Majimbo 10 ya kufa au kupona




Wagombea ubunge wa majimbo 10 wana kazi ya ziada ya kufanya kabla ya Jumapili wakati wananchi watakapopiga kura kuamua ushindani mkali uliotanda kwa karibu miezi miwili ya kampeni za Uchaguzi Mkuu, kwa mujibu wa uchunguzi wa Mwananchi.

Ushindani huo mkubwa unatokana na vyama vya wagombea hao kuwekeza nguvu nyingi kwenye majimbo ili kuyarejesha, kuyalinda au kuwaengua wagombea ambao wanaonekana kuwa watakuwa wasumbufu iwapo watafanikiwa kuingia Bunge la 11.

Iringa
Mkoani Iringa, majimbo ya Iringa Mjini na Kilolo yana ushindani mkali.Jimbo la Kilolo linawaniwa na wagombea kutoka vyama vinne, Venance Mwamoto wa CCM, Taji Mtuga (ACT Wazalendo), Brian Kikoti (Chadema) na Lameck Mgimwa wa Chausta.

Hata hivyo, upinzani mkali unaonekana kuwa kwa Mwamoto, ambaye amerejea tena kwenye kinyang’anyiro hicho baada ya kuenguliwa kwenye kura za maoni za CCM mwaka 2010, na Kikoti, ambaye nguvu yake inatokana na kuungwa mkono na vyama vinne vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Ushindani huo unaelezwa kuanzishwa na mpasuko ndani ya CCM ulitokana na kura za maoni. Baada ya Mwamoto kumshinda Profesa Peter Msolla, aliyekuwa mbunge, na baadhi ya makada wa chama hicho kutimikia Chadema.

Mkazi wa Kilolo, Paulo Ngayomela, aliyekuwa mpambe wa Msolla, alisema yeye na wenzake walimuaga mbunge huyo wa zamani na kuungana na kambi ya upinzani baada ya kutoridhishwa na mchakato wa kumpata mgombea ndani ya CCM.

Mwamoto, ambaye aliangushwa na Profesa Msolla mwaka 2010, alisema bado ana nafasi ya kushinda kwa kuwa ni kama anatetea jimbo kwa kuwa aliliongoza jimbo hilo kuanzia mwaka 2005 hadi 2010.

Iringa Mjini
Jimbo jingine gumu kutabiri ni Iringa Mjini ambalo linawaniwa na Robert Kisinini wa DP, Daudi Masasi (ADC), Mchungaji Peter Msigwa wa Chadema, Chiku Abwao (ACT Wazalendo) na Frederick Mwakalebelea wa CCM.
Hata hivyo, Mchungaji Msigwa anayetetea kiti chake na Mwakalebela ndiyo wanaonekana kupambana vikali.

Mwakalebela anabebwa na falsafa inayotumiwa na CCM za kukomboa jimbo ambayo imefanikisha kuvunjwa makundi yaliyoundwa na wagombea wa nafasi hiyo wakati wa kura za maoni.

Mmoja wa makada wa chama hicho, Abdallah Mpogole alisema kwa sasa wanachama wote wameshikamana na wanachoangalia ni ushindi.

Hata hivyo, kada mmoja wa Chadema, Mussa Ali alisema: “Tukubali tusikubali tangu jimbo lilipoanzishwa, hakuna aliyefanya kazi kama Msigwa akiwa mbunge. Alipigania masilahi ya wakazi wa Iringa ikiwamo ujenzi wa barabara, maji na kutoa misaada ya vitanda katika Hospitali ya Wilaya ya Iringa.



Jimbo hilo linaangaliwa kwa karibu na uongozi wa kitaifa wa vyama hivyo. Mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa alikuwa wa kwanza kupita Iringa Mjini na kuvuta maelfu ya watu. Lakini Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli alifuta nyayo zake alipopita muda mfupi baadaye.

Ilemela
Mkoani Mwanza, Jimbo la Ilemela lina mchuano kutokana na CCM kutaka kulirejesha kutoka Chadema waliolitwaa mwaka 2010. CCM imemsimamisha Anjelina Mabula kupambana na mbunge anayemaliza muda wake, Highness Kiwia wa Chadema.

Kada wa CCM na mkazi wa Kata ya Kirumba, Yusuf Juma alisema uchaguzi wa Jimbo la Ilemela hauna mvutano kama Nyamagana, kwa sababu mgombea amekuwa na ushawishi mkubwa kuliko mwenzake wa Chadema.

Hata hivyo, mkazi wa National ambaye ni mfuasi wa Chadema, Shadrack Magafu alipinga akisema uchaguzi mwaka huu umekuwa mgumu kutokana na kila mtu kuhubiri mabadiliko.
Bukoba Mjini
Hali pia ni ngumu kwenye Jimbo la Bukoba Mjini mkoani Kagera, ambako ushindani ni mkali zaidi ya ule wa mwaka 2005. Linawakutanisha wagombea ambao ni mahasimu wakubwa, Wilfred Lwakatare wa Chadema, na Balozi Khamis Kagasheki wa CCM.

Wakati Kagasheki akitetea jimbo hilo kwa kipindi cha tatu, mshindani wake anawatumia makada wa CCM waliohamia upinzani kujiimarisha kisiasa akiwamo aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Bukoba, Dk Anatory Amani aliyehamia NCCR- Mageuzi iliyo ndani ya Ukawa.

Kundi la Dk Amani lililojiunga linaongezewa nguvu na aliyekuwa mwenyekiti wa UVCCM wa Manispaa ya Bukoba, Chifu Karumuna aliyehamia Chadema na kuongeza ushindani, huku Balozi Kagasheki akitajwa kuungwa mkono na wanawake wengi.

Baadhi ya wakazi wa Bukoba wanafananisha ushindani uliopo sasa na ule wa mwaka 2005. Mkazi wa Mtaa wa Miembeni, Levina Paul alisema anaona ushindani mkubwa.
“Wanawake wengi tunamuunga mkono Kagasheki tofauti na inavyoonekana kwa vijana, ila wagombea wote wanaweza kuwa na nguvu sawa,” alisema Paul.
Musoma Mjini 

Mkoani Mara, vita kali inaonekana Jimbo la Musoma Mjini, kati ya Vincent Nyerere wa Chadema na Vedastus Mathayo wa CCM aliyeangushwa na mshindani wake huyo mwaka 2010.
Jimbo hilo lina wagombea tisa ambao ni Tongora Eliud (ACT–Wazalendo), Ibrahim Seleman (Tadea), Maimuna Matola (ADC), Ruttaga Sospeter (AFP), Vedastus Mathayo (CCM), Vincent Nyerere (Chadema), Gabriel Ocharo (CUF), Nyakitita Chrisant (DP) na Makongoro Jumanne (UMD).

Mkazi wa mjini hapa, Leonard Lugwisha alisema kati ya wagombea hao mwenye nguvu zaidi na uhakika wa ushindi ni Nyerere, kwa kuwa ndiye mbunge anayependwa na vijana na watu wengi wamechoka kuongozwa na CCM.
Moshi Mjini
Hali ni mbaya zaidi Moshi Mjini, ambako wagombea wa CCM na Chadema wanachuana vikali kumrithi Philemon Ndesamburo ambaye ameamua kutogombea.

CCM imemsimamisha Davis Mosha na Jaffar Michael anagombea kwa tiketi ya Chadema, ambao wamefanya uchaguzi wa mwaka huu kuwa na ushindani ambao haujawahi kuonekana tangu mwaka 1995.

Mkazi wa Soweto, George Mberesero alisema ushindani wa vyama hivyo viwili ni mkubwa na kueleza kuwa kama si makosa ya kiufundi, CCM ingepata kura kuliko miaka ya nyuma.
“Huko nyuma ni kama CCM ilikuwa inafanya utani kwenye kampeni lakini safari hii imefanya kampeni,” alisema Mberesero.

Mfanyabiashara Patrick Boisafi alisema awali CCM ilianza vizuri harakati za kukomboa jimbo, lakini vurugu zimewatia doa.

Mkazi mwingine wa jimbo hilo, Goodluck Moshi alisema: “CCM wanaenda nyumba kwa nyumba, lakini Chadema wanaenda mitaani. Vijana wengi wa mtaani si wa jimbo hili. Davis anakubalika kwenye kata zenye watu wengi kama Njoro na Bomambuzi,” alisema.

Katika jimbo hilo, wagombea wa vyama vya ACT-Maendeleo, Buni Ramole na Issack Kireti wa SAU hawana nguvu.
Kawe
Jijini Dar es Salaam, nguvu ya Ukawa na CCM imeelekezwa Jimbo la Kawe ambako CCM imemsimamisha Kippi Warioba na wakati Chadema imeendelea kumuamini mbunge aliyemaliza muda wake, Halima Mdee.

Inaelezwa kuwa Kippi anategemea ushawishi wa baba yake, Jaji Joseph Warioba, ambaye apia ameshasimama jukwaani kumpigia debe mwanaye.
“Watu wanaweza kumchagua kwa kumfananisha na uzalendo wa baba yake,” alisema Maria Mashasi, mkazi wa Kawe.

Hata hivyo, Aliko Mwansisya ambaye pia ni mkazi wa Kawe, alisema Mdee anayo nafasi kubwa zaidi ya kutetea jimbo hilo kutokana na ushawishi wake ndani ya Bunge.
Ubungo
Hali kadhalika, Jimbo la Ubungo lina upinzani mkali kati ya mgombewa wa Chadema, Saed Kubenea, ambaye ni mwandishi wa habari, na wa CCM, Dk Didas Masaburi, ambaye ni meya wa jiji anayemaliza muda wake.

“Kubenea ana nafasi ya kushinda kutokana na umaarufu wake na nguvu ya chama,” alisema mkazi wa Ubungo, Charles Temba.
Lakini Vicent Julius alisema pamoja na umaarufu, Kubenea atakuwa na wakati mgumu wa kushinda jimbo hilo kutokana na ushawishi, uzoefu wa Dk Massaburi.

Ushindani mkali pia upo Same Mashariki, Mtama, Vunjo, Tarime Mjini, Tarime Vijijini, Bunda Mjini na Ukerewe.
Imeandikwa na Geofrey Nyang’oro, Midraji Ibrahim na Phinias Bashaya na Kelvin Matandiko

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni