BALOZI SEIF AAGIZA WATUMISHI WA UMMA WANAOJIINGIZA KATIKA SIASA WACHUKULIWE HATUA MARA MOJA


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Viongozi wa Halamshauri za CCM Mikoa ya Kusini na Kaskazini Pemba kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Makonyo Wawi Chake chake akiwapa pole kutokana na hujuma mbali mbali walizofanyiwa wafuasi wao baada ya kumalizika kwa uchaguzi. Kulia ya Balozi Seif ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Pemba Mzee Mberwa Hamad Mberwa na kushoto ya Balozi Seif ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ Mh. Haji Omar Kheir.
Baadhi ya Viongozi wa Halamshauri za CCM Mikoa ya Kusini na Kaskazini Pemba wakimsikiliza Balozi Seif hayupo pichani kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Makonyo Wawi Chake chake Pemba.
Balozi Seif akizungumza na Wananchi mbali mbali waliopata mitihani ya kuhujumiwa kwa kupigwa na kuvurugiwa mali na mazao yao Kisiwani Pemba aliokutana nao kuwapa pole hapo katika Ukumbi wa Tasaf Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Chake chake Pemba.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wa Tatu kutoka kulia akikatisha ziara yake kwa muda mfupi na kujumuika pamoja na Wazee wa Kijiji cha Wawi katika kumuombnea Dua Marehemu Dr. Omar Ali Juma aliyewahi kuwa Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wa kwanza kutoka kulia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala wa Mikoa na Idara Maalum za SMZ Mh. Haji Omar Kheir pamoja na Viongozi na Maafisa walioshiriki ziara hiyo ya siku Tatu Kisiwani Pemba.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akimaliza ziara yake ya Siku Tatu Kisiwani Pemba kwa kuukagua Msikiti Mpya wa Ijumaa Unaojengwa sambamba na jengo la Madrasa katika Kijiji cha Liko Kuu Chokocho Wilaya ya Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba. Kulia ya Balozi Seif ni Mkuu wa Wilaya ya Mkoani Ndugu Hemed Suleiman Abdullah aliyemkaguza Msikiti huo na kuridhika kwa hatua iliyofikiwa ya ujenzih. Picha na – OMPR – ZNZ.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuwachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kuwasimamisha kazi mara moja Watumishi wa Umma wanaoonekana kuchukuwa mawazo ya baadhi ya Viongozi wa Kisiasa wakati wakitekeleza majukumu yao.

Alisema haiwezekani kwa mtumishi wa Umma akaachwa aendelee kufanya anavyotaka hasa katika kuwatumikia wananchi kwa njia za unyanyasaji au ubaguzi huku akiendelea kula mshahara wa Serikali bure unaotokana na jasho la Wananchi anaowanyanyasa.

Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akizungumza na Viongozi wa Halmashauri za CCM za Mikoa miwili ya Kusini na Kaskazini Pemba hapo katika ukumbi wa Makonyo Wawi pamoja na ule wa kuwapa Pole wananchi waliopatwa na mikasa ya kufanyiwa hujuma mara na baada ya uchaguzi mkuu hapo Ukumbi wa Tasaf Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Chake chake Pemba.

Balozi Seif alisema taratibu za kuwafukuza watumishi waliosimamishwa na watakaosimamishwa kazi kwa mujibu wa kanuni, taratibu na sheria za Utumishi Serikalini zitafuata hapo baadaye kwa wale watakaoshindwa kubadilika kutokana na vitendo vyao vilivyo nje ya maadili yao ya kazi.

Alieleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haiwezi kuvumilia maovu ya watu na hata mtu mmoja atakayoyafanya dhidi ya Serikali na wananchi akiyatolea mfano matendo ya utengwaji kwa baadhi ya wananchi katika kupatiwa huduma muhimu za kijamii kama usafiri wa baharini, bara barani na zile za kibiashara kwa kuuza au kununua.

Aliwapongeza Viongozi hao wa Halmashauri za CCM Mikoa ya Kusini na Kaskazini Pemba pamoja na wanachama wao kwa kazi kubwa waliyoifanya mwezi Oktoba mwaka 2015 na baadae kuimalizia mwezi machi mwaka huu ya kuipa uwezo CCM kuendelea kuongoza Dola ya Tanzania kwa pande zote mbili za Muungano.

Hata hivyo alitahadharisha kwamba Serikali inaelewa kwamba hali ya Pemba bado si nzuri. Hivyo kupitia vyombo vyake vya dola italazimika kuimarisha zaidi ulinzi ili kuwapa fursa pana wananchi mbali mbali waendelee kupata fursa na uwezo wa kuishi kwa amani, utulivu na upendo miongoni mwao,.

Balozi Seif alisema cheche za shari na uvunjifu wa amani zinazofanywa Kisiwani Pemba zina dhamira ya wazi ya kutaka jamii ya Kimataifa iione Zanzibar iko katika vurugu kubwa zilizosababishwa na matokeo ya uchaguzi wa mwezi wa oktoba uliofutwa kutokana na sababu mbali za udanganyifu.

Alifahamisha kwamba mfumo wa vyama vingi vya kisiasa Barani Afrika ikiwemo Zanzibar bado una safari ndefu na hili limethibitishwa wakati wa kura ya maoni ya kuulizwa wananchi mfumo wanaouhitaji ambapo asilimia 80% ya Watanzania walikataa vyama vingi na asilimia 20% ndio iliyotaka mabadiliko hayo.

Akizungumzia wananchi waliopatwa na mitihani ya kufanyiwa hujuma mara na baada ya uchaguzi mkuu Balozi Seif alisema Serikali Kuu inafikiria kuangalia namna itakavyoweza kuwasidia wananchi waliohujumiwa mali, vifaa na vipando vyao.

Mapema Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum ya SMZ Mh. Haji Omar Kheir aliwapongeza Wakuu wa Mikoa na Wilaya za Pemba kwa hatua wanazochukuwa za kusimamia utendaji wa Serikali katika maeneo yao.

Mh. Haji alisema usimamizi imara wa Viongozi hao hasa katika kuwasaidia wananchi waliopatwa na mitihani ya kufanyiwa hujuma sambamba na kuanza hatua za kuwachukuliwa wahusika waliosababisha kuibuka kwa vitendo hivyo vya uvunjifu wa amani unapaswa kuungwa mkono na jamii yote.

Alisema matokeo mengi ya hujuma, uvunjifu wa amani pamoja na vitisho wanavyofanyiwa wananchi wasio na hatia bado udhibiti wake uko chini ya dhamana na usimamizi wa Wakuu hao wa Mikoa na Wilaya ambapo Serikali kuu inabaki kuwa kama mratibu wa utekelezaji huo.

Waziri Haji alisisitiza kwamba haipendezi hata kidogo kuona maamuzi ya masuala madogo yaliyo chini ya dhamana ya Viongozi hao yasubiri kuamuliwa au kuchukuliwa hatua zinazofaa na Rais wa Zanzibar pamoja na msaidizi wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Wakielezea changamoto na matatizo yaliyowakumbwa Viongozi wa CCM wa Mikoa Miwili ya Kusini na Kaskazini Pemba pamoja na Wananchi waliokumbwa na hujuma tofauti walisema hali ya amani katika maeneo mbali mbali ya kisiwa cha Pemba ilikua tete kiasi kwamba maisha ya baadhi ya wafuasi wa kisiasa yalikuwa hatarini.

Walisema elimu ya takwa inapaswa kuandaliwa ili isaidiwe watu waliojitoa mshipa wa fahamu na kuamua kufanya vitendo visivyostahiki kufanywa na binaadamu mwenye akili timamu ambavyo vimepindukia mipata ya imani za Kidini.

Waliiomba Serikali Kuu kupitia vikosi vyake vya ulinzi kupanga mipango maalum ya kuimarisha hali ya ulinzi na hata kuweka utaratibu wa kufanya diroa kwa maeneo yenye cheche za kuendelezwa shari na hujuma ili kuwarejeshea wananchi walio wengi imani ya kuendelea kufanya shughuli zao kama kawaida.

Walionyesha kuridhika kwao na hatua zilizochukuliwa na Serikali ya kuimarisha ulinzi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba mwaka 2015 na ule uliofuatiwa wa marejeo wa mwezi Machi mwaka huu lakini hatua hizo kwa sasa zimefifia kiasi cha kutoa mwanya kwa makundi ya wahalifu kujifanyia wanavyotaka.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alikuwa Kisiwani Pemba kwa ziara ya siku Tatu kujionea hali halisi ya athari ya hujuma za makusudi zilizofanywa na baadhi ya wafuasi wa Kisiasa.

Hujuma hizo zimewakumba wananchi kadhaa na kupelekea kupata majeraha na wengine kulzwa Hospitali wakipatiwa matibabu kutokana na vitendo hivyo pamoja na baadhi yao kuvurugiwa kwa makusudi mali na mazao yao na kuwachwa na hatari ya umasikini utakaochukuwa muda mrefu.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
22/5/2016.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni