Mkurugenzi
Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa akizungumza leo
jijini Dar es Salaam katika hafla ya kukabidhiana magari tisa yenye
thamani ya Shillingi Millioni mia nane na kumi kutoka Shirika la ICAP
Tanzania kwa ajili ya Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania
utakaofanyika nchi nzima kuanzia mwezi Septemba, 2016. Kushoto kwake ni
Claud Kumalija mwakilishi wa katibu Mkuu wa Wizara Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Mwenyekiti
wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS), Dkt. Fatuma Mrisho akizungumza
leo jijini Dar es Salaam katika hafla ya kukabidhiana magari tisa yenye
thamani ya Shillingi Millioni mia nane na kumi kati ya Ofisi ya Taifa ya
Takwimu na Shirika la ICAP Tanzania kwa ajili ya Utafiti wa Viashiria
na Matokeo ya UKIMWI Tanzania utakaofanyika nchi nzima kuanzia mwezi
Septemba, 2016. Kushoto kwake ni Claud Kumalija mwakilishi wa katibu
Mkuu wa Wizara Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na
kulia kwake ni Dkt. Michelle Roland Mkurugenzi Mkaazi wa Taasisi ya
Marekani ya Kudhibiti Magonjwa – (Centre for Disease Control and
Prevention - CDC).
Mkurugenzi
Mkaazi wa Shirika wa Taasisi ya Marekani ya Kudhibiti Magonjwa –
(Centre for Disease Control and Prevention - CDC) Dkt. Michelle Roland
akikata utepe kuashiria kukabidhi rasmi magari tisa yenye thamani ya
Shillingi Millioni mia nane na kumi kwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa
ajili ya Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania
utakaofanyika nchi nzima kuanzia mwezi Septemba, 2016.
Mkurugenzi
Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa pamoja na
mwakilishi wa katibu Mkuu wa Wizara Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto Claud Kumalija wakionyesha ufunguo wa gari mbele ya
waandishi wa habari na wageni waalikwa kuashiria kupokea magari tisa
yaliyotolewa na Shirika la ICAP Tanzania kwa ajili ya Utafiti wa
Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania utakaofanyika nchi nzima kuanzia
mwezi Septemba, 2016.
Mkurugenzi
Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa akiwasha gari kama
ishara ya kupokea magari tisa yenye thamani ya Shillingi Millioni mia
nane na kumi kutoka Shirika la ICAP Tanzania kwa ajili ya Utafiti wa
Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania utakaofanyika nchi nzima kuanzia
mwezi Septemba, 2016. Hafla ya makabidhiano ya magari hayo imefanyika
leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi
Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa (wa kwanza kulia)
pamoja na wageni waliohudhuria katika hafla ya kukabidhiana magari
wakiangalia baadhi ya magari yaliyotolewa na Shirika la ICAP Tanzania
kwa ajili ya Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania
utakaofanyika nchi nzima kuanzia mwezi Septemba, 2016. Hafla ya
makabidhiano ya magari hayo imefanyika leo jijini Dar es Salaam.
(PICHA ZOTE NA EMMANUEL GHULA)
Na: Veronica Kazimoto.
OFISI
ya Taifa ya Takwimu imekabidhiwa magari tisa aina ya Land cruiser yenye
thamani ya Dola za kimarekani laki nne na elfu tano ($ 405,000) sawa na
Shillingi za kitanzania Milioni mia nane na kumi (810,000,000/=) kutoka
Shirika lisilo la kiserikali la ICAP linaloendeshwa na Chuo Kikuu cha
Columbia nchini Marekani kwa ajili ya Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya
UKIMWI Tanzania utakaofanyika mwezi Septemba, 2016.
Akizungumza
katika hafla ya kukabidhiana magari hayo iliyofanyika leo jijini Dar es
Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dkt. Albina Chuwa
amelishukuru Shirika la ICAP kwa msaada huo ambao utasaidia kupunguza
gharama za kukodi magari kwa ajili ya kufanyia utafiti.
“Napenda
kuchukua fursa hii kulishukuru Shirika la ICAP kwa kutupatia msaada huu
wa magari tisa yenye thamani ya Shillingi milioni mia nane na kumi. Huu
sio msaada mdogo kwani fedha ambazo zingetumika kukodisha magari ya
utafiti, sasa zitatumika katika shughuli nyingine za kimaendeleo,”
amesema Dkt. Chuwa.
Amesema
katika kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), takwimu rasmi
zinahitajika ili kupima utekelezaji wake na hivyo utafiti huu
utakapokamilika utasaidia kutoa takwimu zitakazotumika kupima
utekelezaji wa malengo hayo.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la ICAP Tanzania, Dkt.
Fernando Morales amesema utafiti huu unalenga kupima Viashiria na
Matokeo ya UKIMWI nchini ili kujua ni kwa kiwango gani Tanzania imepiga
hatua katika kupambana na ugonjwa huo.
Dkt.
Morales amesema msaada huu wa magari utasaidia kurahisisha usafiri wa
kutoka eneo moja la utafiti hadi lingine na kuweza kusaidia katika
upatikanaji wa taarifa muhimu za utafiti huu.
Nae
Mkurugenzi Mkaazi wa Taasisi ya Marekani ya Kudhibiti Magonjwa –
(Centre for Disease Control and Prevention - CDC) Dkt. Michelle Roland
amesema kutokana na utafiti huu kufanyika kwa kutumia teknolojia ya
kisasa ya ukusanyaji wa takwimu, kutasaidia kupunguza gharama ambazo
zingetumika kama utafiti huu ungefanyika kwa njia ya kutumia madodoso ya
karatasi.
Ameongeza
kuwa utafiti huu utafanyika kwa kutumia sampuli wakilishi ya kaya
zipatazo 15,800 Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar, na kuwafikia
walengwa wapatao elfu arobaini (40,000) wakiwemo watoto wasiopungua elfu
nane (8,000).
Matokeo
yanayotarajiwa kupatikana katika utafiti huo ni pamoja na taarifa
sahihi kuhusu hali ya maambukizi mapya ya VVU, upatikanaji wa huduma za
tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU hapa nchini na kutambua ni kwa
kiwango gani huduma hizi zimesaidia katika kuudhibiti ugonjwa wa
UKIMWI.
Utafiti
huu wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania utafanywa kwa pamoja na
Shirika la ICAP Tanzania, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto kwa Tanzania Bara, Wizara ya Afya kwa Tanzania Zanzibar,
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali,
Zanzibar (OCGS), Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) na Tume ya
UKIMWI Zanzibar (ZAC).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni