FEDHA ZA MAENDELEO KUWAUNGUZA WATAKAOZICHEZEA-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watendaji wa halmashauri mkoani Katavi kuwa makini na matumizi ya fedha za maendeleo zinazopelekwa katika maeneo yao na atakayethubutu kuzichezea zitamuunguza. 

“Fedha hii tafadhali ni ya moto. Msicheze na hii ya halmashauri tunayoileta hapa halmashauri kwa ajili ya wananchi itawakunguza vidole. Tunaileta kwa madhumini, tunataka wananchi wahudumiwe,“ alisema.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana jioni (Jumapili, Agosti 21, 2016) wakati akihutubia umati mkubwa wa wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kiwanja cha Azimio wilayani Mpanda.

Alisema Serikali imeanza kupeleka fedha za miradi ya maendeleo katika halmashauri mbalimbali hivyo ni vema kila mtendaji ahakikishe fedha hizo zinatumika kwa ajili ya ujenzi wa miradi iliyokusudiwa na si vinginevyo.

Waziri Mkuu alisema ni lazima wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa Halmashauri wahakikisha viwango vya ubora wa miradi inayojengwa katika maeneo yao kuwa inalingana na thamani halisi ya fedha zilizotolewa.

Wakati huo huo Waziri Mkuu amemtaka Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu kwenda wilayani Mpanda na kuangalia namna ya kuipanua hospitali ya Manispaa ya Mpanda ambayo inahudumia mkoa wote wa Katavi.

Alisema hospitali hiyo ilijengwa mwaka 1957 kama zahanati ambayo kwa sasa yanatumika katika kuwahudumia wananchi wate wa mkoa huo imezidiwa hivyo alimuagiza mkuu wa mkoa huo Meja Jenerali (Mstaafu) Raphael Muhuga kuharakisha ujenzi wa hospitali ya mkoa.

Aidha, Waziri Mkuu alisema kuwa wakati mkoa ukiwa kwenye harakati za ujenzi wa hospitali ya mkoa wilaya nazo zianze ujenzi wa hospitali za wilaya ili kuhakikisha sera ya Serikali ya kuwa na hospitali katika kila wilaya inatekelezwa.

Alisema kwa sasa madaktari na wauguzi wanaofanya kazi kwenye hospitali ya Manispaa ya Mpanda wamezidiwa kutokana na kuhudumia idadi kubwa ya wagonjwa kuliko uwezo wao. Hivyo amewataka madaktari na wauguzi wa wilaya ya Mpanda kuendelea kufanya kazi kwa kushirikiana na wenzao wa Manispaa.

Awali hospitali hiyo ilikuwa chini ya uongozi wa halmashauri ya Mpanda. Hospitali hiyo kwa sasa ipo chini ya Manispaa ya Mpanda hivyo Waziri Mkuu ameutaka uongozi wa mkoa huo kuboresha huduma kwa kupeleka dawa na vifaa tiba vitakavyoweza hospitali hiyo kuhudumia wagonjwa wa mkoa.

Mkoa umetenga sh. bilioni 1.7 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa hospitali ya mkoa.

IMETOLEWA NA: 

OFISI YA WAZIRI MKUU, 
JUMATATU, AGOSTI 22, 2016.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni