Mkurugenzi  Mkuu wa Mamlaka ya Elimu 
Tanzania Joel Laurent (wa kwanza kushoto) akijadiliana suala  na 
viongozi wa Halmashauri ya Kilosa, Mamlaka ya Elimu  Tanzania inatarajia 
kutekeleza na kufadhili mradi wa kujenga nyumba za walimu kupitia 
Watumishi Housing Ltd katika Ujenzi katika maeneo yasio rahisi kufikika,
 katika shule ya Sekondari Uleling'ombe iliyopo Wilaya ya Kilosa. 
 Mkurugenzi
 Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania,Joel Laurent akiongea na 
viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, kamati ya shule ya 
Uleling'ombe,uongozi wa kijiji cha Uleling'ombe wakijadilana utekelezaji
 wa Mradi wa kujenga nyumba za walimu katika maeneo yasio rahisi 
kufikika, katika shule ya Sekondari Uleling'ombe iliyopo Wilaya ya 
Kilosa.
 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania,Joel Laurent akioneshwa 
eneo lililotengwa kwa ajili ya kujenga nyumba za walimu katika shule ya
 Sekondari Uleling'ombe mradi unaotekeleza na kufadhili na Mamlaka ya Elimu Tanzania ikiwatumia 
Watumishi Housing Ltd katika Ujenzi katika maeneo yasio rahisi kufikika.
Picha ya pamoja.
MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Joel Laurent amesisitiza kuwa taasisi yake itaendelea kutafuta rasilimali ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wanosoma katika maeneo ambayo ni magumu kufikika wanajengewa miundombuni ili kupata elimu bora.
Mkurugeni Mkuu huyo alisema hayo wilayani Kilosa wakati
akikagua eneo la ujenzi wa nyumba ya walimu wa shule ya sekondari ya Uleling’ombe
utakaogharimu zaidi ya 148m/- ambayo walimu sita watakaa katika nyumba hiyo.
Alisema mamlaka hiyo imetiliana saini mkataba na Watumishi
Housing wa ujenzi wa nyumba za walimu 40 nchi nzima katika maeneo ambayo ni
magumu kufikika ili kuhakikisha kuwa walimu wapya wanaopangiwa katika maeneo
hayo ambao wengi wamekuwa wakikimbia kufundisha wanapata sehemu nzuri za
kuishi.
Aliongeza kuwa katika mwaka huu wa fedha mamlaka yake
imetenga bajeti ya kujenga nyumba 30 mwaka huu ambapo ujenzi wa kila nyumba ni
miezi mitatu.
“Nyumba hii itakapokuwa tayari na tunategemea ikamilike
ifikapo Desemba mwaka huu, itakuwa na uwezo wa kuwaweka walimu sita kuishi
katika nyumba hiyo ila tunazitaka halmashauri kuangalia uwezekano wa kuwawekea
samani za ndani” alisema.
  
Na pia alisisitiza juu ya umuhimu wa ushiriki wa wananchi
na halmashauri hizo katika kuhakikisha kuwa ujenzi wa nyumba hizo unazingatia
ujenzi ili ziweze kutumika kwa muda mrefu na hivyo kuwanufaisha wanafunzi wengi
zaidi.
TEA ilibuni mradi huo baada ya kugundua kuwa kuna uhitaji
maalum wa makazi ya walimu katika mazingira ambayo ni vigumu kufikika ambapo wengi
ambao wamekuwa wakipangiwa kufundisha hutafuta uhamisho na hivyo wanafunzi wa
maeneo hayo ufaulu wao umekuwa mdogo kutokana na kukosa walimu.
“Walimu wanaokusudiwa kuishi katika nyumnba hizi ni wale
wanaoanza kazi ndiyo maana ni chumba na sebule kwa kila mwalimu kwani tunaamini
baada ya muda watakuwa wameishazoea na kuweza kujipatia makazi uraiani pale
watakapokuwa tayari kuanza familia” Alisema Bw Laurent.
Aliongeza kuwa mamlaka hiyo inajadiliana na wadau mbali
mbali ili kuona kama wataweza kuwezesha upatikanaji wa internet na ving’amuzi
katika sebule ya pamoja ya nyumba hizo ili wale watakaopangiwa maeneo hayo
wasijione kuwa wamepangiwa katika mazingira ambayo si rafiki au wameonewa.
Akizungumza katika ukaguzi huo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji
wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Bw Rwegerela Katabaro alisema kuwa wako
tayari kushirikiana na TEA japo rasilimali fedha imekuwa ni changamoto kubwa.
Aliomba kuwa katika miradi mingine halmashauri zipewe
taarifa za awali ili ziweke kutenga fungu katika bajeti zaona hivyo kuchangia
katika juhudi za maendeleo.
Alimhakikishia Mkurugenzi Mkuu huyo juu ya ushiriki wa
halmashauri kusimamia kwa karibu ujenzi wa nyumba hiyo ili kupata nyumba ambayo
inalingana na thamani ya fedha zilizotengwa.
Aidha ili kuondoa mgongano alishauri TEA itoe muongozo ili
kila taasisi ijue jukumu lake katika kuhakikisha kuwa ujenzi wa nyumba hiyo
unakuwa bora na kwa viwango walivyokubaliana.
Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari Uleling’ombe, Magashi
Shimba alishukuru kwa kupatiwa mradi huo kwani walimu wengi wanaopangiwa huko
huwa hawarudi kutokana na mazingira hasa upatikanaji wa makazi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni