WAOMBAJI MIKOPO WAISHUKURU HESLB KWA KUWAPA FURSA KUREKEBISHA TAARIFA ZAO

 Afisa wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Bw. Ezra Ndangoya akimwelekeza sehemu ya kuweka sahihi Bw. Sironga Lowassa (kulia) ambaye ni mwombaji wa mkopo kwa mwaka wa masomo 2015/2016 katika ofisi za HESLB jijini Dar es Salaam leo (Jumatano, Septemba 2, 2015). HESLB inaendelea na kazi ya kurekebisha taarifa za wanafunzi waliokosea kujaza fomu zao za maombi.
 Afisa wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Bi. Zahra Kitara (kushoto) akipokea viambatanisho vya maombi ya mkopo kutoka kwa Bw. Paul Yahhi (kulia) mwombaji wa mkopo ambaye fomu yake ya maombi ilikosekana baadhi ya viambatanisho jijini Dar es Salaam leo (Jumatano, Septemba 2, 2015). HESLB inaendelea na kazi ya kurekebisha taarifa za wanafunzi waliokosea kujaza fomu zao za maombi. 
 Maafisa wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) (kulia) wakiwahudumia waombaji wa mikopo kwa mwaka wa masomo 2015/2016 ambao fomu za maombi zimegundulika kuwa na upungufu jijini Dar es Salaam leo (Jumatano, Septemba 2, 2015). HESLB inaendelea na kazi ya kurekebisha taarifa za wanafunzi waliokosea kujaza fomu zao za maombi.
 Afisa wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Bi. Christina Chacha (kulia) akimwelekeza jambo mwombaji wa mkopo ambaye fomu yake ya maombi ilikosekana baadhi ya viambatanisho jijini Dar es Salaam leo (Jumatano, Septemba 2, 2015). HESLB inaendelea na kazi ya kurekebisha taarifa za wanafunzi waliokosea kujaza fomu zao za maombi. (Picha na Eline Maronga-HESLB)
  
Na Eline Maronga 
WAOMBAJI wa mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2015/2016 ambao fomu zao za maombi zimegundulika kuwa na upungufu wameipongeza Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kwa kuwapa fursa ya kufanya marekebisho.
Mwishoni mwa wiki iliyopita HESLB ilitangaza orodha ya waombaji wa mikopo kwa mwaka wa masomo 2015/2016 ambao fomu za maombi ziligundulika kuwa na upungufu na kuwataka waombaji kufika katika ofisi za HESLB jijini Dar es Salaam na kufanya marekebisho kabla au ifikapo tarehe 11 Septemba mwaka huu (2015).
Wakiongea katika ofisi za Bodi leo (Jumatano, Agosti 2, 2015), waombaji hao wamesema hatua hiyo ya Bodi imewawezesha kurekebisha fomu zao katika maeneo waliyokosea na hivyo kuweka kumbukumbu zao sawa.
“Mimi ninaishi Arusha na nilipata taarifa kupitia magazetini na nikatembelea tovuti ya Bodi na kuona jina langu kuwa sikuweka sahihi… nikaamua kuja na sasa nimeweka sahihi,” amesema Bw. Sironga Lowassa leo nje ya Ofisi za HESLB.
Naye Bi. Enid Mneney, ambaye ni mhitimu wa kidato cha sita katika Shule ya Sekondari St. Mary Goreth iliyopo Moshi, anasema baada ya kuona jina lake katika tovuti ya Bodi, aliamua kwenda katika ofisi za Bodi ambako alifanikiwa kuweka sahihi.
“Mimi niliona jina langu kwenye tovuti kuwa sikuweka sahihi yangu, nimekuja na tayari nimeweka sahihi …ninashukuru kwa kupata fursa hii,” amesema Bi. Mneney mara baada ya kurekebisha taarifa zake katika ofisi za Bodi, eneo la Mwenge jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Bodi mwishoni mwa wiki iliyopita, jumla ya fomu za waombaji wa mikopo 7,788 kati ya 68,445 zilizopokelewa na kuhakikiwa zimegundulika kuwa na upungufu na kuwataka waombaji kusoma majina yao katika tovuti ya Bodi (www.heslb.go.tz).
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, taarifa muhimu zinazokosekana ni pamoja na sahihi za waombaji, nakala za vyeti vya kuzaliwa vya waombaji, sahihi na picha za wadhamini na baadhi ya fomu za maombi kutosainiwa na wanasheria na maafisa wa serikali za mitaa kama maelekezo yanavyotaka.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni