MTANDAO WA WATETEZI WA HAKI ZA BINADAMU WAENDESHA MAFUNZO NA KUTOA MAJAKETI MAALUM KWA WAANDISHI WA HABARI ZANZIBAR

1
Makamu Mwenyekiti wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania THRDC(katikati) Harusi Mpatani akionesha Mfano wa Jacketi ambazo wamezitoa msaada kwa Wanahabari wa Zanzibar kupitia Jumuiya ya Waandishi wa habari Zanzibar ZPC,Mwenye Kipaza Sauti ni Mkurugenzi wa THRDC Onesmo Olengurumwa na Salma Said Mdau wa THDRC Mafunzo na Makabidhiano hayo yamefanyika katia Ukumbi wa Hoteli ya Grand Palace mjini Zanzibar.
2
Makamu Mwenyekiti wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania THRDC Harusi Mpatani, Mkurugenzi wa THRDC Onesmo Olengurumwa na Salma Said Mdau wa THDRC wakimkabidhi Jacketi za Waandishi Katibu wa Zanzibar Press Club (ZPC) Faki Mjaka. Jacketi hizo ni msaada ambazo wamezitoa kwa Wanahabari wa Zanzibar kupitia Jumuiya hiyo. Makabidhianao hayo yanaendana na Mafunzo ya siku tatu kwa Waandishi wa Habari wa Zanzibar kuhusu Ulinzi na usalama katika kuandika habari za uchaguzi huko Ukumbi wa Hoteli ya Grand Palace mjini Zanzibar
3
Afisa kutoka Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania Benedict Ishabakaki akitoa mafunzo hayo kwa Waandishi wa Habari wa Zanzibar hawapo pichani kuhusu Ulinzi na usalama katika kuandika habari za uchaguzi huko Ukumbi wa Hoteli ya Grand Palace mjini Zanzibar.

                                                                                      Picha kwa hisani ya THDRC


Na Faki Mjaka- Maelezo Zanzibar

MAKAMO Mwenyekiti wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) Harusi Miraji Mpatani amewataka waandishi wa habari nchini kuzingatia usalama wao wakiwa kazini ili kujiepusha na madhara wanayoweza kuyapata.

Amesema kutokana na umuhimu wa wanahabari katika jamii wamekuwa ni miongoni mwa makundi ya watu wanaowindwa hivyo kuna umuhimu mkubwa kwao kuzingatia usalama wao wakati wote.

Harusi ameyasema hayo wakati akifungua Warsha ya siku tatu kwa waandishi wa habari wa Zanzibar kuhusu ulinzi na Usalama wakati wa kuandika habari za Uchaguzi yaliyofanyika leo katika ukumbi wa hoteli ya Grand Palace Malindi mjini Unguja.

Harusi ambaye pia ni Mkurugenzi mtendaji wa kituo cha huduma za sheria Zanzibar (ZLSC) alisema umuhimu wa kundi hilo kijamii unatokana na kuhitajiwa na makundi mengine ya kijamii katika kuwapasha habari na matukio mbali mbali.

“Jamii inawategemea nyinyi kuweza kuwafikishia yale ambayo mnayapata kutoka kwa watu au viongozi wawe wa kisiasa au kijamii, sasa kuna wakati taarifa hizo huwa haziwafurahishi watu wanaozitoa au kuhuisika nazo hivyo mafunzo haya yamelenga kuwakumbusha wajibu wenu lakini pia kuwapa uelewa wa kuzingatia usalama wenu kuwa ni jambo la muhimu kuliko hata hiyo habari”, alisema Mpatani.

Aidha aliwataka waandishi hao kujitambua na kutumia vyema kalamu zao na kutoandika habari zitakazo ibua hamasa kwa wananchi ili kuepusha vitendo vya uvunjifu wa amani.

“Mtandao mbali ya kukutana na waandishi, tumeyafikia makundi mengine ya kijamii kwa lengo kuhakikisha uchaguzi wa mwaka huu unakuwa huru na wa haki ili kuhakikisha nchi inabaki kuwa na amani kabla na baada ya uchaguzi”, alisema Mpatani.

Mapema akitoa maelezo ya juu ya namna ya mtandao huo unavyowawezesha waandishi wa habari nchini, Mratibu wa mtandao huo Onesmo Olengurumwa alisema mbali na mafunzo hayo pia mtandao huo umetoa Majaketi maalum yatakayowatambulisha wakati wakiwa kazini ili kuwaepusha kuchanganywa na watu wengine wakati wa machafuko ya kisiasa.

Alisema katika warsha hiyo waandishi watapatiwa mafunzo juu ya namna ya kujilinda na kuepuka kuwa chanzo cha madhara miongoni mwao na jamii wanayoitumikia.

“Mafunzo haya kama ilivyokuwa kwa yale yaliyotangulia kwa watendaji wa jeshi la polisi ni muendelezo wa shughuli za mtandao wetu ambazo unalenga katika kuibakisha Tanzania katika hali ya amani na utulivu na kuwafanya waandishi kutekeleza majukumu yao kwa uhuru zaidi”, alisema Olengurumwa.

Aidha aliwataka waandishi kuzingatia maadili ya kazi zao na kuvibaini viashiria vya hatari zinazoweza kuwatokea katika utendaji wa kazi zao katika uchaguzi mkuu ujao ili kuziepuka.

“Mtakapozijua hatari zinazowazunguka katika utendaji wa kazi zenu mtaweza kujikinga na kuepusha athari za moja kwa moja kwenu nyinyi au taifa kwa ujumla na ndio maana tumeamua kutoa haya majaketi ambayo yanaweza kuwapambanua na watendaji wengine wakati wa kutekeleza majukumu yenu”, alisema Olengurumwa na kuwataka wamiliki wa vyombo vya habari nchini kuwawezesha watendaji wao kwa kuwapatia vitendea kazi hivyo.

Nae Mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari wa Zanzibar (ZPC) Abdallah Abrahamani Mfaume aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kufuatilia kwa makini mafunzo hayo ili yawasaidie kuleta ufanisi katika utendaji wa kazi zao za kila siku.

Alisema wakati huu wakati nchi ikielekea katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu, jamii ya wanahabari imekuwa ikikabiliwa na changamoto nyingi hivyo kuna umuhimu mkubwa kwao kuzingatia misingi ya taaluma yao.

“Ni lazima tukumbuke kuwa kuna maisha baada ya uchaguzi hivyo ni lazima tujikite katika kufuata maadili ya kazi zetu na kuepuka kufanya kazi kwa upendeleo badala yake tujikite katika kutenda haki”, alitoa rai hiyo Mfaume ambayo pia iliungwa mkono na naibu katibu mkuu wa klabu ya waandishi wa habari ya Pemba (PPC) Ali Mbarouk Omar.

Mbarouk alisema kuna haja kubwa ya waandishi kuacha ushabiki na kujikita kuandika habari zitakazowasaidia wananchi kufanya maamuzi kwa kyuchagua kiongozi atakayewafaa badala ya kuandika habari zitakazowaongoza kufanya maamuzi yasiyo sahihi au kuwachanganya.

“Katika kipindi kama hiki kwa kiasi kikubwa vyombo vya habari vinakuwa na mkanganyiko wa kimaadili lakini sisi tunaopata elimu hii ni vyema tuitumia vizuri na kuwakumbusha wenzetu waliobaki kuzingatia wajibu wetu kwa jamii ili kujiepusha na madhara na hatari dhidi ya usalama wetu”, alifafanua Mbarouk.

Aidha aliipongeza taasisi hiyo na kuahidi kuwa majaketi waliyopatiwa watayatunza na kuyatumia kwa malengo yaliyokusudiwa na kuwataka waandishi wengine kujitokeza kujiunga na klabu hizo ili kuunganisha nguvu zao.

Katika warsha hiyo jumlaya waandishi 30 kutoka unguja na pemba watapatiwa mafunzo na miongozo mbali mbali itakayowawezesha kuepuka hatari mbali mbali zinazowakabili wakati huu wa kampeni na baadae katika uchaguzi mkuu ujao ambayo yameandaliwa kwa pamoja kati ya mtandao huo na klabu za waandishi wa habari za Unguja (ZPC) na Pemba (PPC) ambapo kwa upande wa Tanzania bara jumla ya waandishi 150 wa mikoa mbali mbali wamepatiwa mafunzo hayo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni