Ndugu
watanzania wenzetu, tunapenda kuwapongeza kwa kumaliza mchakato wa
kampeni za vyama vya siasa na wagombea kwa amani na utulivu. Vile vile
tunawapongeza kwa kupiga kura kwa kwa amani na utulivu, kwani pamoja na
kujitokeza kwa wingi tulipiga kura kwa kufuata sheria, kanuni na
taratibu za uchaguzi ukiachilia mbali kasoro ndogo ndogo zilizojitokeza
katika zoezi hilo.
Ndugu
watanzania wenzetu, tangu juzi jumapili 25 Oktoba tulianza kupokea
matokeo. Hiyo ni hatua muhimu sana kwa taifa letu, demokrasia yetu na
amani ya nchi yetu. Wote tutakubaliana kwamba nchi nyingi za kiafrika
zimeingia katika machafuko ya kisiasa na kuvuruga amani ya nchi hizo
katika kipindi cha kupokea matokeo.
Nchi
za Ivory Cost iliingia katika mgogoro wa kisiasa kwa wakati wa kupokea
matokeo, ikaingia katika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe maelfu ya
wananchi walipoteza maisha, wengine wakijeruhiwa vibaya na wengi
wakiyakimbia makazi yao.
Mwaka
2007, Nchi jirani ya kenya nayo ilingia katika mgogoro wa kupokea
matokeo na hivyo kusababisha machafuko, watu zaidi ya elfu moja
walipoteza maisha, wengi wakiachwa walemavu na maelfu wakiyakimbia
makazi yao.
Sisi
Global Peace Foundation Tanzania, tunaona mwenendo wa kupokea matokeo
ukianza kuingia dosari, kwa baadhi ya wagombea na wafuasi wa wagombea
kujitangazia matokeo. Ambao kwa Mujibu ka sheria ya uchaguzi ni kinyume,
ni kuvunja kanuni kwani chombo chenye dhamana ya kutangaza matokeo ni
Tume ya Taifa ya uchaguzi pekee.
Kwa
sababu hiyo, tumeona tuwakumbushe wanasiasa na viongozi wa vyama vya
siasa kuwa wakati huu wanapaswa kuwa watulivu na waangalifu pindi
wanapotoa matamko. Kwa kufanya hivyo watakuwa wamewasaidia wafuasi wao
kuwa watulivu na hatimaye kutuvusha katika hatua hii tukiwa na amani na
utulivu.
Tunaisihi
tume ya uchaguzi ya Taifa NEC, na ile ya Zanzibar ZEC, kuharakisha
mchakato wa kutangaza matokeo pindi yanapopatikana na kujumlishwa ili
kuepusha minong’ono na hisia hasi zinazoweza kupandikizwa kwa wapiga
kura na wananchi na baadaye kusababisha machafuko.
Tunakiri
kuwa pamoja na kuwapo migogoro ya hapa na pale, kuwepo kwa viashiria
vya uvunjifu wa amani katika baadhi ya maeneo kama huko Unguja Zanzibar,
baadhi ya maeneo ya Mbeya, Dar es Salaam na Lindi. Bado jeshi la polisi
limeendelea kufanya kazi zake kwa weledi. Hata hivyo tunakisii chombo
hicho kuwa waangalifu zaidi katika kipindi hiki adhimu kwani matumizi ya
nguvu zilizopitiliza yanaweza kuchochea uvunjifu wa amani.
Tunawakumbusha
watanzania wenzetu mashabiki wa vyama vya siasa , wapiga kura na vyama
vya siasa wajiandae kupokea matokeo ya aina yeyote. kwani misingi ya
kidemokrasia inatutaka kuchagua na yule aliyepata kura nyingi ndiyo
anakuwa mshindi.
Na
mwisho ni kwa wanahabari na vyombo vya habari nyie mnabeba dhamana kubwa
kwa taifa hili katika wakati huu muhimu kwa taifa letu. Namna
mtakavyotoa taarifa kwa watanzania ndiyo itakayo amua mustakabali wa
amani na utulivu wa taifa hili.
Mnalo
jukumu na wajibu mahususi katika kuhakikisha kuwa nchi hii inabaki
salama, inabaki na umoja na mshikamano, inabaki na utulivu. Toeni habari
kwa kulingana na matakwa ya taaluma yenu muhimu.
Waswahili
husema, sindano ya daktari huponya na kuua na kalamu ya mwandishi
hujenga ama kubomoa. Kama ilivyo daktari mwema, mwenye maadili huchagua
kuponya na mwandishi makini atachagua kujenga jamii yenye amani, utulivu
na mshikamano kwa kutambua kuwa bila amani hakuna maendeleo.
Tunasimamia
msemo wa watanzania uliopata umaarufu katika wakati huu wa uchaguzi
kuwa KUNA MAISHA BAADA YA UCHAGUZI . Asanteni, Mungu ibariki Africa,
Mungu ibariki Tanzania.
Tafadhali bonyeza hapa chini kusikiliza wimbo maalumu wa kuhamasisha Amani ulioimbwa na Barnaba Boy.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni