TANZANIA
imetimiza ndoto za kutinga hatua ya mwisho ya mchujo kuwania kupangwa
kwenye makundi ya kuwania tiketi ya Fainali za Kombe la Dunia, licha ya
kufungwa 1-0 na Malawi jioni ya leo katika Uwanja wa Kamuzu mjini
Blantyre.
Tanzania inasonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 2-1,
baada ya Jumatano kushinda 2-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika
mchezo wa kwanza wa hatua ya kwanza ya mchujo.
Katika mchezo huo
uliochezeshwa na refa wa Angola, Martins de Carlvalho aliyesaidiwa na
Gadzikwa Bongani wa Zimbabwe na Valdmiro Ntyamba wa Angola, hadi
mapumziko Malawi walikuwa mbele kwa bao hilo 1-0, lilifungwa na John
Banda dakika ya 42 aliyefumua shuti kali akimalizia pasi ya Chiukepo
Msowoya.
Taifa Stars ndio walioanza mchezo huo kwa kasi na
dakika ya kwanza tu, mshambuliaji Mbwana Samatta alikaribia kufunga,
baada ya kumtoka beki Limbikani Mnzava, lakini kipa Simplex Nthala
akaokoa.
Malawi wakajibu shambulizi dakika ya pili baada ya
shuti kali la Banda kupanguliwa na kipa Ally Mustafa ‘Barthez’. Barthez
akafanya kazi nzuri tena dakika ya 10 baada ya kuokoa michomo miwili
mfululizo ya Malawi.
Stars ilizinduka dakika ya 35 baada ya
Thomas Ulimwengu kumtoka vizuri beki wa Malawi Yamikani Fodya baada ya
pasi ndefu ya Samatta, lakini shuti lake likaenda nje sentimita chache.
Kipindi
cha pili, kocha wa Stars, Charles Boniface Mkwasa alianza na
mabadiliko, akimtoa kiungo Said Ndemla na kumuingiza mshambuliaji John
Bocco.
Mabadiliko hayo yaliifanya Stars ianze kudumu kwenye eneo
la Malawi, lakini bado mashambulizi ya hatari yalielekezwa langoni mwa
Tanzania.
Dakika ya 58 Nahodha wa Tanzania, Nadir Haroub
‘Cannavaro’ aliokoa hatari langoni mwake na dakika ya 62 Malawi
walifanya mashambulizi matatu mfululizo ya hatari lanoni mwa Stars,
ikiwemo kupata kona mbili.
Dakika ya 72 Mbwana Samatta alipiga shuti hafifu akiwa karibu na lango baada ya kupokea pasi nzuri ya John Bocco likaenda nje.
Malawi walifanya shambulizi la hatari dakika ya 90, lakini Robin Ngalande akashindwa kumalizia vizuri baada ya kupiga nje.
Kwa matokeo hayo, Taifa Stars sasa itamenyana na Algeria katika mechi za mwisho za mchujo mwezi Novemba.
Kikosi
cha Tanzania; Ally Mustafa ‘Barthez’, Shomary Kapombe, Mwinyi Hajji,
Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Himid Mao, Thomas Ulimwengu,
Said Ndemla/John Bocco dk46, Mudathir Yahya, Mbwana Samatta na Farid
Mussa/Mrisho Ngassa dk75.
Malawi; Simplex Nthala, Stanley
Sanudi, Miracle Gabeya/Robin Ngalande dk76, Yamkani Fadya, Limbikani
Mzava, Gerald Phiri, Chimango Kayira, Micium Mhone, Chiukepo Msowoya,
John Banda na Shumaker Kuwali.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni