaji wa Mpango huo ambao utaiwezesha Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo 2025. Mkakati unalenga maeneo yafuatayo: viwanda vya nguo, ngozi, madawa, maeneo maalum ya kiuchumi, ukuaji wa miji na usimamizi wa maendeleo ya miji.
  • Mheshimiwa Spika, Wizara imefanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa Miradi ya Kitaifa ya Maendeleo iliyobainishwa katika Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano. Aidha, Wizara kwa kushirikiana na Wizara za kisekta ilifanya ufuatiliaji wa miradi 29 katika mikoa ya Morogoro, Shinyanga, Mwanza, Pwani, Iringa na Mbeya. Miradi iliyofuatiliwa ilijumuisha miradi ya sekta ya Umma na Binafsi, na sekta za Viwanda, Kilimo, Uvuvi, Maji, Afya, Elimu, Mifugo, Ujenzi na Miundombinu. Malengo makuu ya ufuatiliaji yalikuwa kubainisha hatua halisi za utekelezaji wa miradi husika, changamoto na hatua stahiki za kuzitatua ili yazingatiwe katika maandalizi ya Mpango wa mwaka 2018/19.
  • Uratibu wa Mikakati ya Kupunguza Umaskini
  • Mheshimiwa Spika, Wizara imekamilisha Taarifa ya mwanzo ya Hali ya Umaskini na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya mwaka 2016/17. Taarifa hii inabainisha mwelekeo wa hali ya umaskini, changamoto na jinsi ya kukabiliana nazo. Aidha, imeonesha  viashiria vitakavyotumika na kubainisha wapi tulipoanzia (baselines) ili kupima mafanikio katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia 2030.
  • Mheshimiwa Spika, taarifa hiyo inaonesha mafanikio yafuatayo: wastani wa umri wa kuishi umeongezeka kutoka miaka 63.3 mwaka 2015 na kufikia miaka 64.4 mwaka 2017; vifo vya watoto wachanga vimepungua kutoka wastani wa vifo 38 mwaka 2015 hadi kufikia vifo 34.5 kwa vizazi hai 1,000 mwaka 2017; Pato la wastani la Mtanzania limeongezeka kutoka shilingi 1,918,931 mwaka 2015 na kufikia shilingi 2,275,601 mwaka 2017 sawa na ongezeko la asilimia 18.6; kuongezeka kwa umiliki wa samani katika kaya nao umeongezeka na upatikanaji wa huduma za jamii ikiwemo elimu, afya ya jamii, maji safi na salama, umeme  na miundombinu ya barabara umekuwa bora zaidi.
  • Mheshimiwa Spika, tathmini ya hali ya umaskini nchini iliyofanyika mwaka 2015/16 kwa ushirikiano baina ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Benki ya Dunia ilionesha kuwa umaskini wa mahitaji ya msingi umeendelea kupungua kutoka asilimia 28.2 mwaka 2011/12 hadi asilimia 26.4 mwaka 2015/16. Malengo ya Serikali ni kupunguza umaskini hadi kufikia asilimia 12.7 mwaka 2025/26. Hata hivyo, ili kubainisha hali ya umaskini hususan wa kipato, Ofisi ya Taifa ya Takwimu ikishirikiana na Benki ya Dunia hivi sasa inaendesha Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi (Household Budget Survey -HBS) kwa mwaka 2017/18. Hatua iliyofikiwa ni  ukusanyaji wa takwimu za mapato na matumizi ya kaya kwa miezi sita ya kwanza ya 2018 katika mikoa yote. Kwa msingi huo tunatarajia kuwa matokeo rasmi ya hali halisi ya umaskini na hususan wa kipato katika ngazi ya kitaifa, kimkoa na kiwilaya yatatolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu mwezi Machi, 2019.  
  • Usimamizi wa Ukusanyaji wa Mapato ya Serikali

  1. Mapato ya Ndani
  • Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18, sera za mapato zililenga kukusanya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi ya shilingi bilioni 19,977.0 ikijumuisha mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa. Hadi Aprili, 2018 jumla ya makusanyo ya ndani yakijumuisha mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa yalikuwa shilingi bilioni 14,838.5, sawa na asilimia 74 ya makadirio ya mwaka. Kati ya kiasi hicho, mapato ya kodi yalifikia shilingi bilioni 12,611.0 sawa na asilimia 74 ya lengo la mwaka la kukusanya shilingi bilioni 17,106.4; mapato yasiyo ya kodi yalifikia shilingi bilioni 1,789.9 sawa na asilimia 82 ya lengo la mwaka la kukusanya shilingi bilioni 2,183.4; na mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa yalikuwa shilingi bilioni 437.6, sawa na asilimia 64 ya makadirio ya shilingi bilioni 687.3 kwa mwaka. Vile vile, hadi kufikia Aprili 2018, Serikali ilikopa jumla ya shilingi bilioni 4,958.0 kutoka soko la ndani sawa na asilimia 80 ya shilingi bilioni 6,168.9 zilizotarajiwa kukopwa kwa mwaka. Kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni 4,125.7 zilikopwa kwa ajili ya kulipia dhamana na hati fungani za Serikali zilizoiva (rollover), na shilingi bilioni 832.3 zilikopwa ili kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo. Aidha, mikopo kutoka kwenye chanzo hiki, ilielekezwa kulipia sehemu ya madeni ya wakandarasi wa barabara na maji na umeme.
  1. Misaada na Mikopo nafuu toka kwa Washirika wa Maendeleo
  • Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Aprili 2018 Serikali imepokea kiasi cha shilingi bilioni 1,865.76 sawa na asilimia 47 ya lengo la shilingi bilioni 3,971.10. Kati ya kiasi kilichopokelewa, shilingi bilioni 70.2 ni Misaada na Mikopo nafuu ya Kibajeti (GBS) sawa na asilimia 7 ya ahadi  ya shilingi bilioni 941.26, shilingi bilioni 180.52 ni za mifuko ya pamoja ya kisekta sawa na asilimia 33 ya ahadi ya shilingi bilioni 556.08 na shilingi bilioni 1,612.61 kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo sawa na asilimia 65 ya ahadi ya shilingi bilioni 2,473.77.
  • Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na Sekta, Washirika wa Maendeleo, na Wadau wengine ilifanikiwa kuandaa na kukamilisha Mwongozo wa Ushirikiano wa Maendeleo (Development Cooperation Framework – DCF) ambao uliidhinishwa na Serikali mwezi Agosti 2017. Mwongozo huu umeanza kutekelezwa mwaka 2017/18 na utadumu hadi 2024/25. Aidha, Wizara imeendelea kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa programu na miradi ya maendeleo inayonufaika na fedha za nje ili kuhakikisha kwamba fedha hizo zinatumika kwa mujibu wa makubaliano kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo.
  • Uandaaji na Usimamizi wa Utekelezaji wa Bajeti ya Serikali
  • Mheshimiwa Spika, katika uandaaji na usimamizi wa bajeti ya Serikali ya mwaka 2017/18, Wizara ilifanya Uboreshaji wa Mfumo wa Uandaaji na Usimamizi ya Bajeti ya Serikali (Central Budget Management System – CBMS) ambao umeanza kutumika rasmi katika uandaaji wa bajeti ya mwaka 2018/2019. Pamoja na mambo mengine, mfumo huo utarahisisha utoaji na uchambuzi wa taarifa za mapato na matumizi na pia na  utaondoa kabisa tatizo la uingizwaji wa takwimu za bajeti mara mbili kama ilivyokuwa kwenye mifumo iliyopita. Kazi nyingine zilizotekelezwa ni pamoja na: kuendesha mafunzo ya mfumo wa CBMS kwa maofisa 246 kutoka kwenye Wizara, Idara Zinazojitegemea na Sekretariati za Mikoa; kuandaa, kuweka kwenye tovuti ya wizara, kuchapisha na kusambaza nakala 3,000 za Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti wa mwaka 2018/19; ukamilishaji wa Vitabu vya Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa mwaka 2018/19 Juzuu  Na. I, II, III na IV ambapo nakala 2,150 zilichapishwa na kuwasilishwa Bungeni kwa ajili ya kujadiliwa na pia kusambazwa kwenye Wizara, Idara Zinazojitegemea na Sekretarieti za Mikoa na Wadau wengine; na uandaaji wa Kijitabu cha Bajeti ya Serikali ya mwaka 2017/18 Toleo za Wananchi (Citizens Budget) kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza.
  • Usimamizi na Udhibiti wa Matumizi
  • Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18, Wizara kupitia Idara ya Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali imeendelea kufanya uhakiki wa madeni ya Serikali kama ifuatavyo:  Uhakiki wa madeni ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (NSSF, PPF, PSPF, GEPF, LAPF na NHIF), uhakiki wa madeni ya Mamlaka ya Uchimbaji Visima (DDCA) uliofanyika katika Halmashauri mbalimbali za mikoa ya Katavi, Morogoro, Arusha, Pwani na Lindi ambapo kiasi cha shilingi bilioni 1,166.85 kiliokolewa kutokana na uhakiki huo; na uhakiki wa madeni ya Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali 61 na Sekretarieti za Mikoa 26 umekamilika. Aidha, Wizara imefanya ukaguzi maalum katika maeneo yafuatayo; Hospitali Teule ya Mvumi Dodoma; Mradi wa SELF Microfinance Fund, kuchunguza ukwepaji wa kodi katika Biashara ya  vinywaji vikali; Kukagua mfumo wa kukusanya maduhuli  (ITS/AFCS system) wa Wakala wa Usafiri wa Mwendo wa Haraka (DART) na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA).
  • Mheshimiwa Spika, majukumu mengine yaliyotekelezwa chini ya Usimamizi na Udhibiti wa fedha za Umma ni kama inavyooneshwa kwenye kitabu cha hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 19 hadi ukurasa wa 24.
  • Usimamizi wa Malipo
  • Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2017/18, Wizara imeendelea kuboresha usimamizi wa malipo kwa kuunganisha mfumo wa malipo wa TISS katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani, Kagera, Geita, Simiyu, Shinyanga, Mara, Kilimanjaro, Manyara, Singida, Tabora na Kigoma.  Aidha, mfumo wa TISS umeunganishwa katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Fungu 25 na 37), Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (Fungu 57), Jeshi la Polisi (Fungu 28), Jeshi la Wananchi (Fungu 38), Jeshi la Kujenga Taifa (Fungu 39) na kuwapatia mafunzo Watumishi ili kuwawezesha kutumia mfumo huo. Vile vile, Wizara imesimika mfumo wa malipo (EPICOR) kwenye ubalozi wa Tanzania kule Nairobi-Kenya kwa lengo la kudhibiti matumizi nje ya bajeti. Kadhalika, Wizara imetoa mafunzo ya matumizi ya viwango vya kimataifa (IPSAS) kwenye uandaaji wa Hesabu kwa Wahasibu wa Wizara, Idara Zinazojitegemea na Wakala, Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Taasisi na Mashirika ya Umma 650 na kuwezesha kuandaa Hesabu za Majumuisho kwa mwaka wa fedha 2016/17 kwa kutumia Viwango vya Kimataifa (IPSAS Accrual Basis).
  • Deni la Serikali
  • Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kusimamia Deni la Serikali kwa kuzingatia Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada SURA 134. Mwezi Novemba 2017, Serikali ilifanya tathmini ya uhimilivu wa Deni la Serikali kwa kipindi kilichoishia Juni 2017. Tathmini hiyo inaonesha kuwa deni ni himilivu kwa kipindi cha muda wa kati na muda mrefu. Uwiano wa Deni la Serikali kwa Pato la Taifa ni asilimia 34.4 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 56; thamani ya sasa ya ya Deni la nje pekee kwa pato la Taifa ni asilimia 19.7 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 40; thamani ya sasa ya deni la nje kwa mauzo ya nje ni asilimia 81.8 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 150; na thamani ya sasa ya deni la nje kwa mapato ya ndani ni asilimia 117.1 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 250.
  • Mheshimiwa Spika, kazi ya viashiria hivyo vinne ni kupima uwezo wa nchi kukopa. Viashiria vilivyobaki vinapima uwezo wa nchi kulipa deni. Kutokana na tathmini, ulipaji wa deni la nje kwa kutumia mapato ya ndani umefikia asilimia 9.3 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 20 na ulipaji wa deni la nje kwa kutumia mauzo ya bidhaa nje ni asilimia 13.3 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 20. Kwa kuzingatia vigezo hivyo, Tanzania bado ina uwezo wa kuendelea ili kugharamia shughuli zake za maendeleo na pia ina uwezo wa kulipa mikopo inayoiva kwa kutumia mapato yake ya ndani na nje.
  • Mheshimiwa Spika, Pamoja na uhimilivu huo Serikali imeendelea kuchukua tahadhari kwa kukopa kwenye vyanzo vyenye masharti na gharama nafuu na kuhakikisha kuwa mikopo hiyo inaelekezwa kwenye miradi ya maendeleo itakayo chochea ukuaji wa uchumi, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, viwanja vya ndege na ujenzi wa mitambo ya kufua Umeme. Aidha, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kila robo mwaka inapitia viwango vya Deni la Serikali ili kuhakikisha kuwa deni linaendelea kuwa himilivu. Vile vile, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali amekamilisha ukaguzi wa deni hilo na Serikali inapitia taarifa hiyo kwa lengo la kuzingatia ushauri uliotolewa.
  • Mheshimiwa Spika, taarifa ya malipo ya Deni la Serikali iko katika hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 26 hadi ukurasa wa 28.
  • Usimamizi wa Mifumo ya Taarifa za Kifedha
  • Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18, Wizara imeendelea na kazi ya kuboresha Mfumo wa kutolea taarifa za kulipia mishahara kwa watumishi wa Umma kwa njia ya Kielektroniki (Government Salaries Payment Platform and Government Online Salary Slip Portal) ambapo mfumo wa kutolea taarifa za malipo ya Mishahara ya watumishi wa Umma na hati za mishahara (Government Salary Slip Portal) ulikamilika na kuanza kutumika mwezi Julai, 2017. Watumishi wa umma wanaweza kupata hati za mishahara kwa njia ya kielektroniki mahala popote palipo na mtandao. Aidha, maboresho haya yamepunguza gharama kubwa za usambazaji wa taarifa za mishahara. Pia Wizara imesimika mfumo wa makusanyo ya mapato yasiyo ya kodi, (Government electronic Payment Gateway – GePG) ambapo hadi sasa taasisi 86 zimeunganishwa na kati ya hizo taasisi 51 zimeanza kukusanya maduhuli kwa njia ya kielektroniki.
  • Usimamizi wa Mali za Serikali
  • Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha kunakuwa na usimamizi bora wa Mali za Serikali, Wizara imeendelea kufanya uthamini wa mali katika Wizara, Idara na Wakala za Serikali. Hadi Aprili 2018, uthamini wa ardhi na majengo ya Serikali katika Mafungu 48 ulifanyika ili kuwa na taarifa sahihi za mali za Serikali za Mafungu hayo. Aidha, Wizara imefanya uhakiki maalum wa Mali za Watu binafsi zilizo chini ya uangalizi wa Serikali kwa vituo 145 vya Polisi Tanzania Bara na Zanzibar  kwa lengo la kuipunguzia Serikali mzigo wa kulipa fidia zinazotokana na upungufu wa uangalizi na usimamizi wa Mali hizo.
  • Mheshimiwa Spika, kazi nyingine zilizofanyika katika usimamizi wa Mali za Serikali ni kama inavyooneshwa katika kitabu cha hotuba yangu ukurasa wa 31-32.
  • Ununuzi wa Umma
  • Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18, Wizara imetoa mafunzo kwa maafisa ununuzi na ugavi 75 juu ya matumizi ya mfumo wa uagizaji wa mahitaji wa Hati ya Ununuzi (Local Purchase Order-LPO) kupitia Mfumo wa Malipo ya Serikali (Epicor); na kukamilisha zoezi la tathmini ya Ufanisi wa Mfumo wa Ununuzi wa Umma na kuandaa mikakati ya utekelezaji wa matokeo ya zoezi hilo.
  • Mheshimiwa Spika, shughuli nyingine zilizotekelezwa chini ya Ununuzi wa Umma, Rufaa za Zabuni za Umma, Huduma ya Ununuzi Serikalini, na kupitia Bodi ya watalaam wa Ununuzi na Ugavi ni kama inavyooneshwa katika kitabu cha hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 32 hadi ukurasa wa 35.
  • Ukaguzi wa Hesabu za Serikali
  • Mheshimiwa Spika,  Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi katika kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Ibara ya 143 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanya ukaguzi wa mapato na matumizi ya Serikali kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2016/17.  Ofisi ilifanya ukaguzi wa hesabu za Wizara na Idara za Serikali zinazojitegemea 55, mikoa yote 26 ya Tanzania Bara; Wakala za Serikali 37, Mifuko maalum 15, Taasisi nyingine za Serikali 60, Balozi za Tanzania nje ya nchi 40. Aidha, ukaguzi ulifanyika kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa 185 na Mashirika ya Umma 105.
  • Mheshimiwa Spika, kazi nyingine za Ukaguzi wa Hesabu za Serikali zilizofanyika ni kama inavyooneshwa katika kitabu cha hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 35 hadi ukurasa wa 37.
  • Usimamizi wa Mashirika na Taasisi za Umma
  • Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18 Ofisi ya Msajili wa Hazina imefanya tathmini na uchambuzi wa Mikataba ya Utendaji Kazi 31 iliyoingiwa baina ya Msajili wa Hazina na Wenyeviti wa Bodi za Taasisi na Mashirika ya Umma katika mwaka 2016/17. Lengo la zoezi hilo ni kupima utekelezaji wa mikataba hiyo kwa mujibu wa viashiria vya mafanikio ambapo mambo ya msingi yanayozingatiwa katika tathmini ni pamoja na: utawala bora; usimamizi wa fedha; usimamizi wa rasilimali watu; na huduma kwa mteja. Katika zoezi la Mikataba ya Utendaji, kigezo ni taasisi husika kuwa na bodi hai na kuwa na bajeti iliyoidhinishwa. Matokeo ya tathmini yanaonesha wastani wa taasisi kufanya vizuri kwa asilimia 70.
  • Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Msajili wa Hazina imeendelea kufanya uchambuzi wa taasisi na mashirika ya umma ambayo majukumu yao kwa namna moja au nyingine yanafanana kwa lengo la kuunganisha taasisi hizo ili kuongezea tija na kupunguza gharama za uendeshaji.
  • Mheshimiwa Spika, shughuli zingine zilizotekelezwa katika kusimamia Mashirika na Taasisi za Umma ni kama inavyooneshwa katika kitabu cha hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 37 hadi ukurasa wa 39.
  • Mafao ya Wastaafu na Mirathi
  • Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18, Serikali ilitenga kiasi cha shilingi bilioni 1,008.61 kwa ajili ya kulipia michango ya mwajiri kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.  Hadi kufikia Aprili, 2018 kiasi cha shilingi bilioni 716.19 sawa na asilimia 71 kilitumika kulipa michango ya mwajiri kwa watumishi wa umma. Aidha, nitumie fursa hii kuiagiza Mifuko ya Hifadhi ya Jamii iandikishe wanachama wake, kuwapa vitambulisho vya uanachama na kutunza vizuri na kwa usahihi taarifa za uchangiaji kwa kipindi chote cha utumishi wa wanachama ili kuwaondolea usumbufu siku za kustaafu kwao kama ilivyoelekezwa na Miongozo ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Vile vile, ninawakumbusha watumishi wa Umma wawe na tabia ya kukagua taarifa za madaraja ya mishahara, makato ya lazima na yale yasiyo ya lazima kutoka kwenye mishahara yao na kutoa taarifa kwa wakati kwa mamlaka husika ili kama kuna makato hayako sawasawa mamlaka husika zichukue hatua za kurekebisha mapema na kuisaidia Serikali kuepuka tozo zinazoweza kutozwa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na Taasisi nyingine za fedha.
  • Mheshimiwa Spika, shughuli zingine zilizotekelezwa katika kusimamia Mafao ya Wastaafu na Mirathi ni kama inavyooneshwa katika kitabu cha hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 39 hadi ukurasa wa 41.
  • Udhibiti wa Utakasishaji Fedha Haramu na Ufadhili wa Ugaidi
  • Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18, Kitengo cha Udhibiti wa Fedha Haramu na Ufadhili wa Ugaidi kimeendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Udhibiti wa Fedha Haramu kwa kufanya yafuatayo: Kupokea na kuchambua taarifa 254 za miamala shuku inayohusu fedha haramu na ufadhili wa ugaidi na kuwasilisha taarifa za kiintelijensia 32 kwenye vyombo vinavyosimamia utekelezaji wa sheria kwa ajili ya uchunguzi. Aidha, katika kujenga uwezo wa watumishi, Maafisa wa Kitengo walipata mafunzo ya namna bora ya uchambuzi na upembuzi wa taarifa za miamala shuku katika Kituo cha Kudhibiti Fedha Haramu (Financial Intelligence Centre – FIC) cha Afrika ya Kusini na Maafisa wanne (4) walihudhuria mafunzo ya Financial Action Task Force (FATF) standards yaliyofanyika nchini Korea Kusini ambayo ni muhimu katika nyanja ya udhibiti wa fedha haramu na ufadhili wa ugaidi.
  • Mheshimiwa Spika, shughuli zingine zilizotekelezwa katika kusimamia utekelezaji wa Udhibiti wa Fedha Haramu na Ufadhili wa Ugaidi ni kama inavyooneshwa katika kitabu cha hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 41 hadi ukurasa wa 43.
  • Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP)
  • Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18, Wizara imeendelea kuratibu na kuchambua miradi ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi na kuishauri Serikali juu ya utekelezaji wa miradi hiyo. Aidha, kulingana na Sheria ya Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi Sura 103; uchambuzi wa miradi ya Ubia hupitia hatua tatu zifuatazo; (i) Mamlaka za utekelezaji kuwasilisha andiko la awali la mradi kwa ajili ya uchambuzi (ii) Mamlaka kuandaa taarifa ya awali ya upembuzi yakinifu (iii) Mamlaka ya utelekezaji wa miradi ikishirikiana na Mshauri Elekezi kuandaa na kuwasilisha Taarifa ya Upembuzi Yakinifu. Wizara hufanya uchambuzi wa taarifa hizo kwa kuangalia, pamoja na mambo mengine maeneo makuu matatu: (a) Uhamishaji wa mianya hasi ya mradi kwenda kwa sekta binafsi; (b) Uwezo wa Serikali kugharimia mradi; na (c) Manufaa ya mradi kwa Serikali  na wananchi kwa ujumla. Endapo mradi unakidhi vigezo utaidhinishwa na Kamati ya Wataalam wa PPP kwa ajili ya kuendelea na hatua ya kumpata mbia.
  • Mheshimiwa Spika, Wizara imefikia hatua mbalimbali za uchambuzi wa miradi itakayotekelezwa kwa utaratibu wa PPP. Upembuzi Yakinifu wa Mradi wa Uzalishaji wa Madawa muhimu na Vifaa Tiba wa Bohari Kuu ya Madawa (MSD) umekamilishwa na kuwasilishwa kwenye Kitengo cha Ubia kwa ajili ya hatua za uidhinishaji; Mradi wa Kujenga na Kuendesha Vyuo 10 vya VETA kwa Utaratibu wa PPP katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Manyara, Tabora na Shinyanga. Wizara  imefanya uchambuzi wa Taarifa ya Upembuzi Yakinifu na kuwasilisha kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia mapendekezo yanayotakiwa kuzingatiwa ili mradi uwe na tija kwa Taifa; Mradi wa Barabara ya Tozo kutoka Dar Es Salaam hadi Chalinze, taarifa ya upembuzi yakinifu wa mradi imefanyiwa uchambuzi ambapo Wizara imetoa idhini yenye masharti (Conditional Approval) ya kutekeleza  kabla ya kuendelea na hatua ya kumpata mbia; Mradi wa Uendeshaji wa Huduma ya Usafiri jijini Dar es Salaam Awamu ya kwanza, zabuni kwa ajili ya ununuzi wa mtoa huduma wa kudumu, mkusanyaji mapato na mwendesha mfuko zilitangazwa na wazabuni wamepatikana; na Wizara imekamilisha uchambuzi wa andiko la awali la mradi wa Mradi wa Mwambani Port lililowasilishwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania, hatua inayoendelea ni maandalizi ya Upembuzi Yakinifu.
  • Mheshimiwa Spika, shughuli zingine zilizotekelezwa katika kusimamia utekelezaji wa PPP ni kama inavyooneshwa katika kitabu cha hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 44 hadi ukurasa wa 46.
    1.  USIMAMIZI NA URATIBU WA TAASISI NA MASHIRIKA YA UMMA CHINI YA WIZARA
  • Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza hapo awali, Wizara yangu inaratibu na kusimamia mashirika na taasisi za umma 36 zilizo chini yake. Utekelezaji wa majukumu ya taasisi na mashirika haya kwa mwaka 2017/18 ni kama inavyooneshwa katika kitabu cha hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 47 hadi ukurasa wa 78.  Aidha, utekelezaji wa miradi ya maendeleo chini ya Wizara kwa mwaka 2017/18 ni kama unavyooneshwa katika kitabu cha hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 79 – 81.
    1. CHANGAMOTO NA HATUA ZILIZOCHUKULIWA
  • CHANGAMOTO
  • Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango, changamoto  zilizojitokeza ni pamoja na:
    1. Ukwepaji wa kodi;
    2. Kuchelewa kupatikana kwa misaada na mikopo ya masharti nafuu pamoja na mikopo ya kibiashara kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo;
    3. Uelewa mdogo wa wananchi juu ya dhana ya utakasishaji wa fedha haramu na ufadhili wa ugaidi ambayo ni pana na inabadilika kwa kasi;
    4. Baadhi ya wawekezaji kutelekeza mali walizouziwa na Serikali wakati wa zoezi la Ubinafsishaji; na
    5. Uelewa mdogo wa dhana ya ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi.
  • HATUA ZA KUKABILIANA NA CHANGAMOTO
  • Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto za utekelezaji wa bajeti, Wizara inaendelea kuchukua hatua mbalimbali zikiwemo:
    1. Kutekeleza mkakati wa ulipaji kodi kwa hiari na kuendelea kuboresha makusanyo ya mapato yasiyo ya kodi kwa kujenga mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji wa mapato;
    2. Kuendelea kuelimisha wadau mbalimbali kupitia makongamano, mikutano na warsha kuhusu dhana ya utakasishaji wa fedha haramu na ufadhili wa ugaidi;
    3. Kuendeleza mazungumzo na Washirika wa Maendeleo kuhusu njia mpya za kutoa na kupokea misaada na mikopo (New Financing Instruments);
    4. Wizara kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina imeongeza nguvu   katika kufanya ufuatiliaji wa karibu kwa wawekezaji wote ili kuhakikisha wanaendesha viwanda na mali walizouziwa kwa kuzingatia Masharti ya Mikataba ya Mauzo; na
    5. Kuendelea kutoa mafunzo kuhusu ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi kwa watumishi wa umma na sekta binafsi.
  1. MALENGO YA MPANGO NA BAJETI KWA MWAKA 2018/19
  • Mheshimiwa Spika, Mpango na Bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa mwaka 2018/19 umeandaliwa kwa kuzingatia Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025, Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030, Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016 /17- 2020/21), Sheria ya Bajeti Na.11 ya Mwaka 2015, Ilani ya Chama Cha Mapinduzi – CCM (2015 – 2020), Hotuba ya Mheshimiwa Rais wakati wa Uzinduzi wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na masuala mtambuka kama vile Jinsia, watu wenye ulemavu, Mazingira, UKIMWI, makundi mengine yaliyo katika mazingira hatarishi na masuala ya lishe kwa jamii pamoja na maelekezo na ahadi zilizotolewa Kitaifa.
    1. MPANGO WA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA WIZARA
  • Kusimamia Utekelezaji wa Sera ya Uchumi Jumla
  • Mheshimiwa Spika, shabaha za uchumi jumla katika kipindi cha mwaka 2018/19 ni kama ifuatavyo:-
  1. Pato la Taifa kukua kwa asilimia 7.2 mwaka 2018 kutoka ukuaji halisi wa asilimia 7.1 mwaka 2017;
  2. Mfumuko wa bei kuendelea kubaki katika wigo wa tarakimu moja;
  3. Mapato ya ndani kufikia asilimia 15.8 ya Pato la Taifa mwaka 2018/19 kutoka matarajio ya asilimia 15.3 mwaka 2017/18 na asilimia 15.6 mwaka 2016/17;
  4. Mapato ya kodi kufikia asilimia 13.6 ya Pato la Taifa mwaka 2018/19 kutoka matarajio ya asilimia 13.0 mwaka 2017/18 na asilimia 13.3 mwaka 2016/17; na
  5. Nakisi ya bajeti kufikia asilimia 3.2 ya Pato la Taifa mwaka 2018/19 kutoka matarajio ya asilimia 2.1 mwaka 2017/18 na asilimia 1.5 mwaka 2016/17.
  • Uratibu wa Mipango ya Maendeleo ya Taifa
  • Mheshimiwa Spika, kutokana na kuunganishwa kwa iliyokuwa Tume ya Mipango na Wizara ya Fedha, imebidi kuupitia muundo wa Wizara ili uweze kuyaingiza mabadiliko haya ili kutoathiri utekelezaji wa majukumu pamoja na maslahi ya watumishi kwa ujumla. Muundo wa Wizara uko katika hatua za mwisho za kuidhinishwa na Mamlaka husika, ambapo imependekezwa iundwe Divisheni ya Mipango ya Maendeleo ya Taifa itakayoongozwa na Kamishna na kuwa na kifungu chake.
  • Mheshimiwa Spika, hivyo katika mwaka 2018/19, shughuli za kipaumbele zitakazotekelezwa katika uratibu wa mipango ya maendeleo ya Taifa ni pamoja na: Kuandaa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2019/20; Kufuatilia utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2018/19; Kufanya tathmini ya muda wa kati katika utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano; Kukamilisha uundwaji wa Mfumo wa Kielektroniki wa usimamizi wa miradi ya kitaifa ya Maendeleo; na Kufuatilia matumizi ya Mwongozo wa Usimamizi wa Uwekezaji wa Umma (Public Investment Management – Operational Manual – PIM – OM).
  • Uratibu wa Mikakati ya Kupunguza Umaskini
  • Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Wizara itaendelea kusimamia na kuratibu utekelezaji wa juhudi za kupunguza umaskini ikiwemo kusimamia utekelezaji wa Mfumo wa  Ufuatiliaji wa Jitihada za Kuondoa Umaskini nchini (Poverty Monitoring System – PMS); kufuatilia utekelezaji wa malengo yaliyoainishwa katika Mipango ya kitaifa na kisekta na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) 2030 na programu zinazolenga kuondoa umaskini katika maeneo ya vijijini na mijini; kufanya uchambuzi wa kina juu ya Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya (HBS-2017/18); kutoa mafunzo kwa Maafisa Mipango na Maendeleo ya Jamii wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa kuhusu jitihada za kupambana na umaskini na kutunza mazingira ili kuweza kujumuisha katika mipango na bajeti zao.
  • Mheshimiwa Spika, Mipango mingine katika uratibu wa Mkakati wa Kupunguza Umaskini iko katika hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 87 hadi ukurasa wa 89.
  • Usimamizi wa Ukusanyaji wa Mapato ya Serikali
  1. Mapato ya Ndani
  • Mheshimiwa Spika, katika kuboresha ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa mwaka 2018/19, Wizara imepanga kutekeleza yafuatayo: kusimamia sera za fedha na za kibajeti zinazolenga kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara; kuhamasisha ulipaji kodi kwa hiari kwa kuimarisha Mkakati Shirikishi wa Mawasiliano na Walipa kodi na kuboresha utaratibu wa utozaji kodi; kujenga  uwezo wa watumishi ili kukabiliana na tatizo la uhamishaji faida (Transfer Pricing) unaofanywa na kampuni zenye mitandao ya kimataifa kwa lengo la kukwepa au kupunguza kodi; kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa ulipaji kodi kupitia Mfumo wa Vitalu vya Walipakodi; kusimamia zoezi la uunganishaji wa Wizara, Idara, Wakala, taasisi na mashirika ya umma kwenye Mfumo wa Serikali wa  Kielektroniki wa ukusanyaji wa mapato (GePG) ili kuboresha ukusanyaji na kudhibiti upotevu wa mapato ya Serikali; na kuongeza kasi ya uthaminishaji wa majengo ili kuongeza mapato yatokanayo na kodi ya majengo.
  • Mheshimiwa Spika, mikakati mingine iliyopangwa iko katika hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 89 hadi ukurasa wa 90.  
  1. Misaada na Mikopo
  • Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19 Wizara itaendelea na uratibu wa upatikanaji wa fedha za misaada na mikopo nafuu kutoka kwa Washirika wa Maendeleo kwa ajili ya kugharamia programu na miradi ya maendeleo mbalimbali nchini. Washirika wa Maendeleo wameahidi kuchangia Bajeti ya Serikali kiasi cha shilingi bilioni 2,676.64. Kati ya fedha hizo,  shilingi bilioni 545.76 ni kwa ajili ya Misaada na Mikopo nafuu ya Kibajeti (GBS), shilingi bilioni 125.86 kwa ajili ya Mifuko ya Pamoja ya Kisekta na shilingi bilioni 2,005.02 kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
  • Mheshimiwa Spika, kazi nyingine zilizopangwa kutekelezwa ni pamoja na: kukamilisha Mpango Kazi wa kutekeleza Mwongozo mpya wa ushirikiano (Development Cooperation Framework- DCF); na kukagua miradi inayofadhiliwa na Washirika wa Maendeleo.
  • Uandaaji na Usimamizi wa Utekelezaji wa Bajeti ya Serikali
  • Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19 Wizara imepanga kutekeleza shughuli mbalimbali ikiwemo: kuendelea kuboresha Mfumo mpya wa Uandaaji na Usimamizi wa Bajeti ya Serikali (CBMS) ili kurahisisha utoaji  wa mgao wa fedha za matumizi kila mwezi na kuendesha mafunzo ya mfumo huo; kufanya marekebisho, kuchapisha na kusambaza nakala 2,200 Vitabu vya Makadirio ya Matumizi ya Serikali ya mwaka 2018/19 kama yalivyopitishwa na Bunge, kuchapisha na kusambaza: Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya mwaka 2019/20, Taarifa za Utekelezaji wa Bajeti ya Serikali za kila Robo Mwaka, Vitabu vya Makadirio ya Matumizi ya Serikali ya mwaka 2019/20 na kuviwasilisha Bungeni na kuvisambaza kwa Wizara, Idara Zinazojitegemea, Sekretarieti za Mikoa  kwa Wadau wengine.
  • Mheshimiwa Spika, kazi nyingine zilizopangwa kufanyika ziko katika hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 92 hadi ukurasa wa 93.
  • Usimamizi na Udhibiti wa Matumizi ya Serikali
  • Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2018/19, Wizara itaendelea kudhibiti matumizi ya fedha za umma kwa kufanya ufuatiliaji wa uzingatiaji wa miongozo mbalimbali ya ukaguzi wa ndani iliyotolewa na Wizara na kutoa mafunzo kwa wakaguzi wa ndani katika maeneo ya ukaguzi wa miradi, ukaguzi wa kiufundi, usimamizi wa vihatarishi, mfumo wa usimamizi wa kazi za ukaguzi na mfumo wa kusimamia utekelezaji wa mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
  • Mheshimiwa Spika, mipango mingine ambayo Wizara inatarajia kutekeleza katika usimamizi wa udhibiti wa fedha za umma iko katika hotuba yangu ukurasa wa 94 hadi ukurasa wa 95.
  • Usimamizi wa Malipo
  • Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Wizara imepanga  kusimamia mfumo wa udhibiti wa matumizi ya fedha za umma ikiwa ni pamoja na uanzishwaji wa Akaunti Jumuifu  (Treasury Single Account) kwa lengo la kuboresha mfumo wa matumizi ya Umma ili kuiongezea  Serikali uwezo wa kugharamia shughuli zake kwa wakati. Aidha, Wizara itaendelea na usimikaji na usimamizi wa mifumo ya malipo ya kieletroniki (EFT na TISS) ili kuondoa ucheleweshaji wa malipo kwa wadau mbalimbali wakiwemo wastaafu, watoa huduma kwa Serikali pamoja na watumishi wa Umma. Vile vile, Wizara itaendelea na uunganishaji wa mfumo wa Malipo (Epicor) kwenye Balozi saba (7) ili kudhibiti matumizi nje ya bajeti.
  • Deni la Serikali
  • Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Serikali itahakikisha kuwa Deni la Serikali linaendelea kuwa himilivu na kutokuwa mzigo kwa uchumi wetu na kuendelea kuwa fursa na kichocheo cha maendeleo kwa nchi yetu. Aidha, Serikali itaendelea kukopa kwa uangalifu kwa kuzingatia masharti nafuu. Mikopo hiyo itatumika kwenye miradi ya maendeleo yenye kuchochea ukuaji wa uchumi.
  • Mchango wa Mwajiri (Serikali) kwenye Mifuko ya Hifadhi ya  Jamii
  • Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea kuwasilisha kwa wakati michango ya kisheria ya mwajiri ya kila mwezi kwa ajili ya watumishi wa umma kwenye Mfuko Mpya wa Hifadhi ya Jamii utakaochukua nafasi ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii iliyounganishwa ya PSPF, GEPF, LAPF na PPF pamoja na mifuko ambayo haitaunganishwa ya NSSF, ZSSF, WCF na Bima ya Afya (NHIF).
  • Mheshimiwa Spika, ninatumia fursa hii  kuwasisitiza maafisa utumishi wote wanaohusika na kuingiza taarifa za watumishi wa umma kwenye mfumo wa kompyuta wa kutunza taarifa za watumishi wa umma waingize taarifa za watumishi kwa ukamilifu na usahihi ili uwasilishaji wa michango ya mwanachama na mwajiri kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii iwe kamili na sahihi kwa kipindi chote cha utumishi na hatimaye kurahisisha malipo ya mafao, pensheni na mirathi wakati wa hitimisho la utumishi wa umma ili kuwaondolea usumbufu watumishi wa umma walioitumikia nchi yao kwa weledi na uaminifu.
  • Usimamizi wa Mifumo ya Taarifa za Kifedha
  • Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Wizara imepanga kusimamia na kuboresha uendeshaji na utumiaji wa mfumo wa  taarifa za mishahara ya watumishi wa umma (Government Salaries Payment Platform – GSPP) kwa kuunganisha mfumo huo na taasisi za kibenki na mfumo wa pensheni kwa ajili ya urahisishaji wa huduma za mikopo na pensheni.  Aidha, Wizara itaendelea kuunganisha taasisi 260 katika mfumo wa kukusanya mapato yasiyo ya kodi (Government Electronic Payment Gateway System – GePG), ili kuweza kufanikisha ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali. Vile vile, Wizara itaunganisha mifumo 10 ya kielektroniki ya taarifa za kifedha kwa lengo la kuiwezesha mifumo iweze kubadilishana taarifa.
  • Usimamizi wa Mali za Serikali
  • Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Wizara imepanga kufanya kaguzi za mali za Serikali katika balozi kumi (10), kufanya kaguzi maalum na kutoa elimu ya utumiaji na utunzaji bora wa mali katika taasisi mbalimbali za Serikali ili kuepusha hasara zinazoweza kuzuilika.
  • Ununuzi wa Umma
  • Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Wizara imepanga kufanya yafuatayo: kukamilisha uandaaji na kuzindua Sera ya Ununuzi wa Umma pamoja kuanza utekelezaji wa sera hiyo; kukusanya maoni ya wadau kuhusu changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa sheria na kanuni za ununuzi wa umma kwa lengo ya kuzifanyia marekebisho pale itakapohitajika; kuwajengea uwezo maafisa ununuzi na ugavi serikalini juu ya matumizi ya mwongozo wa utekelezaji wa shughuli za ununuzi na ugavi; kuendesha mafunzo kwa maafisa ununuzi na ugavi kuhusu  matumizi ya mfumo wa malipo wa EPICOR katika ununuzi; kuandaa mpango kazi wa usimamizi wa ununuzi wa umma katika Serikali Kuu na Mamlaka ya Serikali za Mitaa; na kutekeleza mapendekezo ya taarifa ya tathmini ya ufanisi wa mfumo wa ununuzi wa umma.
  • Mheshimiwa Spika, kazi nyingine zilizopangwa kufanyika ziko katika hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 98 hadi ukurasa wa 101.
  • Ukaguzi wa Hesabu za Serikali
  • Mheshimiwa Spika,  katika mwaka 2018/19, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi imelenga kuimarisha ukaguzi wa mapato na matumizi ya Serikali kwa lengo la kuimarisha uwajibikaji na uwazi kwenye matumizi ya rasilimali za umma. Ili kufikia malengo hayo, Ofisi imepanga kutekeleza vipaumbele nane (8) kama ifuatavyo:  kufanya ukaguzi wa mafungu ya bajeti za Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala na Taasisi za Serikali, Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Mashirika ya Umma na Miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na wahisani; kufanya ukaguzi wa sekta ya gesi, mafuta na madini; kufanya maboresho ya mfumo wa ukaguzi kwa kutumia TEHAMA; na kukagua ukusanyaji wa mapato ya kodi na yasiyo ya kodi. Aidha, Ofisi imelenga kufanya ukaguzi wa kiufanisi na kaguzi maalum katika maeneo yatakayoainishwa; kuwajengea wakaguzi uwezo wa kufanya ukaguzi katika maeneo mapya ya ukaguzi kwenye sekta ya gesi asilia na mafuta, sekta ya madini, Serikali mtandao na katika uhalifu wa kifedha kwa kutumia mtandao (Financial crimes auditing). Vile vile, ofisi itaendelea na ujenzi wa majengo ya Ofisi za Ukaguzi katika Mikoa ya Rukwa na Mara.
  • Usimamizi wa Mashirika na Taasisi za Umma
  • Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Ofisi ya Msajili wa Hazina imepanga kutekeleza  yafuatayo: kufanya mapitio na kufuatilia kampuni ambazo Serikali ina Hisa chache na hazijawasilisha gawio serikalini; kufanya uchambuzi wa uwekezaji unaofanywa na Mashirika ya Umma katika Kampuni Tanzu na kampuni nyinginezo; kushirikiana na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, kufanya urejeshaji wa viwanda vinavyosuasua na kuwapatia wawekezaji mahiri; kusimamia kwa karibu ukusanyaji wa madeni ya ubinafsishaji wa iliyokuwa Benki ya NBC; kushirikiana na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mifuko ya Jamii, Taasisi za Fedha pamoja na wadau mbalimbali katika suala zima la uwekezaji na ufufuaji wa viwanda, kampuni na mashamba yaliyobinafsishwa.
  • Mheshimiwa Spika, Mipango mingine katika kusimamia Mashirika ya Umma iko katika hotuba yangu ukurasa wa 102 hadi ukurasa wa 103.
  • Mafao ya Wastaafu na Mirathi
  • Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea kuboresha, kutunza na kusimamia huduma za Pensheni kwa wastaafu wanaolipiwa Hazina ikiwa ni pamoja na kuendelea kulipa kwa wakati mafao na pensheni kwa wastaafu wa Serikali, mirathi na malipo ya kiinua mgongo kwa watumishi wa Serikali walio kwenye mikataba. Aidha, wizara itaendelea kuboresha masijala ya pensheni kwa kuendelea kuhifadhi kumbukumbu za wastaafu kielektroniki, ili kurahisisha malipo kufanyika kwa wakati.
  • Mheshimiwa Spika, naomba nisisitize kwa maafisa utumishi wote wanaohusika kuandaa mapema nyaraka za watumishi wanaotarajia kustaafu na kuziwasilisha Hazina zikiwa zimekamilika ili malipo ya mafao, pensheni na mirathi ya wastaafu wa kawaida yafanyike kwa wakati na kuwaondolea adha ya usumbufu watumishi pindi wanapokuwa wamestaafu. Aidha, nahimiza ofisi zote za umma zitunze taarifa za watumishi wa umma kielektroniki kwa kushirikiana na Wakala wa Serikali Mtandao.
  • Udhibiti wa Utakasishaji Fedha Haramu na Ufadhili wa Ugaidi
  • Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Kitengo cha Udhibiti wa Utakasishaji Fedha Haramu na Ufadhili wa Ugaidi itaendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Udhibiti wa Fedha Haramu ya Mwaka 2012 na Sheria ya Udhibiti Fedha Haramu na Mali Athirika ya Zanzibar ya Mwaka 2009 kwa kutekeleza yafuatayo: kufanya marekebisho ya Sheria ya Udhibiti wa Fedha Haramu (The Anti-Money Laundering Act, 2006) na kanuni zake za mwaka 2012 ili kuendana na mahitaji; kuendelea na utekelezaji wa mikakati ya kitaifa na kimataifa ya udhibiti wa utakasishaji wa fedha haramu na ufadhili wa ugaidi; kuendelea kupokea na kuchambua taarifa za miamala shuku zinazohusu utakasishaji wa fedha haramu na ufadhili wa ugaidi na taarifa za usafirishaji wa fedha kutoka na kuingia nchini kupitia mipakani; na kuendelea kuwasilisha taarifa za intelijensia kwenye vyombo vinavyosimamia utekelezaji wa sheria.
  • Tume ya Pamoja ya Fedha
  • Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Tume ya Pamoja na Fedha imepanga kufanya uchambuzi wa Mapato na Matumizi yanayohusu utekelezaji wa Mambo ya Muungano.
  • Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi
  • Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Wizara imepanga kufanya marekebisho ya Sheria na Kanuni za Ubia ili kuimarisha usimamizi wa mifumo ya usimamiaji wa miradi ya ubia na kupunguza mlolongo wa uidhinishaji wa miradi hiyo; kusimamia uibuaji na utekelezaji wa miradi ya ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP); kuandaa miongozo ya kitaalam ya kuainisha na kufanya uchambuzi wa miradi ya PPP; na kutoa mafunzo kuhusu utekelezaji wa miradi ya ubia kwenye Wizara, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Taasisi na Mashirika ya Umma na taasisi binafsi.
  • Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na mamlaka husika inategemea kukamilisha maandiko ya ujenzi wa reli ya Mchuchuma/ Liganga – Mtwara na reli ya Tanga – Arusha – Musoma kwa kiwango cha standard gauge; ujenzi wa miundombinu ya reli katika jiji la Dar Es Salaam kwa ajili ya treni ya abiria na mradi wa kusambaza gesi asilia nchini. Aidha, Wizara itaendelea na hatua ya kutangaza mradi wa ujenzi wa viwanda vya uzalishaji wa madawa muhimu na vifaa tiba chini ya MSD ili kuwapata wawekezaji.
  • Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma
  • Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Wizara kupitia Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma itaendelea kuziwezesha Wizara, Idara Zinazojitegema, Wakala, Taasisi za Serikali, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kutekeleza maboresho ya usimamizi wa fedha za umma katika maeneo mbalimbali, hususan:  marekebisho ya sheria za kodi ili sheria hizi ziendane na Sheria ya Uwekezaji; kuhuisha mikataba ya madini ambayo inapata misamaha ya kodi na mfumo wa kufanya maoteo ya viashiria vya uchumi jumla.
  • Mheshimiwa Spika, maeneo mengine ya maboresho ni pamoja na: kuandaa na kukamilisha Sera ya Kitaifa ya Ufuatiliaji na Tathmini; kuhuisha mikataba ya makubaliano na Washirika wa Maendeleo ili iendane na Sheria za Kodi za Tanzania; kufanya tathmini ya matokeo ya kiutendaji ya mfumo wa vihatarishi katika Wizara, Taasisi, Wakala na Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuimarisha mfumo wa udhibiti wa ndani; kuanzisha Ofisi mpya za Mhakiki Mali wa Serikali katika mikoa ya Simiyu, Katavi na Songwe; kufanya marekebisho ya sheria ya Udalali ya mwaka 1928; na kuimarisha ununuzi wa Umma.
  • Mradi wa Kimkakati wa kuongeza mapato kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa (Strategic Revenue Generation in LGAs Project)
  • Mheshimiwa Spika, kupitia Mradi huu, Wizara itatoa fedha katika Serikali za Mitaa zitakazokidhi vigezo vya miradi ya kimkakati ya kuongeza mapato ya Serikali za Mitaa. Aidha, Wizara imepanga kutoa mafunzo  kwa wawezeshaji wa kitaifa juu ya Usimamiaji na Uandaaji wa Miradi ya Kimkakati ya kuongeza mapato kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa.
    1. USIMAMIZI NA URATIBU WA TAASISI NA MASHIRIKA YA UMMA CHINI YA WIZARA
  • Mheshimiwa Spika, mipango na malengo ya bajeti kwa mwaka 2018/19 kwa upande wa mashirika na taasisi za umma zilizochini ya wizara ni kama inavyooneshwa katika kitabu cha hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 109 hadi ukurasa wa 127.
  1. MAKADIRIO YA  MAPATO NA MAOMBI YA FEDHA KWA MWAKA 2018/19
    1. MAKADIRIO YA MAPATO
  • Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19 Wizara inakadiria kukusanya maduhuli kiasi cha shilingi bilioni 597.81 kutoka katika vyanzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na mauzo ya nyaraka za zabuni, kodi za pango,  mauzo ya leseni za udalali, gawio, marejesho ya mikopo na michango kutoka katika Taasisi na Mashirika ya Umma.
    1. MAOMBI YA FEDHA KWA MWAKA 2018/19
  • Mheshimiwa Spika, Wizara ya Fedha na Mipango imepanga kutumia kiasi cha jumla ya shilingi 12,058,714,013,500 (Bilioni 12,058.71) kwa mafungu yote nane.  Kati ya fedha hizo, shilingi 10,763,501,474,000 (Bilioni 10,763.50)  ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi 1,295,212,539,500 (Bilioni 1,295.21) ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo. Matumizi ya Kawaida yanajumuisha shilingi 65,764,075,000 (Bilioni 65.76) kwa ajili ya mishahara, shilingi 693,257,399,000  (Bilioni 693.26) kwa ajili ya matumizi Mengineyo (OC) na shilingi 10,004,480,000,000 (Bilioni 10,004.48) ni malipo ya deni la Serikali na michango ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Aidha, katika fedha za matumizi ya maendeleo, shilingi 1,266,033,128,500 (Bilioni 1,266.03) ni fedha za ndani na shilingi 29,179,411,000 (Bilioni 29.18) ni fedha za nje.
MAOMBI YA FEDHA
  • FUNGU 50 – WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO
  • Mheshimiwa Spika, katika fungu hili kwa mwaka 2018/19, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:
  • Matumizi ya kawaida – Shilingi 57,022,927,000 (bilioni 57.02). Kati ya hizo:
  1. Mishahara – Shilingi 7,577,332,000 (bilioni 7.58)
  2. Matumizi mengineyo – Shilingi   49,445,595,000 (bilioni 49.44)
  • Miradi ya Maendeleo – Shilingi 28,790,817,000  (bilioni 28.79). Kati ya hizo:
  1. Fedha za Ndani – Shilingi 19,642,535,000            (bilioni 19.64).
  2. Fedha za Nje – Shilingi 9,148,282,000 (bilioni 9.15).
  • FUNGU 21 – HAZINA
  • Mheshimiwa Spika, katika Fungu hili kwa mwaka 2018/19, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:   
  • Matumizi ya Kawaida – Shilingi  531,890,056,000 (bilioni 531.89). Kati ya fedha hizo:
  1. Mishahara ya fungu hili – Shilingi 21,467,017,000 (bilioni 21.47).
  2. Matumizi Mengineyo – Shilingi 510,423,039,000.00  (bilioni 510.42) ambazo ni kwa ajili ya matumizi ya idara, taasisi zilizo chini ya Fungu hili, pamoja na matumizi maalum.
  • Miradi ya Maendeleo – Shilingi 1,247,611,267,500        (bilioni 1,247.61). Kati ya hizo:
  1. Fedha za Ndani – Shilingi 1,236,190,593,500       (bilioni 1,236.19)
  2. Fedha za Nje – Shilingi 11,420,674,000 (bilioni 11.42)
  • FUNGU 22- DENI LA TAIFA
  • Mheshimiwa Spika, katika fungu hili kwa mwaka 2018/19, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:
  • Matumizi ya kawaida – Shilingi 10,013,706,140,000    (bilioni 10,013.71). Kati ya fedha hizo:
  1. Mishahara – Shilingi 9,226,140,000 (bilioni 9.23)
  2. Matumizi Mengineyo (Malipo ya Madeni na Michango ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii) – Shilingi 10,004,480,000,000  (bilioni 10,004.48)
  • FUNGU 23 – MHASIBU MKUU WA SERIKALI
  • Mheshimiwa Spika, katika Fungu hili kwa mwaka 2018/19, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:-
  • Matumizi ya Kawaida – Shilingi 46,725,409,000                    (bilioni 46.72).    Kati ya fedha hizo:
  1. Mishahara – Shilingi 7,908,675,000 (bilioni 7.91)
  2. Matumizi Mengineyo – Shilingi Shilingi 38,816,734,000 (bilioni 38.82)
  • Miradi ya Maendeleo – Shilingi 3,200,000,000.00
         (bilioni 3.20).     Kati ya fedha hizo:
            (i)    Fedha za Ndani – Shilingi 2,000,000,000.00                             (bilioni 2.00).
        (ii)    Fedha za Nje  – Shilingi 1,200,000,000.00                     (bilioni 1.20).
  • FUNGU 7 –     OFISI YA MSAJILI WA HAZINA
  • Mheshimiwa Spika, katika Fungu hili kwa mwaka 2018/19, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:
    1. Matumizi ya kawaida – Shilingi 54,592,065,000.00         (bilioni 54.59). Kati ya fedha hizo:-
  1. Mishahara – Shilingi 2,362,279,000.00  (bilioni 2.36)
  2. Matumizi Mengineyo – Shilingi Shilingi 52,229,786,000.00 (bilioni 52.23).
    1. Miradi ya Maendeleo – Shilingi 1,650,000,000.00         (bilioni 1.65).     Kati ya fedha hizo:
            (i)    Fedha za Ndani – Shilingi 1,000,000,000.00                         (bilioni 1).
        (ii)    Fedha za Nje  – Shilingi 650,000,000.00 (bilioni 0.65).
  • FUNGU 10 – TUME YA PAMOJA YA FEDHA
  • Mheshimiwa Spika, katika Fungu hili kwa mwaka 2018/19, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:-
  1.     Matumizi ya Kawaida – Shilingi 2,155,075,000 (bilioni 2.15). Kati ya     fedha hizo:-
  1. Mishahara – Shilingi 574,933,000 (bilioni 0.57)
  2. Matumizi Mengineyo – Shilingi 1,580,142,000         (bilioni 1.58).
  • FUNGU 13 –     KITENGO CHA KUDHIBITI FEDHA HARAMU
  • Mheshimiwa Spika, katika Fungu hili kwa mwaka 2018/19, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:
  1. Matumizi ya kawaida – Shilingi 2,015,586,000 (bilioni 2.01).
  2. Miradi ya Maendeleo – Shilingi 248,363,000 (bilioni 0.25) ambazo ni fedha za nje.
  •     FUNGU 45 – OFISI YA TAIFA YA UKAGUZI
  • Mheshimiwa Spika, katika Fungu hili kwa mwaka 2018/19, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:
  1. Matumizi ya kawaida – Shilingi 55,394,216,000       (bilioni 55.39). Kati ya fedha hizo:
  1. Mishahara – Shilingi 16,647,699,000 (bilioni 16.65).
  2. Matumizi Mengineyo – Shilingi 38,746,517,000     (bilioni 38.75).
  1. Miradi ya Maendeleo – Shilingi 13,712,092,000       (bilioni 13.71). Kati ya fedha hizo:
            (i)    Fedha za Ndani – Shilingi 7,200,000,000                              (bilioni 7.20).
        (ii)    Fedha za Nje  – Shilingi 6,512,092,000 (bilioni 6.51).
       
  1. SHUKRANI
  • Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kuzishukuru nchi na mashirika mbalimbali ya kimataifa ambayo kwa namna moja ama nyingine yamesaidia katika utekelezaji wa bajeti ya Wizara. Aidha, napenda kuwashukuru sana Wafanyakazi na wananchi wote ambao wameendelea kulipa kodi kwa hiari na pia kushiriki katika ujenzi wa Taifa letu.
  • Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa napenda kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa kunisikiliza. Hotuba hii inapatikana katika tovuti ya Wizara (www.mof.go.tz).
  • Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni