MICHEZO HULETA AMANI, UPENDO NA KUHESHIMIANA - TANZANIA

Bw. Noel Kaganda, Afisa wa Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, akizungumza kwa niaba ya Tanzania wakati wa upitishaji wa Azimio kuhusu nafasi ya michezo katika ujenzi wa ulimwengu ulio bora na wenye amani. Azimio hilo limepitishwa siku ya Jumatatu na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Kabla ya kupitishwa wa Azimio, Wajumbe wa Baraza Kuu walifanya mkutano mfupi wa kumuenzi na kumkumbuka, Bw. Ali Treki mwanadiplomasia wa Libya na aliyewahi kuwa Rais wa Baraza Kuu la 64 la Umoja wa Mataifa. Bw. Treki alifariki Octoba 19 huko Misri.
  Katika hatua nyingine,Bw. Benedict Msuya Pichani Afisa Mambo ya Nje, akizungumza kwa niaba ya Tanzania wakati wa majadiliano ya Kamati ya Sita ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, kuhusu umuhimu wa programu ya mafunzo ya Sheria ya Kimataifa kwa nchi zinazoendelea. Tanzania imezishukuru baadhi ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kwa kutoa michango yao ya hiari ambayo imekuwa ikisaidia sana katika uendeshaji mafunzo kuhusu Sheria ya Kimataifa. Mafunzo hayo ambayo hutolewa Kikanda na ambayo baadhi ya wanasheria na wanadiplomasia kutoka Tanzania wamekuwa wakinufaika yanakabiliwa na uhaba mkubwa wa rasilimali fedha kutoka na kutotengewa bajeti na Umoja wa Mataifa licha ya umuhimu wa mafunzo hayo hususani kwa nchi zinazoendelea. Anayefuatilia majadiliano hayo nyuma ya Bw. Msuya ni Bi. Jamila Illomo kutoka Idara ya Uhamiaji, Wizara ya Mambo ya Ndani.
Michezo kama hii ya Bao, inaweza kuwa njia moja wapo ya vijana hawa kama wanavyoonekana pichani kutambua vipaji vyao, kuimarisha uwezo wao wa kufikiri, lakini kubwa zaidi kujenda maelewano, ushirikiano na kupendana kupitia mchezo huu na mingine mingi.


                                                                               Na MwandishiMaalum, New York
 

Imeelezwa kwamba michezo ya aina yoyote ile kuanzia mpira wa miguu hadi mchezo wa bao,ikutumiwa vema na kwa uzito unaostahili ni moja ya eneo ambalo linaweza kuchangia katika siyotu kuchochea kasi ya maendeleo bali hata katika kudumisha Amani, upendo na mshikamano miongoni mwa baina ya mataifa.

Ni kwa sababu hiyo jana (jumatatu) Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, limepitisha kwa mara nyingine Azimio ambalo pamoja na mambo mengine linasisitiza ujenzi wa ulimwengu bora na wenye Amani kupitia michezo ikiwamo michezo ya Olimpiki.

Azimio hilo na ambalo hupitishwa kila baada ya miaka miwili na ikiwa ni miezi michache kabla ya kuanza kwa michezo ya Olimpiki ya majira ya kiangazi, majira ya baridi na Olimpiki ya watu wenye ulemavu (Paralympic).

Miongoni mwa mambo yanayosisitizwa ni kuachana vitendo vyenye viashiria vya fujo, ugomvi au kubaguana siku saba kabla ya michezo kuanza na siku saba baada ya michezo kumalizika.

Michezo ya Olimpiki kwa majira ya kiangazi itafanyika mwakani (2016) huko Rio de Janairo,Brazil.

Na kwa kupitia azimio hilo, nchi wanachama wameipongeza Brazil kwa kuwa mwenyeji wa michezo hiyo pamoja na Olimpiki ya walemavu.

Azimio hilo pia limeitambua terehe 6 Aprili ya kila mwaka kuwa siku ya Kimataifa ya Michezo kwa ajili ya Maendeleo na Amani.

Tanzania ni miongoni mwa Nchi wanachama 150 zilizounga mkono azimio hilo lililopita kwa kauli moja. Akizungumza kwa niaba ya Tanzania wakati wa upitishaji wa Azimio ,Afisa wa Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Bw. Noel Kaganda, amesema, Tanzania ilianza kutambua umuhimu wa michezo katika ujenzi wa taifa mara tu ilipopata uhuru wake.

Akasema,Tanzania,inaamini kwamba, michezo ni kiungo muhimu katika ujenzi wa umoja wa kitaifa, kuleta usawa wa kijinsia, uwezeshwaji wa wanawake, fursa za elimu,afya,
maendeleo pamoja na kuzuia machafuko na utafutaji wa suluhu na kwamba azimio hili limekuja wakati muafaka ambapo Jumuiya ya Kimataifa imepitisha Ajenda 2030 na ikiadhimisha pia miaka 70 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa.

Na kuongeza ,tangu kuanzishwa kwa Taifa la Tanzania, Serikali kuanzia ile ya muasisi waTaifa hili, Mwalimu Julius Nyerere michezo imepewa umuhimu wa aina yake kwa kutungiwa sera na sheria mbali mbali ikiwa pamoja na kuwa na Wizara yake.

Akaeleza zaidi kwamba, michezo pia inafanyika mashuleni kuanzia shule za msingi, sekondari hadi elimu ya juu kwa kutoa mfano wa kama SHIMIWI ikiwa ni sehemu ya kuvumbua vipaji kwa wanafunzi wote bila ya kubagu jinsia zao

Akabinisha zaidi kuwa michezo kama ya Bao,mchezo ambao Baba wa Taifa aliuenzi sana na kuuendeleza ni baadhi ya michezo kati ya mingine mingi ya kiasili ambayo imekuwa ni kielelezo na nembo ya utaifa wa watanzania.

Aidha akasema, katika kuhakikisha kwamba vijana wanaanza kupata fursa ya kuanza kuonyesha vipaji vyao tangu wakiwa wadogo, hivi karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete amefungua kiwanja cha kisasa cha michezo kwa ajili ya vijana, kiwanja ambacho kimejengwa kwa ushirikiano na Kampuni ya Symbion ya Marekani na Sunderland A.F.C ya Uingereza.

Tanzania imesema, inakaribisha ubia na ushirikiano kama huo katika kuendeleza michezo pamoja na kubadilishana maarifa na uzoefu
Akizungumza dhana ya kuheshimiana, kuvumuliana kutokubagua na kwa misingi yoyote ile kama inavyosisitizwa kupitia Azimio hilo, Bw. Noel Kaganda amesema, Tanzania inasikitishwa na kuendelea kuwapo kwa vitendo vya kibaguzi na ubaguzi wa rangi wakati wa michezo hususani michuano ya kimataifa.

Akaeleza kuwa tabia hizo zinakwenda kinyume na dhana ya maudhu inamisingi ya Katiba ya Umoja wa Mataifa na Katika ya Olimpiki. Na hivyo Tanzania inatumia nafasi hiyo kuiomba Jumuiya ya Kimataifa kukemea vitendo hivyo kwa nguvu na kwa kauli moja.

Akagusia pia kwamba pamoja na umuhimu wa michezo katika ujenzi wa taifa na kama moja ya nguzo muhimu katika kuleta Amani,bado mataifa mengi hasa yale yanayoendelea yapo nyuma katika eneo hilo kutokana na sababu mbali mbali zikiwamo za ukoloni.

Awali akizungumza kabla ya kupitishwa kwa Azimio hilo. Rais wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki, Bw. Thomas Bach ,amelitaarifu Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwamba, Kamati hiyo imeamua kuwaalika wakimbizi wenye vipaji vya hali juu kuwa miongoni mwa washiriki 11,000 wanaoshiriki michuano ya Olimpiki mwakani huko Brazil.
 

Amesema wakimbizi hao ambao watashiriki bila ya bendera za nchi zao wala kupigiwa nyimbo za mataifa yao,watakimbia kwa bendera ya Olimpiki na wataimbiwa wimbo wa Olimpiki lengo ni kuwafanya au kuwapatia wakimbizi hao fursa ya kuonyesha vipaji vyao lakini kubwa zaidi kuwaonye sha upendo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni