Waziri Simbachawene awaasa wawekezaji wa madini, mafuta na gesi kushirikiana na jamii zinazowazunguka




Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI Mhe. George Simbachawene akifungua rasmi mkutano wa kikanda kuhusu Leseni za Kijamii za Uendeshaji iliyoandaliwa na Taasisi ya Uongozi mapema leo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujadili namna ambavyo wawekezaji katika sekta ya madini, gesi na mafuta wanaweza wakaongeza uwajibikaji na kupunguza migogoro kati yao na jamii zinazowazunguka katika maeneo yao ya biashara.
Mtaalam wa kimataifa wa Leseni za Kijamii za Uendeshaji Dkt. Ian Thomson, akiwasilisha mada kuu katika mkutano wa kikanda iliyoandaliwa na Taasisi ya Uongozi leo jijini Dar es Salaam kuhusiana na namna ambavyo wawekezaji wa madini, gesi na mafuta wanaweza wakajitahidi kuongeza kiwango chao cha kukubalika na kupunguza migogoro kati yao na jamii zilizopo katika maeneo yao ya uwekezaji.

Makamu wa Rais Mwandamizi wa kampuni ya uchimbaji madini ya Acacia Mining Plc Bw. Deodatus Mwanyika (kulia) akichangia mjadala katika mkutano wa kimataifa wa kikanda kuhusu Leseni za Kijamii za Uendeshaji iliyoandaliwa na Taasisi ya Uongozi mapema leo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujadili namna ambavyo wawekezaji katika sekta ya madini, gesi na mafuta wanaweza wakaongeza uwajibikaji na kupunguza migogoro kati yao na jamii zinazowazunguka katika maeneo yao ya biashara. Kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa TCME Balozi Ami Mpungwe, Mwezeshaji wa mkutano huo Bw. Aidan Eyakuze na Mbunge na Mwenyekiti wa Fedha ya Bunge kutoka nchini Ghana Mhe. James Avedzi.

Mwenyekiti wa McAlister Consulting Corporation na Balozi mstaafu wa Canada nchini Tanzania Balozi Andrew McAlister akizungumzia uzoefu wake kuhusiana na uwekezaji na uwajibikaji wa kampuni za madini, gesi na mafuta katika mkutano wa kikanda iliyoandaliwa na Taasisi ya Uongozi leo jijini Dar es Salaam yenye malengo ya kupunguza migogoro kati ya kampuni hizo na jamii zilizopo katika maeneo yao ya uwekezaji.
Maafisa waandamizi wa serikali, sekta binafsi, taasisi zisizo za kiserikali na taasisi za elimu wakishiriki mkutano wa kikanda kuhusu Leseni za Kijamii za Uendeshaji iliyoandaliwa na Taasisi ya Uongozi leo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujadili namna ambavyo wawekezaji katika sekta ya madini, gesi na mafuta wanaweza wakaongeza uwajibikaji na kupunguza migogoro kati yao na jamii zinazowazunguka katika maeneo yao ya biashara.


Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais anayeshughulika na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mh. George Simbachawene (Mb) ameasa wawekezaji katika sekta ya madini, mafuta na gesi kushirikiana na jamii zinazozunguka maeneo yao ya uwekezaji ili kuweza kutunza amani, utulivu na kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini na bara la Afrika kwa ujumla.

Waziri huyo alitoa rai hiyo katika mkutano wa siku moja ya kikanda uliondaliwa na Taasisi ya Uongozi kuhusiana na ‘Leseni za Kijamii za Uendeshaji’. Leseni za Kijamii za Uendesheji ni dhana ya kitaalam inayohusiana na kiwango cha kukubalika kwa kampuni za madini, mafuta na gesi kwa jamii zinazowazunguka katika maeneo yao ya uwekezaji.

“Migogoro kati ya wawekezaji wa madini, gesi na mafuta na jamii yana madhara mbalimbali ikiwemo ya kifedha, kiutendaji, na kitaswira kwa kampuni husika. Migogoro ya aina hii yakipuzwa madhara yake ni makubwa, na ni kwa sababu hii hii kampuni katika sekta hii zinapaswa kufanya bidii zaidi katika kuhakikisha kwamba shughuli zao za uwekezaji haziwakeri watu,” alisema Simbachawene.

Aliendelea, “Majadiliano na mashauriano katika ngazi ya wananchi yanaweza yakaleta suluhu katika maeneo mbalimbali ikiwemo katika ulipwaji wa fidia, utoaji wa misaada kwa jamii, na utolewaji wa kazi mbadala kwa baadhi ya wananchi ambao wamekoseshwa kazi kutokana na shughuli za kiuwekezaji.”

Waziri huyo pia alisisitiza dhamira ya serikali katika kugatua madaraka kutoka katika serikali kuu ili kuwawezesha ushirikishwaji wa wananchi kuwa wa urahisi zaidi, yenye uwazi na usawa.

“Kwa kufanya hivyo, tutakuwa tuna uwezo wa kuongeza idadi ya wawekezaji katika sekta tofauti, na kujenga amani, utulivu na maendeleo katika jamii za wananchi,” Waziri alisema.

Kwa upande wake, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Bw. Dennis Rweyemamu alisema kwamba taasisi hiyo iliandaa mkutano huo ili kuweza kufahamu changamoto za kujenga mahusiano kati ya wawekezaji wa sekta ya madini, mafuta na gesi na jamii zinazowazunguka, pamoja na kutafuta namna bora za kukuza mahusiano hayo.

“Kampuni katika nchi nyingi sana, hususan katika nchi zinazoendelea, yamewekeza mamilioni ya madola katika kutoa misaada ya kijamii, lakini bado yanakutana na pingamizi kutoka kwa wananchi katika maeneo waliyowekeza,” alisema Rweyemamu.

Aliendelea, “Mkutano huu unalenga kujenga uelewa wetu ya namna Leseni za Kijamii za Uendeshaji zinapatikana na kukuzwa, kupitia uzoefu wa Tanzania katika dhana hii, na kujifunza pia kutoka katika nchi ambazo zimefanikiwa na zingine ambazo zilijaribu lakini hazijafanikiwa.”

Mkutano huu wa siku moja imekusanya wadau zaidi ya mia moja kutoka nchini Tanzania na barani Afrika wanaofanya kazi katika serikali, sekta binafsi, taasisi zisizo za kiserikali na taasisi za elimu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni