KILA KIJIJI KUPATIWA UMEME IFIKAPO 2020

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kulia) akisalimiana na sehemu ya watendaji kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) pamoja na wakandarasi wanaosimamia miradi ya umeme vijijini inayosimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) mara baada ya kuwasili wilayani Handeni mkoani Tanga.
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (kulia) na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela (kushoto) wakifuatilia taarifa ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini inayosimamiwa na REA Awamu ya Pili (REA II) iliyokuwa inasomwa na Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani Tanga Mhandisi Abdulrahman Nyenye (hayupo pichani)
Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani Tanga Mhandisi Abdulrahman Nyenye akisoma taarifa ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini chini ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) mbele ya Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo pamoja na watendaji wengine kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Wilaya ya Handeni, Wizara ya Nishati na Madini, TANESCO na wakandarasi wanaotekeleza miradi ya REA.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martine Shigela akielezea mafanikio ya miradi ya usambazaji wa umeme vijijini iliyotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini Awamu ya Pili (REA II).

                                                                                                Na Greyson Mwase, Tanga

Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo amesema kuwa serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2020 kila mwananchi anapata umeme wa uhakika na kupelekea uchumi wa nchi kukua kwa kasi.

Profesa Muhongo aliyasema hayo mara baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa miradi ya usambazaji wa umeme vijijini inayosimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini Awamu ya Pili (REA II) kutoka kwa watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani Tanga. Profesa Muhongo yupo mkoani Tanga kwa ajili ya kukagua miradi ya umeme vijijini inayotekelezwa na REA pamoja na kuzungumza na wananchi.

Profesa Muhongo alisema kuwa kwa kutambua mchango wa nishati ya umeme katika ukuaji wa viwanda nchini, serikali imeweka mkakati wa kuhakikisha kuwa kasi ya usambazaji wa umeme vijijini inaongezeka ili ifikapo mwaka 2020 mgawo wa umeme uwe ni historia

Alieleza kuwa serikali imeamua kuweka nguvu katika usambazaji wa umeme hususan katika maeneo ya vijijini ili kufuta umaskini kwani kupitia nishati ya umeme wananchi waishio vijijini wana uwezo wa kuanzisha viwanda vidogo vidogo na kuongeza ajira na kupunguza wimbi la vijana wengi kukimbilia mijini kwa ajili ya kutafuta maisha.

Akielezea mpango wa utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini itakayosimamiwa na REA Awamu ya Tatu (REA III), Profesa Muhongo alisema kuwa serikali imetenga zaidi ya shilingi trilioni moja kwa ajili ya kusambaza umeme katika maeneo yote kipaumbele kikiwa ni katika vijiji vilivyokosa umeme REA Awamu ya Pili. (REA II) Hata hivyo Profesa Muhongo alieleza kuwa wakandarasi waliokwamisha miradi ya REA Awamu ya Pili hawatapewa kazi ya kusambaza umeme vijijini katika REA Awamu ya Tatu.

“Serikali iko makini katika kuhakikisha kuwa wakandarasi wenye sifa wanapewa kasi ya kusambaza umeme vijijini, hatuhitaji wakandarasi wasiotekeleza miradi kwa wakati,” alisema Profesa Muhongo.

Profesa Muhongo aliwataka wakandarasi wa kitanzania wenye vigezo kujitokeza na kuchangamkia fursa ya kusambaza umeme vijijini kupita REA Awamu ya Tatu. Aliongeza kuwa kupitia REA Awamu ya Pili wakandarasi wa kitanzania walionyesha uwezo mkubwa sana katika kusambaza umeme vijijini.

Ili kuendana na mahitaji ya umeme nchini Profesa Muhongo alilitaka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha linaongeza Megawati 200 za ziada ndani ya miezi 18.

Alisema wakati serikali kupitia REA ikiendela na kasi yake ya kusambaza umeme nchi nzima, shirika la TANESCO linatakiwa kuhakikisha nishati ya uhakika inapatikana ikiwa ni pamoja na ubunifu wa vyanzo vipya vya umeme.

Awali akielezea utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini mkoani Tanga, Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania mkoani Tanga, Mhandisi Abdulrahman Nyenye alisema kuwa miradi ya umeme vijijini chini ya ufadhili wa REA imekuwa ikitekelezwa katika wilaya zote nane za mkoa wa Tanga ambazo ni pamoja na Tanga Mjini, Muheza, Korogwe, Handeni, Kilindi, Lushoto, Pangani na Mkinga ambazo zinapata umeme wake kutoka Gridi ya Taifa kupitia vituo vya Hale, Kange na Tanga (Majani Mapana)

Alisema kundi la kwanza lilihusisha wilaya za Korogwe, Lushoto, Handeni na Kilindi ambapo mradi wa wilaya hizi ulitekelezwa na mkandarasi STEG International Services Ltd ya Tunisia na kusimamiwa na TANESCO.

Alifafanua kuwa gharama za mradi huo ilikuwa ni Dola za Marekani 9,463,502 ambazo ni sawa na shilingi bilioni 14.6 na kuendelea kusema kuwa kundi la pili lilihusisha wilaya za Muheza, Mkinga, Tanga Vijijini na Pangani na kutekelezwa na mkandarasi Sengerema Engineering Group Ltd ya Tanzania na kusimamiwa na TANESCO.

Alisema kuwa mradi huu uligharimu shilingi bilioni 15.6 na kusisitiza kuwa miradi yote kwa mkoa wa Tanga imekamilika kwa asilimia 99 ambapo jumla ya vijiji 178 vimepatiwa huduma ya umeme.

Akielezea changamoto katika utekelezaji wa miradi hiyo Mhandisi Nyenye alieleza kuwa ni pamoja na tatizo la wananchi kuzuia upitishwaji wa laini za umeme kwenye maeneo yao kwa kudai fidia ili kuruhusu mazao yao yakatwe na hali ya hewa ya mvua isiyotabirika hasa maeneo ya wilaya za Muheza na Lushoto.

Alitaja chagamoto nyingine kuwa ni pamoja na ubovu wa miundombinu hasa ya barabara kwenye maeneo mengi , hali duni ya kiuchumi ya wananchi inayopelekea wananchi kushindwa kulipa gharama za kuunganishiwa umeme na gharama kubwa za ukaguzi wa miundombinu ya ndani (wiring) zinazotozwa na wakandarasi ambazo zimekuwa ni kikwazo kwa wananchi wanaohitaji huduma ya umeme.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni