Utunzi mahiri wa mashairi na
ughani uliotukuka wa Mrisho Mpoto, umeligusa sikio la Rais wa Jamhuri wa
Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ambaye ameeleza kuwa
shabiki mkubwa wa kazi za msanii huyo hususan wimbo wake ‘Sizonje’.
Akizungumza na Mpoto jana, muda
mfupi baada ya kuwasili jijini Dar es Salaam katika Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere, Rais Magufuli alimueleza msanii huyo kuwa
anazifahamu vizuri kazi zake na kwamba anaupenda sana wimbo wake wa
‘Sizonje’ huku akichambua baadhi ya mistari iliyomo kwenye beti za wimbo
huo.
Mpoto alikuwa msanii pekee
aliyeongozana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Waziri wa Habari,
Utamaduni, Michezo na Sanaa, Nape Nnauye, Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Paul Makonda, Wakuu wote wa Wilaya za Dar es Saalam pamoja na
viongozi wengine waliofika katika uwanja huo wa ndege kumpokea Mkuu huyo
wa nchi.
“Nasikiliza nyimbo zako sana, ila
huu wimbo wako wa Sizonje nimeuelewa sana na nausikiliza kila siku,
kwangu umekuwa kama wimbo wa taifa, mwanzoni nilipata tabu kuuelewa
lakini sasa hivi… aaaah, nimeuelewa vizuri sana. Halafu Sizonje namjua, nimtaje?,” yalisikika baadhi ya maneno ya Rais Magufuli kwa Mrisho Mpoto.
Akielezea tukio hilo lililoleta
msisimko wa aina yake uwanjani hapo, Mpoto alisema kuwa baada ya
kumsikia Rais ameanza kuusifia wimbo wake alishtuka na kujawa na furaha
ya aina yake kwani kwa msanii ni jambo la thamani kubwa kusifiwa kazi
yake na Mkuu wa Nchi.
Alisema kuwa pamoja na kuusifia
wimbo huo, Rais alionesha kuufahamu vizuri zaidi baada ya kuanza
kuipitia baadhi ya mistari na kuahidi kumfumbulia fumbo lililofichwa
kwenye wimbo huo watakapokutana tena.
“Unapopata thamani kutoka kwa Mkuu
wa Nchi inaleta faraja sana,” amesema Mpoto. “Kwahiyo, mheshimiwa Rais
leo kuniambia kwamba yeye ni shabiki wa kazi zangu na kwamba anapenda
sana wimbo wa Sizonje, na akafunguka kwa mistari ‘minane’ ya Sizonje
ikiwa ni pamoja na ile inayosema ‘huyu mgeni anayepitia madirishani
wakati milango ipo!’ Na akaniambia siku tukikutana ataniambia vile
vyumba vitatu kwanini havifunguki,” ameongeza.
Msanii huyo amemshukuru Rais
Magufuli kwa kuthamini mchango wake katika sanaa kwakuwa anaamini
kuthaminiwa ni hitaji kubwa la kila msanii.
“Kwakweli leo ni siku yenye furaha
sana. Najisikia furaha sana. Asante sana mheshimiwa Rais John Pombe
Magufuli. Umenifanya nimekuwa na siku nzuri sana,” Mpoto amefunguka kwa
furaha.
Mwaka huu mwanzoni, Mrisho Mpoto
aliachia audio na video ya ‘Sizonje’ aliomshirikisha Banana Zorro ambapo
kwa muda mfupi tu, wimbo huo uligeuka kuwa mkubwa na kufanya vizuri.
Kutokana na ufanisi wa kazi zake, Mpoto ameendelea kukubalika akipata
mikataba ya ubalozi wa mashirika na taasisi kubwa nchini ikiwa ni pamoja
na mfuko wa pensheni wa PSPF.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni