Siku
moja baada ya kifo cha dada wa bilionea Erasto Msuya, Aneth imebainika
kuwa msaidizi wa ndani aliondoka saa sita mchana kwa kuacha funguo
nyumba ya jirani.
Akizungumza nyumbani.
dada
wa marehemu, Mbezi Juu, mama mdogo wa marehemu Lilian Benjamin alisema
msaidizi huyo alimpigia simu bosi wake mchana na kumwambia anaondoka na
hataendelea na kazi.
Alisema
marehemu alilazimika kuomba ruhusa mapema kazini ili arudi nyumbani
kwake Kibada lakini ilimlazimu kukaa nje ya nyumba kwa saa mbili baada
ya kufika saa tisa alasiri na kukuta mlango umefungwa.
Mama
huyo alisema baada ya kusubiri kwa muda aliwauliza majirani wakamweleza
kuwa walipelekewa funguo na mwanafunzi wasiyemfahamu akadai kuwa
alipewa na dada mmoja aliyemuelekeza aipeleke nyumba hiyo.
Haifahamiki mpaka sasa mahali alipo mfanyakazi huyo anayedaiwa kuwa mwenyeji wa Arusha.
Dada mkubwa wa marehemu, Happy Msuya alisema marehemu aliwaeleza mambo hayo baada ya kupigiwa simu na msichana huyo wa kazi.
Dada
mwingine wa marehemu ambaye ni wa nne kuzaliwa kati ya watoto saba wa
Elisaria Msuya, Ester, alisema wauaji hao hawakuwa na nia ya kuiba, bali
ni kuua kwa sababu hawakuchukua kitu chochote zaidi ya televisheni
ambayo nayo waliitupa mbali na nyumbani.
Ester
alisema mara ya mwisho kuonana na marehemu ilikuwa Mei saba
walipokutana benki na mazungumzo yao yalihusu hali ngumu ya maisha.
Alisema hakuwahi kumwambia kama ana ugomvi na mtu kwa sababu alikuwa
mpole na msiri.
Akielezea
tukio hilo alisema inaonekana kulikuwa na purukushani kubwa chumbani
kwa sababu besela la kitanda lilikuwa limevunjika na neti ilikuwa
imetoka, huku nyaraka zikiwa zimepekuliwa na kusambazwa karibu kila kona
ya chumba.
“Walikuja
kuua, kuna kitu walikuwa wanatafuta katika nyaraka pia, ooh... Aneth
umekufa kinyama, umechinjwa kama mnyama,” Ester alishindwa kuendelea na
kuanza kulia na baadaye kidogo alisema wauaji walimkata marehemu koromeo
lakini hawakutenganisha kichwa na kiwiliwili.
Simulizi ya mtoto
Mtoto
wa marehemu mwenye umri wa miaka minne ambaye alikuwa akiishi na mama
yake alisema: “Walikuja watu watano weusi usoni, wakanifanya na kitu
shii usoni, nikalala kwenye kiti mbu wameniuma hadi niliposikia gari la
shule likiita pipii, nikaamka na nikamuamsha mama anivalishe nguo za
shule lakini akakataa kuamka, ”alisema mtoto huyo na kuongeza.
“Nikavaa
mwenyewe nguo za shule na nikamwambia mama nitaendaje shule huku
sijafanya “Home work” lakini mama hakujibu, mbu walining’ata pale kwenye
kochi nilipolala, nikatoka nje nikakuta gari limeshaondoka, nikaenda
kwa mama Salum,” alisema.
Alisema alienda huko akale kwa sababu njaa ilikuwa inamuuma hakula jana yake baada ya ‘wageni’ hao kuja na yeye kulala.
Alieleza
kuwa alipowaambia mama yake hamjibu amelala tu alirudi na dada ambaye
amemsahau jina kutoka hapo kwa mama Salum ambaye alipofika nyumbani kwao
na alipomuona mama yake alianza kupiga kelele.
Ester alisema mwili wa marehemu utasafirishwa Jumatatu ijayo kuelekea kijijini kwao Kairo, Simanjiro mkoani Manyara.
Mtu
wa karibu na familia ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema mbali ya
kaka yao Erasto kuuawa kwa risasi, dada yao Ester akiwa na mumewe
katika Baa ya Hongera, Dar es Salaam alipigwa risasi na kunusurika kufa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni