Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt. James Jesse akitoa mada mbele ya
waandishi wa habari kuhusu Mpango wa Kimataifa wa Kujitathmini juu ya
Masuala ya Haki za Binadamu (UPR) wakati wa warsha ya siku moja 29
Aprili 2016 Mkoani Morogoro.
Afisa
Utetezi na Haki za Binadamu wa Shirika la Under The Same Sun (UTSS) Bi.
Perpetua Senkoro akitoa mada kuhusu masuala ya watu wenye ulemavu
kupewa haki zao wakati warsha ya siku moja kuhusu Mpango
wa Kimataifa wa Kujitathmini juu ya Masuala ya Haki za Binadamu (UPR)
wakati wa warsha ya siku moja 29 Aprili 2016 Mkoani Morogoro.
Wadau
wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora wakiwa katika picha ya
pamoja na Waaandishi wa Habari waliohudhuria mafunzo ya siku moja ya
warsha kuhusu Mpango wa Kimataifa
wa Kujitathmini juu ya Masuala ya Haki za Binadamu (UPR) wakati wa
warsha ya siku moja 29 Aprili 2016 Mkoani Morogoro.
(Picha zote na Benedict Liwenga)
Na Benedict Liwenga.
Asasi
za Kiraia pamoja na Taasisi za kutetea haki za binadamu nchini
zimewaasa Waandishi wa Habari nchini kujikita katika kuhabarisha umma
kuhusiana na masuala ya haki za binadamu ikiwemo mauaji ya watu wenye
ualbino, mauaji ya vikongwe, ukatili dhidi ya watoto, pamoja na adhabu
ya vifo.
Rai
hiyo imetolewa leo na Kamishna wa Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bi.
Salma Ally Hassan wakati wa Warsha ya siku moja iliyofanyika mkoani
Morogoro yenye lengo la kuwajengea uelewa Wanahabri kuhusu Mpango wa
Kimataifa wa kujitathmini juu ya Masuala ya Haki za Binadamu (UPR).
Bi.
Salma ameeleza kuwa kutokana na tathmini ya masuala ya haki za binadamu
nchini, vyombo vya habari havinabudi kuwa na uelewa mkubwa kuhusu
umuhimu wa kuziongelea haki za binadamu kwani jamii imekuwa haizitambui
baadhi ya haki hizo na kumekuwepo na kukithiri kwa vitendo vya uvunjifu
wa amani yakiwemo matukio ya mauaji ya watu wenye ualbino, vikongwe
pamoja na ukatili kwa watoto.
Ameongeza
kuwa, baadhi ya watu nchini wamekuwa wakijichukulia sheria mkononi kwa
kuua watu ambapo watu wenye kuyasemea hayo ni Vyombo vya Habari lengo
likiwa ni kukemea kuendelea kwa vitendo hivyo.
“Uvunjaji
wa haki za binadamu unafanywa na watu katika jamii, kwa mfano, mauaji
ya Watu wenye Ualbino, mauaji ya vikongwe, pale sio Serikali inakua
imevunja haki za binadamu, bali ni watu katika jamii”, alisema Bi.
Salma.
Kwa
upande wake Mshauri wa masuala ya haki za binadamu kutoka Ofisi ya
Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Bi. Chitralekha Massey ameeleza kuwa,
ni vema Tanzania ikakubalina na mapendekezo yanayohusiana na masuala ya
haki za binadamu yanayoendana na Dunia kwa ajili ya ulinzi wa haki hizo.
“Sisi
kama Umoja wa Mataifa tunapenda kuona Tanzania inafanya uamuzi
utakaosaidia kuboreshwa kwa haki za binadamu nchini kwani ni wakati sasa
wa jamii kusema kwa uwazi kuwa mapendekezo hayo yatakuwa yenye manufaa
kwao”, alisema Massey.
Aidha,
katika warsha hiyo, vyombo vya habari, jamii pamoja na Serikali
wanajukumu la kulinda haki za binadamu na kuendelea kukemea matukio
yanayovunja amani katika jamii.
Tarehe
9 Mei, 2016 Tanzania inatarajiwa kufanyiwa tathmini ya pili juu ya hali
ya haki za binadamu nchini na Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa ambapo
tayari Asasi za Kiraia na Watetezi wa haki za binadamu wamekwisha
wasilisha mapendekezo yao kwa Wawakilishi wa nchi wanachama wa umoja
huo.
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni