KESI YA MWANASIASA ALIYEFUNGWA VICTOIRE INGABIRE YAENDELEA KUSIKILIZWA NA MAHAKAMA YA AFRIKA YA HAKI ZA BINADAMU


picha maktaba
Na Mahmoud Ahmad ,Arusha

MAHAKAMA ya Afrika ya haki za binadamu  iliyoko mjini Arusha , imeamua
kuendelea kusikiliza kesi ya mwanasiasi aliyefungwa  Victoire Ingabire
Umuhoza dhidi ya serikali ya Rwanda, licha ya Rwanda kuamua kufuta Tamko la
kukubalia raia wake kupeleka mashauri kwenye Mahakama hiyo.

Katika hukumu iliyosomwa Mahakamani hapo   na jaji El Haj Guissé kutoka
Senegal kwa niaba ya wenzake, Mahakama inaeleza kuwa serikali ya Rwanda
imechukua uamuzi wa kufuta Tamko baada ya muda mrefu  wakati shauri la
Ingabire ilikuwa imeshawasili mahakamani hapo.

 Mahakama, kwa wingi wa majaji tisa dhidi ya wawili, jaji Agustino
Ramadhani(Tanzania) na Gerard Niyungeko (Burundi) wakiwa wametoa maoni
tofauti, inaona kitendo cha Mlalamikiwa kuondoa Tamko alilofanya kuafuatia
kifungu 44 (6) cha sheria ya Mahakama,  kimekuja miezi kumi na mbili baada
ya shauri kuwasilishwa

. Kwa pamoja, Mahakama imeamua kuwa kuondoa tamko hilo hakuathiri hata
kidogo shauri la mlalamikaji, hivyo Mahakama ina mamlaka ya kuendelea
kulisikiliza» ameeleza Jaji Guissé.

Kwenye Itifaki ya kuunda Mahakama hiyo, sheria inataka nchi wanachama
walioridhia Itifaki hiyo, kutoa Tamko la kuruhusu watu binafsi na Mashirika
yasiyo ya kiserikali (NGOs) kuleta kesi moja kwa moja kwenye Mahakama hiyo,
lasivyo Mahakama haina mamlaka ya kuwasikiliza.

Madame Ingabire aliwasilisha shauri lake tarehe 30 Octoba 2014. Mahakama
ililipokea maana vigezo vyote vilikuwa vimezingatiwa.
Lakini tarehe 1 Machi 2016, siku tatu kabla ya kesi yake kuanza
kusikilizwa, serikali ya Rwanda iliamua kufuta Tamko lake, na hivyo kudai
kuwa kesi hiyo haina budi kutupiliwa mbali.

Mahakama iliagiza pande mbili, yaani serikali ya Rwanda na utetezi wa
Ingabire kuleta hoja zao juu ya aidha kesi kusimama na kufutwa au kuendelea.

Ni baada ya kupitia hoja za pande mbili, ambapo Mahakama imeamuru kesi
kuendelea. Hata hivyo tarehe ya kuendelea kwa kesi haikutajwa.

Katika kesi hiyo, Bi Ingabire anatetewa na wakili Gatera Gashabana kutoka
Rwanda na Dr Caroline Buisman kutoka Uholanzi, wakati serikali
inawakilishwa na Rubango Epimaque kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu nchini
mwake.

Ingabire , anayetumikia kifungu cha miaka 15 nchini Rwanda, analalamikia
serikali ya Rwanda kukiuka haki zake za msingi wakati wa kukamatwa kwake na
kusikilizwa kwa kesi yake kwenye mahakama za Rwanda.

Bi Ingabire Victoire Umuhoza(48) alikuwa nchini Uholanzi akifanya masomo
yake ya elimu ya juu ya Uchumi na Biashara wakati wa mauaji ya kimbari ya
Rwanda mwaka 1994 . Mwaka 2000 aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama RDR
kilichokuwa kikifanyia shughuli zake uhamishoni.

Baadaye aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Muungano wa chama hicho na chama cha
FRD, uliojulikana kwa jina na FDU.
Mwaka 2010, baada ya miaka 17 nje ya nchi, aliamua kurudi Rwanda, kusajili
chama kipya hicho, na baadaye kugombea urais, kupambana na jenerali Paul
Kagame.

Mama huyo lakini hakufikia ndoto zake, maana mapema Februari 2010 alianza
kusumbuliwa na polisi, na baadae Aprili 23, 2010 kutiwa mbaroni na
kushitakiwa kwa makosa mbali mbali ikiwa ni pamoja na kueneza fikra za
mauaji ya kimbari, kuhatarisha usalama wa nchi, na kushirikiana na makundi
ya kigaidi.

 Alihukumiwa kifungo cha miaka minane jela na Mahakama kuu, na baadae miaka
15 na mahakama ya juu.

Uamuzi  wa Mahakama ya Afrika ya kuendelea kusikiliza kesi yake licha ya
Rwanda kufuta Tamko, inayapa njia mashauri ya Wanyarwanda wengine
yaliyowasilishwa mwaka 2015, ikiwa ni pamoja na Kayumba Nyamwasa, Kennedy
Gihana na wengine, Rutabigwa Chrisanthe na Laurent Munyandilikwa

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni