WASIMAMIZI WA UCHAGUZI SINGIDA: Watakiwa kusimamia shughuli zao kwa kuzingatia Haki, Uadilifu na kutopendela chama!

SAM_0215 Mkuu wa wilaya ya Singida,Bwana Saidi Amanzi(aliyesimama) akifungua semina ya siku mbili kwa wasimamizi 42 kutoka jimbo la Singida kaskazini.(Picha  zote  na Jumbe Ismailly).
Na. Jumbe Ismailly
[SINGIDA] MKUU wa Wilaya ya Singida,Saidi Amanzi amewaagiza wasimamizi wa uchaguzi wa wilaya hiyo kuhakikisha wanakwenda kusimamia shughuli za uchaguzi kwa kuzingatia haki,uadilifu,bila upendeleo na kwa kutoegemea upande wowote.
Mkuu wa wilaya huyo alitoa agizo hilo kwenye ufunguzi wa semina ya siku mbili kwa wasimamizi wa uchaguzi 42 wa Halmashauri ya wilaya ya Singida iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo.
“Kwa nafasi yenu mna dhamana kubwa,mnapaswa kufanya kazi yenu kwa uangalifu wa hali ya juu bila upendeleo,bila kuegemea upande wowote,mtende haki kuyahakikishia mataifa mengine kwamba Tanzania tunaweza tukafanya mambo yetu wenyewe kwa uwazi,kwa usalama bila upendeleo wowote na mambo yetu ya uchaguzi mwaka huu yapite bila malalamiko yeyote”alisisitiza Amanzi.
Alisisitiza mkuu huyo wa wilaya kuwa dhamana hiyo ya kuhakikisha hakutokei malalamiko baada ya kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu ujao ipo mikokononi mwao,na endapo watafanya kinyume watakaotia doa kwenye uchaguzi huo ni wao wasimamizi wa uchaguzi huo.
“Lakini naamini ninyi ni watu wazima,mtaapa kwa hiyo mtazingatia viapo vyenu,mzingatie viapo vyenu na muwe waaminifu kweli kweli na mfanyekazi vile ambavyo inatakiwa kufanywa kwa mujibu wa maelekezo ya tume ya uchaguzi na siyo vinginevyo”alifafanua
Hata hivyo Amanzi alitumia fursa hiyo kuwatahadharisha wasimamizi hao kutoegemea chama chochote kile cha siasa,wasiegemee wagombea na badala yake watende haki kwa kila mgombea wa chama cha siasa na wanapokuwa kwenye vituo vyao wasisite kumtanguliza mungu kwenye shughuli zao.
“Mimi mwenzenu hapa ni kada wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) kilichonileta nikafikia kuwa mkuu wa wilaya ni ukada wangu wa Chama Cha Mapinduzi wala siyo kitu kingine,lakini kama alivyo rais yeye amechaguliwa na wananchi wote na hivyo anakuwa raisi wa watu wote”alisisitiza huku akiwakodolea macho waandishi wa habari.
Katika hatua nyingine mkuu wa wilaya huyo hakusita kuwatupia tuhuma wawakilishi wa kituo cha sheria na haki za binadamu kuwa wanapokuwa kwenye shughuli hizo za uchaguzi wamekuwa wakiangalia zaidi makosa ya serikali na kuyapa mgongo mazuri yote yanayofanywa na serikali.
Awali afisa uchaguzi katika jimbo la Singida kaskazini,Joseph Sabore alisema kuwa semina hiyo ya siku mbili inawashirikisha watu 42 kutoka katika kila kata washiriki wawili.
Kwa mujibu wa Sabore ambaye pia kitaaluma ni afisa maendeleo ya jamii wa wilaya hiyo madhumuni ya semina hiyo ni kuwapatia mafunzo na maelekezo kwa ajili ya kuwawezesha wasimamizi ngazi ya kata ili wakasimamie vizuri shughuli za uchaguzi katika maeneo yao.
SAM_0211
SAM_0212
SAM_0213
Pichani chini na juu ni  baadhi ya washiriki wa semina ya siku mbili kwa wasimamizi wa uchaguzi mkuu wa Rais,Wabunge na Madiwani wa jimbo la Singida kaskazini unaotarajiwa kufanyika Okt, 25,mwaka huu wakiwa kwenye ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya wilaya ya Singida wakimsikiliza mtoa mada(hayupo pichani) jana.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni