BALOZI SEIF AKAGUA KAZI ZA USAFISHAJI WA KARO ZINAZOHUDUMIA UHIFADHI WA UCHAFU KATIKA NYUMBA ZA MAENDELEO, WETE

Kushoto ya Balozi Seif ni Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Mh. Omar Khamis Othman.

                                                                                                  Picha na – OMPR – ZNZ.


Uongozi wa Wizara na Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Kisiwani Pemba kwa kushirikiana na Baraza la Mji wa Wete umeanza matayarisho ya kujiandaa na kazi ya usafishaji wa karo zilizotengwa kuhifadhi uchafu unaotoka katika Nyumba za Maendeleo zilizopo Mtaa wa Mtemani Mjini Wete Kisiwani Pemba.

Kazi hiyo imeanza kwa hatua ya awali ya uchimbaji wa mashimo yatakayotumika kufukia mabaki ya uchafu utakaosafishwa kutoka kwenye Karo Saba zinazohudumia Nyumba hizo zilizojengwa katika miaka ya sabini.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa Kisiwani Pemba alipata fursa ya kukagua hatua iliyofikiwa ya kazi hiyo itakayosaidia kuimarisha hali ya usafi pamoja na utunzaji wa mazingira katika Mtaa huo.

Mkurugenzi wa Baraza la Mji wa Wete Pemba Ndugu Mgeni Othman Juma alimueleza Balozi Seif kwamba Wananchi wa Nyumba za Maendeleo Mtemani Wete wamewahi kujaribu kufanya usafi katika eneo hilo bila ya kupata mafanikio yoyote.

Ndugu Mgeni alisema changamoto zilizowakumba wakaazi hao na kushindwa kukamilisha kazi waliyoamua kuitekeleza zilitokana na ukosefu wa vifaa vya kufanyia kazi ambavyo vinahitaji gharama kubwa.

Naye Afisa Ujenzi Mkoa wa Kaskazini Pemba Ndugu Badru Hamad Hassan alisema kwamba kazi hiyo ingekuwa imeshamalizika kama uwezo wa kifedha ungeruhusu kuwalipa Vijana walio tayari kutekeleza jukumu hilo.

Nd. Badru alisema kazi yote inayohitaji usafishaji wa kina kwenye mashimo ya karo hizo Saba inahitaji jumla ya shilingi Laki saba ambazo kwa hivi sasa tayari Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Pemba imeshatoa ahadi ya kuzitafuta ili kazi hiyo ianze na kumalizika mapema kabla ya kuanza kwa mvua za Vuli.

Akitoa nasaha zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba Nyumba za Maendeleo zilizojengwa katika maeneo mbali mbali ya Visiwa vya Unguja na Pemba zililenga kuwapatia makaazi Bora wananchi wa Visiwa hivi.

Balozi Seif alisema wazo la Taasisi hizo mbili za Umma la kufanya usafi ni zuri kwa vile mbali ya kulinda Afya za Wananchi hasa Watoto wadogo lakini pia litasaidia kuimarisha mazingira mazuri katika eneo hilo la Mji.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwashauri watendaji wanaosimamia nyumba hizo kujitahidi kuweka utaratibu maalum utakaowapa muda maalum wa kufanya ukaguzi wa nyumba hizo ili kujua athari na baadaye kuitafutia ufumbuzi katika kipindi muwafaka.

Ujenzi wa Nyumba za Maendeleo katika Wilaya zote za Visiwa vya Unguja na Pemba uliosimamiwa na Rais wa kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume ulifanywa ili kuwajengea mazingira bora ya Makaazi Wakwezi na Wakulima mara tu baada ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni