Baadhi ya magari yanayopigwa picha njiani na raia wema na mabalozi wa
usalama barabarani yakifanya makosa na picha zao kutumwa kituo cha
mawasiliano cha kikosi cha usalama barabarani
Baadhi ya magari yanayopigwa picha njiani na raia wema na mabalozi wa
usalama barabarani yakifanya makosa na picha zao kutumwa kituo cha
mawasiliano cha kikosi cha usalama barabaran
Na
Augustus Fungo, Balozi wa Usalama Barabarani
HIVI karibuni imejitokeza njia mpya ya kusaidia kupambana na wimbi la
ajali za barabarani, ambapo pamoja na faini kwa madereva wanaokiuka
sheria za barabarani wamekuwa wakipigwa picha na baadaye picha hizo
kuwekwa kwenye mitandao ya kijamii au magazetini na hata wakati mwingine
kwenye televisheni. Mathalani katika mtandao wa facebook kundi la
Mabalozi wa Usalama Barabarani maarufu kama, RSA wakishirikiana na Jeshi
la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani hutumia mbinu hii kuwapiga
picha wakiukaji wa sheria za barabarani kisha kuzituma katika Kituo cha
Mawasiliano cha Usalama Barabarani (Traffic Control Center, TCC).
Kituo
hiki huwatumia picha hizi ambazo pia ni ushahidi askari waliopo katika
vituo mbalimbali barabarani, ili kuwezesha watuhumiwa kukamatwa na
magari husika. Baada ya kukamatwa magari husika askari humwandikia faini
mkosaji, kumpiga picha na kuituma kwenye kituo cha mawasiliano ya
polisi (TCC) ambacho na chenyewe hutoa mrejesho kwa watoa taarifa.
Picha
hizo hatimaye kuwekwa kwenye mtadao wa facebook, hutumika kuandaa
vipindi vya televisheni vya kuelimisha jamii mfano, ni kipindi cha ‘Aibu
yako' kinachorushwa na televisheni ya ITV na pia picha hizo huhifadhiwa
na kikosi cha usalama barabarani kwa ajili ya kumbukumbu na rejea iwapo
dereva husika atarudia kosa hilo.
Njia hii mpya ambayo inaitwa kutaja na kuaibisha, ama kwa kiingereza
“Naming and Shaming” ni maarufu sana inayotumika si tu na nchi nyingi za
Ulaya bali pia na mashirika ya haki za binadamu kama 'Human Rights
Watch', hutumia kuyaaibisha mataifa yaliyokubuhu kwa ukiukaji wa haki za
binadamu.
Saudi Arabia kupitia sheria yake ya makosa ya mtandao (Anti-cyber-crime
law (Royal Decree No. M/17 dated 8 Rabi1 1428) imepitisha mbinu hii kama
mojawapo ya adhabu. Mbinu kama hii hutumika pia katika nchi nyingi za
Ulaya kuwaaibisha watu au makampuni yanayokwepa kodi. Moja ya makampuni
yaliyowahi kuathirika na kadhia hii ni kampuni ya Kahawa ya Starbuck.
Januari 15, 2015, serikali ya Uingereza iliwataja na kuwadhalilisha
waajiri 37 wa Uingereza walioshindwa kulipa kima cha chini kwa
wafanyakazi wao.
Hata hivyo, mwandishi James Meernick(2012), anaitaja njia hii kama
chaguo kuu la mashirika mengi ya kimataifa katika kuhakikisha haki za
binadamu zinazingatiwa.
Njia hii hutumika ikiaminika kwamba kumuweka mtu au taasisi hadharani
ili aweze kujiona mwenyewe, aonwe na familia yake, marafiki zake, na
hata waajiri wakati akitenda kosa inasaidia kumfanya mtu ajitafakari na
kutorudia kosa au pia kuwafanya wanaomzunguka kumpa shinikizo la kufuata
sheria au kuheshimu haki za wengine.
Baadhi ya magari yanayopigwa picha njiani na raia wema na mabalozi wa
usalama barabarani yakifanya makosa na picha zao kutumwa kituo cha
mawasiliano cha kikosi cha usalama barabarani
Pamoja
na hayo baadhi ya wadau nchini wameipokea mbinu hii kwa hisia tofauti.
Wengine wamedai kwamba ni kinyume cha sheria japokuwa hawajaweka kutaja
ni sheria gani hasa inayokiukwa kwa kufanya hivyo; wengine wamedai ni
kuingilia usiri(privacy) ya mtu bila kusema ni kwa vipi siri ya mtu
inaingiliwa pale anapotenda kosa. Pia wameshindwa kuushawishi umma
kuelewa je, mtu anapokuwa mathalani anatanua barabarani (matumizi mabaya
ya barabara), au analipita gari pasiporuhusiwa au anakimbia kwa zaidi
ya mwendo kasi wa 80 (speed) kinyume na sheria akakamatwa akapigwa picha
ni kwa jinsi gani anadhalilishwa zaidi ya kuaibishwa?
Maana wakati anapigwa hiyo picha kwanza anakuwa ameshakubali kosa; pili,
anakuwa hajavuliwa nguo wala kurushwa kichurachura, kupigwa au kufungwa
pingu. Isitoshe wapinzani wa mbinu hii wameshindwa kuwashawishi
Watanzania kuelewa iwapo kumpiga picha mkosaji barabarani ni kosa,
inakuwaje au ni mara ngapi watuhumiwa wamekuwa wakipigwa picha
wanapofikishwa mahakamani?
Je, ni mara ngapi kumekuwa na matukio mfano ya ujambazi na watuhumiwa wa
ujambazi katika eneo la tukio au walipokamatwa vyombo vya habari
vimekuwa vikiwapiga picha. Je, huku si kuvunja sheria? Itakumbukwa Kituo
cha Luninga cha ITV na vingine nchini vimewahi kurusha kipindi maalumu
kinachoonesha askari wanaodaiwa wanapokea rushwa, mbona hili
halikusemewa? Ni mara ngapi polisi wamekuwa wakitoa picha wa watu
wanaotafutwa kwa uhalifu (wanted), ni mara ngapi waajiri wamekuwa
wakitoa picha za wafanyakazi wao waliofukuzwa kazi kwa makosa ya
kutokuwa waaminifu? Iweje leo picha za wakosaji wa barabarani tu
tutolewa ionekane wanadhalilishwa?
Wapo watu wametoa hoja kuwa dereva mkosaji ana maisha yake mengine eti
yanaathirika kutokana na kupigwa picha. Kimsingi hoja hii haina mashiko
kwakuwa lengo la mbinu ya kutaja na kuaibisha ni kumfanya muhusika aone
aibu kwa upuuzi alioufanya na kuweza kujirekebisha. Dereva anayejua kuwa
hiyo inaweza kumuharibia hadhi yake huko baadae atakuwa makini zaidi
kutokiuka sheria za barabarani au kuchezea maisha ya watanzania wasio na
hakia.
Picha kama hii inaweza kutumwa katika kituo cha cha taarifa cha kikosi cha usalama barabarani kwa hatua zaidi Baadhi ya Mabalozi wa Usalama Barabarani maarufu kama, RSA
Gari
za serikali, mashirika ya umma, miradi, na zinginezo haziko juu ya
sheria. Bila kujali operesheni wanayofanya au lengo la safari yao
hawapaswi kuvunja sheria, na endapo watakuwa wamevunja sheria kwa sababu
ya kwenda kuhudhuria dharula husika, askari aliyesimamisha hilo gari
akiridhika na sababu hiyo hata toza faini wala kupiga picha, kwa hiyo
hakuna kitakachoathirika. Na endapo kuna hofu ya matumizi mabaya ya hizo
picha, atakaye wajibika ni huyo anayetumia vibaya picha hiyo ili mradi
tu picha halisi (original) ya tukio zima ipo na ndiyo itakayotumika kama
ushahidi dhidi ya mtu aliyeitumia picha vinginevyo.
Ni ushauri wetu kuwa askari waendelee na mbinu hii ili wavunja sheria
waaibike na kuweza kujirekebisha. Haiwezekani dereva amesomea
amejaribiwa na kupewa leseni, anajua amebeba abiria kwenye gari lake
halafu aendeshe kwa mwendo hatarishi, ayapite magari mengine kana kwamba
amebeba viazi, au abiria ni mateka wake.
Faini peke yake hazi saidii. Binafsi ningependa hata siku moja mahakama
imhukumu mkosaji kufagia barabara za Kariakoo kwa wiki zima badala ya
kumpeleka jela hii ingesaidia zaidi kurekebisha watu. Kimsingi ipo haja
kama taifa tuwe na adhabu mbadala. Na kwa kuwa hakuna sheria inayovunjwa
kwa mtu kupigwa picha wakati akitenda kosa na kuwekwa hadharani, mbinu
hii bado itaendelea kuwa sahihi ili wahusika waache kutenda makosa
ambayo yanagharimu si tu maisha ya watanzania bali pamoja na uchumi wa
nchi. Naimani Jeshi la Polisi ni Jeshi lenye ueledi na wataalamu
mbalimbali hivyo litaendelea kubuni mbinu mbalimbali za kurekebisha
tabia na kutekeleza sheria. Hii ndio imani yangu kwa taasisi hii muhimu
nchini Tanzania, wananchi tushirikiane nao.
Usalama Barabarani ni Jukumu Letu sote.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni