MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amekabidhi ramani ya jengo
la Ofisi ya Makao Makuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA),
ikiwa ni ahadi ya kuwajengea jengo hilo.
Akizungumza wakati akikabidhi ramani hiyo, Makonda alisema jengo hilo
linatarajiwa kuwa na ghorofa tatu na litagharimu zaidi ya Sh bilioni
tano.
“Ijumaa nitakuja hapa kwa ajili ya kuweka jiwe la msingi na niseme tu
ujenzi utaanza hivi karibuni na nimeshawaambia watu wangu wahakikishe
jengo hilo linajengwa kwa muda usiozidi miezi 14 tu,” alisema Makonda.
Licha ya kukabidhi ramani hiyo, Makonda pia aliwataka viongozi hao wa
dini kuendelea kuhubiri amani ili taifa liendelee kuwa na amani na
mshikamano. Alisema ujenzi wa jengo hilo, umekuja baada ya kuona kuwa
Bakwata imekuwa na mchango mkubwa kwa taifa ikiwemo kuhubiri amani na
mshikamano.
“Viongozi wa dini ni watu muhimu sana wamekuwa wakituhubiria amani na
pia viongozi hao wamekuwa wakituongoza katika safari ya kutupeleka kwa
mola, endeleeni kudumisha na kuihubiri amani ili taifa ili liendelee
kusifika,” alisema Makonda.
Kwa upande wake, Mufti wa Tanzania, Shehe Mkuu Abubakar bin Zubeir
alimshukuru Makonda kwa uamuzi alioufanya; na kusema ameonesha njia kwa
wadau wengine walio na wasio waislamu kujitolea kuchangia.
“Najua jamii inaweza kushangaa kwa nini nimepokea msaada kutoka kwa mtu
ambaye si Muislamu, lakini niseme tu hata Mtume alipokea misaada kutoka
kwa watu kama hawa, ni rai yangu kuwaombeni na ninyi Waislamu mjitokeze
kuunga mkoa juhudi hizi kwa hali na mali,” alisema.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni