Balozi
Mdogo Mpya wa Jamuhuri ya Watu wa China Bwana Xie Xiaolon kushoto
akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
Vuga Mjini Zanzibar alipofika kujitambulisha rasmi kuanza kazi zake za
Kidiplomasia hapa Zanzibar.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kulia akizungumza na
Balozi Mdogo Mpya wa Jamuhuri ya Watu wa China Bwana Xie Xiaolon aliyepo
kati kati alipofika kujitambulisha rasmi.Wa kwanza kutoka kushoto ni msaidizi wa Balozi Xie Xiaolon anayeshughulikia Utawala Bwana Wang Xingjun.
Balozi
Mdogo Mpya wa Jamuhuri ya Watu wa China Bwana Xie Xiaolon
akibadilishana mawazo na Balozi Seif mara baada ya kumaliza mazungumzo
yao.
Picha na – OMPR – ZNZ.Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba Zanzibar inaendelea kufaidika kiuchumi na Maendeleo kutokana na kuungwa mkono kimisaada kutoka kwa mshirika wake mkubwa wa maendeleo Jamuhuri ya Watu wa China.
Alisema China imekuwa mshirika wa karibu na Zanzibar hasa katika sekta ya Kilimo na Viwanda ulioanza mara baada ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964 ambao umewezesha kufungua milango ya ajira kwa Vijana waliowengi Visiwani Zanzibar.
Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati akizungumza na Balozi Mdogo Mpya wa Jamuhuri ya Watu wa China aliyepo Zanzibar Bwana Xie Xiaolon aliyefika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kujitambalisha rasmi kushika wadhifa wa mtangulizi wake Bwana Xie Yunliang aliyemaliza muda wake.
Alisema ujenzi wa utanuzi wa eneo la maegesho ya Ndege, Bandari ya Mpiga Duri Maruhubi, Hospitali ya Rufaa ya Abdulla Mzee Mkoani Pemba pamoja na uendeshaji wa shughuli za Serikali kwa kutumia mfumo wa Teknolojia ya Kisasa ya mtandao wa Mawasiliano { E. Government }ni miongoni mwa Miradi Minne mikubwa inayofadhiliwa na China kupitia Benki ya Kimataifa ya Exim.
Balozi Seif kupitia Balozi huyo aliishukuru Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China na Benki hiyo kwa kuendelea kuiunga Mkono Zanzibar katika miradi hiyo ya Maendeleo, Kiuchumi na Ustawi wa Jamii.
Alisema hatua hiyo itazidi kuimarisha uhusiano wa pande hizo mbili uliodumu kwa takriban miaka 52 sasa ambao unazidi kukuwa kadri maisha ya Wananchi wa sehemu hizo yanavyoendelea kuingiliana Kibiashara na Kiutamaduni.
Aidha Balozi Seif alifahamisha kwamba mabadiliko ya haraka ya kiuchumi yanayoendelea kufanywa na Taifa hilo kubwa la Bara la Asia yataendelea kutoa nafasi kubwa zaidi kwa Nchi changa zinazoendelea hasa zile za Bara la Afrika kuiga mfano huo.
Mapema akijitambulisha rasmi kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, Balozi Mdogo Mpya wa Jamuhuri ya Watu wa China Bwana Xie Xiaolon ameahidi kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa katika kuhakikisha miradi iliyoanzishwa Zanzibar na kupata msukumo wa kiuwezeshaji kutoka Nchini Mwake inakamilika kwa wakati.
Balozi Xie alielezea faraja yake kutokana na Uongozi wa Kampuni ya Kimataifa ya Mtandao wa Mawasiliano ya ZTE yenye Makao Makuu yake Nchini China uliofadhili mradi wa uwekaji wa Taa za bara barani zinazotumia mwanga wa Jua kuanzisha mpango maalum wa kuzifanyia matengenezo taa hizo.
Alisema zipo baadhi ya taa tayari zimeanza kuleta hitilafu zinazopelekea kushindwa kufanya kazi zake kama kawaida za kutoa mwanga kwenye bara bara kutokana na uchakavu wa betri zake.
Ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Wananchi wake kwa kuendelea na harakati zao za kimaisha katika misingi ya amani na utulivu mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu.
Balozi Xie alieleza kwamba hatua hiyo itatoa fursa kwa Viongozi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla pamoja na Jamuhuri ya Watu wa China kuendelea kishirikiana kwa maslahi ya pande hizo mbili.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
12/8/2016.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni