TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF

Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2016/17 inatarajiwa kuanza kesho Jumamosi Agosti 20, 2016 kwa michezo mitano huku Bingwa Mtetezi wa Kombe hilo 2015/16, Young Africans ya Dar es Salaam ikisubiri hadi Agosti 31, 2016 kuanza kutetea taji lake.

Young Africans inatarajiwa kusafiri kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kucheza na TP Mazembe kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho unaotarajiwa kufanyika Agosti 23, mwaka huu.

Michezo itakayochezwa kesho ni pamoja na Simba SC itakayoikaribisha Ndanda FC ya Mtwara kwenye Uwanja wa Taifa, ulioko Chang’ombe Dar es Salaam, katika mchezo utakaoanza saa 10.00 jioni wakati Azam itakuwa mwenyeji wa African Lyon kwenye Uwanja wa Azam FC ulioko Chamazi-Mbagala, nje kidogo ya jiji.

Kadhalika Stand United ya Shinyanga itakuwa mwenyeji wa Mbao FC ya Mwanza kwenye Uwanja wa CCM Kambarage mkoani Shinyanga sawa na Mtibwa Sugar itakayoikaribisha Ruvu Shooting ya Pwani kwenye Uwanja wa Manungu uliuoko Turiani, Mvomero mkoani Morogoro wakati Prisons ya Mbeya itasafiri hadi Uwanja wa Majimaji ya Songea kucheza na Majimaji FC ya huko.

Wakati ligi ikianza, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaonya timu kuchezesha wachezaji wa kigeni kama hawana vibali vya kuishi, kufanya kazi na leseni inayomruhusu kucheza ligi husika kwa mujibu wa sheria za nchi na kanuni za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Vibali vya kuishi na kufanya kazi vinatolewa na Idara ya Uhamiaji Tanzania (Uhamiaji) wakati leseni ya kucheza inatolewa na TFF. Vilevile tumeziagiza klabu kulipia ada za ushiriki kwa kila timu; leseni za wachezaji, ada za wachezaji na ada za mikataba. Mchezaji hatapewa leseni ya kucheza kama uongozi wa timu hautakamilisha taratibu za malipo.

TFF linapenda kuzikumbusha timu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwamba hatutatoa leseni ya mchezaji yeyote ambaye timu haikuleta mkataba wakati wa maombi ya usajili, hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 68 vipengele vya 1, 2, 3 na 8 ya Ligi Kuu ya Tanzania toleo la 2016/2017.

Kila timu inatakiwa kuleta nakala tatu za mkataba wa mchezaji, ili kamati ya katiba, sheria na hadhi za wachezaji iweze kupitia na TFF iweze kuidhinisha mikataba hiyo. Baada ya hapo timu na mchezaji, watakuja kuchukulia mikataba hiyo hapa TFF. Ni matarajio yetu kuwa kila klabu itatimiza wajibu wake ili kuondoa migogoro kati ya timu na mchezaji na mchezaji na timu. Tunategemea kupata ushirikiano.

USAJILI KUU TANZANIA BARA, KESI AIDHINISHWA KUCHEZA YOUNG AFRICANS
Kamati ya Sheria na Haki za wachezaji imepisha usajili wa wachezaji wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara huku ikiwa imepitisha jina la Hassan Ramadhani ‘Kesi’ kuitumikia Young Africans kuanzia msimu huu 2016/17 baada ya kuona kuwa hana tatizo katika usajili badala yake madai ambayo pande husika zinaweza kudaiana wakati mchezaji anaendeleza kipaji chake.

Kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake, Richard Sinamtwa imepitia usajili wa timu zote na kujiridhisha kwamba suala la mchezaji Hassan Kessy limeegemea kwenye madai na si usajili ambako Simba ndiye mdai kwa kumtuhumu mchezaji huyo kuwa alianza kuitumikia Young Africans kabla ya kumaliza mkataba wake Simba SC. Mkataba wake ulifika mwisho, Juni 15, 2016.

Kama ni madai Simba inaweza kuendelea kumdai Kessy au Young Africans wakati mchezaji huyo anatumika uwanjani kwa mwajiri mpya. TFF inafuatilia na kuangalia haki ya Simba namna ya kupata haki yake baada ya kuwasilisha madai kuhusu kuvunja mkataba na mwajiri wake wa zamani.

Kanuni hazimzuii mchezaji kuendelea kucheza kwa hoja ya madai badala yake suala hilo linaweza kumalizwa wakati mashindano yanaendelea. Kamati inaendelea kupitia malalamiko na pingamizi za wachezaji wengine na inatarajiwa kutoa taarifa rasmi kuhusu wachezaji wote wakati wowote kuanzia sasa.

KUIONA SERENGETI BOYS, AFRIKA KUSINI SH 2,000, 5,000

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetangaza kiingilio cha Sh 2,000 kwa mzunguko na Sh 5,000 kwa jukwaa kuu wakati timu ya taifa ya Tanzania ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 itakapocheza na Amajimbos ya Afrika Kusini kwenye mchezo wa kuwania nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazofanyika Madagascar, mwakani.

Mchezo huo utaoanza saa 9.00 alasiri Jumapili Agosti 21, 2016 kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi – Mbagala, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam utachezeshwa na Mwamuzi Noiret Jim Bacari wa Comoro akisaidiwa na Mmadi Faissoil na Said Omar Chebli wakati mezani atakuwa Ali Mohamed Adelaid huku Kamishna wa mchezo huo atatoka Somalia ambaye anaitwa Amir Abdi Hassan.

Jumamosi Agosti 6, 2016, Serengeti ilitoka sare ya 1-1 na Afrika Kusini katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Dobsonville ulioko Soweto, Mji ulioko Kusini – Magharibi mwa jiji la Johannesburg, mabao yote yalipatikana kipindi cha pili yakiwa ni ya penalti kwa kila upande. Afrika Kusini ndio walioanza kupata penalti katika dakika 65 iliyofungwa na Luke Gareth kabla ya Ally Msengi kuisawazishia Serengeti Boys katika dakika ya 70.

Penalti ya Afrika Kusini ilitokana na mmoja wa mabeki wa Serengeti Boys kumfanyia madhambi Linamandla Mchilizeli wa Amajimbos ndani ya eneo la hatari wakati ile ya Serengeti Boys ilitoakana na beki Luke Donn wa Amajimbos kunawa mpira eneo la hatari. Mwamuzi wa mchezo huo alikuwa, William Koto kutoka Lesotho.

Kocha Mkuu wa Serengeti Boys, Bakari Shime maarufu kama Mchawi Mweusi amesema: “Watanzania wakaribie Chamazi, waje kutushangilia ili tushangilie ushindi kwa pamoja kikosi change kiko vema na ninamshukuru Mungu kwa hilo, akili yangu na akili za wachezaji wangu ni kumuondoa Msauzi (Afrika Kusini).”

MALINZI AMLILIA KELVIN HAULE

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amemtumia salamu za rambirambi Mwenyekiti wa Klabu ya Majimaji ya Songea, mkoani Ruvuma, Humphrey Millanzi kutokana na kifo cha mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Kelvin Haule kilichotokea jana Agosti 18, 2016 kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma.

Rais Malinzi amesema, amepokea taarifa za kifo cha Haule kwa masikitiko makubwa.

Rais Malinzi amemuelezea Haule kuwa alikuwa na mchango mkubwa katika mafanikio ya timku ya Majimaji ya Songea na Lipuli ya Iringa hivyo ameacha alama ya ucheshi, kujituma na uwajibikaji katika kufanikisha kazi zake katika timu ambazo alichezea.

Salamu za rambirambi za Rais wa TFF Malinzi pia zimekwenda kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki na kuwataka kuwa na moyo wa subira wakati huu mgumu wa msiba wa Kelvin Haule.

Mwenyezi Mungu aipumzishe roho ya marehemu Kelvin Haule mahala pema peponi.

Bwana alitoa, Bwana alitoa, jina la Bwana lihimidiwe.

IMETOLEWA NA SHIRIKIS
HO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni