Wajumbe
wa Baraza la Vyama vya Siasa Nchini ambalo linaundwa na wawakilishi
wawili kutoka kila chama cha siasa chenye usajili wa kudumu wamekutana
mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa mikutano wa GEPF uliopo Victoria
Jijini Dar es salam kujadili mapendekezo ya mfumo wa utatuzi wa migogoro
ya ndani na baina ya vyama vya siasa .
Mapendekezo
hayo yalitolewa na Mtaalamu wa utatuzi wa Migogoro Bw. Ghalib Galant
ambaye awali alifanya utafiti wa utatuzi wa migogoro ya ndani na baina
ya vyama vya siasa nchini chini ya usimamizi wa Ofisi ya Msajili wa
Vyama vya Siasa na kwa udhamini wa UNDP kupitia mradi wake wa
“Democratic Project” ukiwa na lengo la kuiboresha sura namba 258 ya
Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992 ili kuendana na mahitaji ya
ukuaji wa demokrasia nchini. Utafiti huo ulishirikisha wadau mbalimbali
wa demokrasia ya vyama vingi nchini vikiwemo vyama vya siasa.
Akiwasilisha
mapendekezo, Msajili Msaidizi Bi. Piencia C. Kiure ,alisema kuwa
ilipendekezwa kuwa Sheria ya Vyama vya Siasa nchini iweke masharti
yanayohusu utaratibu wa kutatua migogoro ndani na baina ya vyama vya
siasa “ migogoro ndani ya chama ni lazima ishughulikiwe kwanza ndani ya
chama cha siasa na kufikia tamati kwa mfumo wa utatuzi wa migogoro
uliowekwa kwa mujibu wa katiba ya chama, kabla ya kuwasilishwa katika
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa ajili ya upatanishi”
ilikaririwa sehemu ya mapendekezo
“Upatanishi
ukishindikana mgogoro husika uwasilishwe kwenye Baraza la Uamuzi la
Migogoro ya Vyama vya Siasa kwa uamuzi. Ikiwa muhusika wa mgogoro
asiporidhika na uamuzi wa Baraza la Uamuzi wa migogoro ya vyama vya
siasa atawasilisha mgogoro husika Mahakama Kuu mbele ya Majaji watatu
kwa mapitio ya uamuzi wa Baraza. Muhusika asiporidhika na uamuzi wa
Mahakama Kuu, atakata rufaa Mahakama ya Rufaa” ilifafanua sehemu ya
Mapendekezo.
Aidha
kumekuwa na msisitizo wa kufuata mtiririko wa hatua katika utatuzi wa
migogoro kama ilivyobainishwa hapo juu ili kuepusha migogoro ndani ya
vyama kwenda moja kwa moja Mahakamani ambako huchukua muda mrefu na
kuathiri ukuaji wa demockaria ndani na nje ya vyama vya siasa hapa
nchini.
Wakichangia
katika mjadala huo, baadhi ya wajumbe walikubaliana na hoja kuwa vyama
vya siasa vitatue kwanza migogoro yake ndani ya vyama na kwamba pale tu
itakaposhindikana ndipo ipelekwe kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya
Siasa.
Wajumbe
walishindwa kukubaliana katika hoja ya uwepo wa Baraza la Uamuzi wa
Migogoro ya vyama vya siasa, wapo walioona haja ya uwepo wake na wapo
walipendekeza kuwa majukumu ya Baraza hilo yafanywe na Baraza la Vyama
vya siasa lililopo sasa jambo lililosababisha kutokukubaliana katika
hoja hiyo.
Pamoja
na michango iliyotolewa , Wajumbe wameishauri Serikali kuona umuhimu wa
kuwekeza katika Baraza la Vyama vya Siasa ili kusaidia utatuzi wa
migogoro nchini kwa kuwa imebainika kuwa machafuko katika nchi nyingi
duniani yamesababishwa na machafuko katika masuala ya siasa.
Akihitaji
ufafanuzi wa hatua gani imefikiwa katika uboreshaji wa Sheria ya Vyama
vya siasa, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama Vya Siasa, Mhe. Peter Kugar
Mziray aliiomba Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kutoa ufafanuzi.
Naye
Msajili Msaidizi, Bw. Sisty Nyahoza akitoa ufafanuzi alisema tayari
vyama vyote vya siasa vimeshapelekewa barua vikiombwa kuwasilisha
mapendekezo kwa ajili ya kuboresha Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka
1992 na Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010 na kwamba Ofisi
inafanya jitihada za kupokea mapendekezo kutoka kwa wadau wa siasa na
ikishakamilisha upokeaji huo, mapendekezo hayo yatawasilishwa kwenye
kamati ya Katiba na Sheria.
Mwenyekiti
wa Baraza la Vyama vya Siasa Nchini Mhe. Peter Kuga Mziray akifafanua
jambo wakati wa kikao cha Baraza kujadili Mapendekezo ya Mfumo wa
utatuzi wa migogoro ndani na baina ya vyama vya siasa kilichofanyika
mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa GEPF Victoria Jijini Dar es salaam .
Kulia ni Mhe. Jaji Francis S.K Mutungi, Msajili wa Vyama vya Siasa na
Mhe. Vuai Ali Vuai, Makamu Mwenyekiti wa Baraza.
Msajili
Msaidizi (Elimu kwa umma na Gharama za uchaguzi) Bi. Piencia C. Kiure
akiwasilisha mada ya Mapendekezo ya Mfumo wa utatuzi wa migogoro ndani
na baina ya vyama vya siasa katika baraza la Vyama vya Siasa
lilichofanyika mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa GEPF Victoria Jijini
Dar es salaam.
baadhi
ya wajumbe wa Baraza la Vyama vya Siasa wakifuatilia mjadala wakati wa
kikao cha Baraza kujadili Mapendekezo ya Mfumo wa utatuzi wa migogoro
ndani na baina ya vyama vya siasa kilichofanyika mwishoni mwa wiki
katika ukumbi wa GEPF Victoria Jijini Dar es salaam.
Bw.
John Cheyo mmoja wa wajumbe wa Baraza la vyama vya siasa akichangia hoja
wakati wa kikao cha Baraza kujadili Mapendekezo ya Mfumo wa utatuzi wa
migogoro ndani na baina ya vyama vya siasa kilichofanyika mwishoni mwa
wiki katika ukumbi wa GEPF Victoria Jijini Dar es salaam.
Picha
ya Pamoja ya Wajumbe wa Baraza la vyama vya Siasa baada ya kikao cha
Baraza kujadili Mapendekezo ya Mfumo wa utatuzi wa migogoro ndani na
baina ya vyama vya siasa kilichofanyika mwishoni mwa wiki katika ukumbi
wa GEPF Victoria Jijini Dar es salaam.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni