WASIRA AWAIMIZA WAKAZI WA MTWARA KUWEKEZA KATIKA UZALISHAJI WA MAZAO YA KILIMO NA UVUVI

 Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira akiongea na baadhi ya wanachama wa CCM mkoani Mtwara alipofika kuomba kudhaminiwa
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira akipokewa na baadhi ya wanachama wa CCM mkoani Mtwara alipofika kuomba kudhaminiwa
Na Woinde Shizza
WAZIRI wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira,amewahimiza wakazi wa Mtwara kuwekeza katika uzalishaji wa mazao ya kilimo na uvuvi ikiwa ni sehemu ya shughuli za kiuchumi zitakazowanufaisha kutokana na kugundulika kwa gesi asilia katika ukanda wa kusini mwa nchi.


Wasira ambaye pia ni Mbunge wa Bunda alikuwa akizungumza na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliomdhamini ili apitishwe na chama hicho kuwania Urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.


Alisema ingawa zipo fursa nyingi zitakazowanufaika Watanzania  kutokana na sekta hiyo mpya (gesi), lakini mazao ya kilimo na uvuvi yanaweza kuwa miongoni mwa shughuli zitakazowanufaisha wananchi wengi hasa wa hali ya chini.


Mtwara ni eneo lililowahi kukumbwa na machafuko kutokana na hisia tofauti zilizokuwapo kuhusu manufaa yanayopaswa kuwafikia wakazi wa mkoani Mtwara, hasa kuhusu ujenzi wa viwanda na kuibadili gesi ili itakaposafirishwa isiwe katika mali ghafi.


Hata hivyo, Wasira alisema anatarajia kufungua fursa nyingi zaidi za kiuchumi kwa ajili ya wananchi kama atateuliwa na CCM na hatimaye kushinda katika Uchaguzi huo.


Hakuelezea kwa undani kutokana na kuwa wakati wa kampeni bado haujafika, bali sasa hivi anatafuta udhamini ndani ya CCM.


Wakati huo, Wasira na mtia mwingine, Makongoro Nyerere, wameelezea kuridhika na namna wanavyoshiriki mchakato wa kusaka Urais kwa kutumia magari, tofauti na watia nia waliowekeza fedha nyingi kiasi cha kutumia usafiri wa angani katika maeneo mengi.


Waliyasema hayo walipokutana kwenye ofisi za CCM mkoa wa Mtwara, ambapo Makongoro, alirukaruka na kumkumbatia Wasira. Tukio hilo lilitafsiriwa kuwa ni ishara za umuhimu wa kufanya ushawishi kwa amani pasipo kuiathiri CCM, wanachama ama Watanzania kwa ujuma.


“Hizi ndizo siasa tunazozitaka ndani ya CCM na Tanzania yetyu, sio wagombea wengine wanaotumia utajiri na fedha zao kuwakandamiza wadogo na kuibua mafarakano kwenye jamii,” akasikika kiongozi mmoja wa CCM (jina tunalo) akisema.


Wasira, alikwenda pia katika mkoa wa Lindi ambapo alifadhiliwa. Leo (alhamis) ataelekea mkoani Mwanza kuendelea na ziara ya kuomba udhamini kwa wana-CCM wa mikoa ya kanda ya Ziwa Victoria.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni