Diamond Platnumz akiwa na moja ya tuzo alizoshinda pamoja na mchekeshaji kutoka Nigeria Basketmouth.
Ommy Dimpoz |
Tuzo tatu alizoshinda Diamond Platnumz. |
Inaweza
ikawa siyo mara ya kwanza kwa msanii Diamond Platnumz kuchukua tuzo
mbalimbali za kimataifa lakini kwa Vanessa Mdee inaweza ikawa moja kati
ya historia nzuri kwake huku Ommy Dimpoz akiwa na kila sababu ya
kufurahia tuzo yake ya kwanza ya kimataifa baada ya kujinyakulia tuzo
maarufu za Afrimma.
Wasanii
hao walijinyakulia tuzo hizo usiku wa kuamkia leo huko Dallas, Marekani
ambapo Diamond alichukua tuzo tatu katika vipengele vya Best Dance
Video kupitia wimbo wake wa Nana, Best Male East Africa Artist na Artist
of The Year huku wimbo wa Alive alioshirikiana na Brackets ukichukua
tuzo ya Best Inspirational Song of The Year.
Wakati
huohuo mwanadada, Vanessa Mdee akichukua tuzo ya Best Female East
Africa huku Ommy Dimpoz akichukua tuzo ya Best New Comer na kufanya
Tanzania kukusanya jumla ya tuzo tano.
Washindi
wengine wa tuzo hizo katika vipengele tofautitofauti kutoka nchi
mbalimbali ni kama vile; God Father, AKA, Yemi Alade, Davido, Wizkid na
Yuri.
Hii ni orodha ya washindi.
Best Male (South Africa) – AKA
Best Male (East Africa) – Diamond Platnumz
Best Male (Central Africa) – Yuri Da Cunha
Best Male (West Africa) – Davido
Best Female (East Africa) – Vanessa Mdee
Best Female (West Africa) – Yemi Alade
AFRIMMA Inspirational Song – Bracket feat. Tiwa Savage and Diamond Platnumz for ‘Alive’
Best DJ (US) – DJ Simplesimon
Best Newcomer – Ommy Dimpoz
Best Collaboration – AKA feat. Da Les and Burna Boy for ‘All Eyes on Me’
Best Dance Video – Diamond Platnumz for ‘Nana’
Best Video – Wizkid for ‘Ojuelegba’
Artist of the Year – Diamond Platnumz
Legendary Award – Yossou N’Dou
Na wakati huo huo.....
BASATA LAWAPONGEZA WASANII DIAMOND, VANESSA MDEE NA OMMY DIMPOZ KWA KUSHINDA TUZO ZA AFRIMMA
Baraza
la Sanaa la Taifa (BASATA) likiwa ni msimamizi na mratibu wa sekta ya
Sanaa nchini linapenda kutoa pongezi za dhati kwa Wasanii wa muziki wa
kizazi kipya Nassib Abdul maarufu kama Diamond, Omary Faraji Nyembo
maarufu kwa jina la Ommy Dimpoz na Vanessa Mdee maarufu kwa jina la Vee
Money kwa kushinda tuzo mbalimbali kwenye Tuzo za African Music Magazine
Awards (AFRIMMA) zilizofanyika jijini Dallas nchini Marekani.
Katika
tuzo hizo Msanii Diamond ameshinda tuzo tatu ambazo ni Video Bora ya
Kucheza (Best Dance Video), Msanii Bora wa Mwaka (Best Artist of the
Year) na Msanii Bora wa Kiume wa Afrika Mashariki (Best Male East
African Artist). Aidha Ommy Dimpoz na Vanessa Mdee wameshinda tuzo za
Best New Artist in Africa (Msanii Bora Mpya Africa) na Msanii Bora wa
kike wa Afrika Mashariki (Best Female East African Artist) sawia.
Kuteuliwa
kwa wasanii wetu na baadaye kushinda katika tuzo mbalimbali za Afrika
na duniani ni ishara kwamba wasanii wetu wanakubalika ndani na nje ya
Tanzania na kwamba hawana budi kuhakikisha wanatumia fursa hizi katika
kupanua wigo wa fursa za masoko kitaifa na kimataifa.
Baraza
linatoa wito kwa wasanii na wadau wote wa muziki kuzidisha ubunifu,
nidhamu, bidii, mshikamano na weledi katika kazi wanazozifanya ili
wasanii wengi wa Tanzania waweze kuchomoza katika tuzo na majukwaa
mbalimbali ya kimataifa kwa lengo la kulitangaza Taifa na kukuza soko la
kazi zao.
Ni
matumaini ya Baraza kwamba wasanii wataendelea kutambua umuhimu wa
kufanya kazi na mapromota wenye upeo na mapenzi mema, kufuata Sheria,
Kanuni na taratibu za kutambuliwa na Serikali na zaidi kuhakikisha
wanapokwenda nje ya nchi wanafuata taratibu zote sambamba na kukabidhiwa
bendera ya Taifa kama ishara ya uwakilishi wa Taifa letu.
SANAA NI KAZI TUIKUZE, TUILINDE NA KUITHAMINI
Godfrey Mngereza
KAIMU KATIBU MTENDAJI
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni