Mwalimu
wa Timu ya Mchezo wa Watu wenye ulemavu wa Akili Zanzibar {Special
Olympic} Maalim Amour Ali Khamis akisoma risala wakati wa hafla fupi
ya kukabidhi medali za ushindi kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi kwenye mashindano ya Kitaifa yaliyofanyika Kibaha.
Makamu
Mwenyekiti wa Chama cha Michezo cha Watu wenye ulemavu wa Akili
Zanzibar Bibi Saada Hamad Ali akimkabidhi Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Medali 32 walizopata wachezaji wa Zanzibar katika
mashindano ya Kitaifa Mkoani Kibaha.
Balozi
Seif akimvisha Medali Mchezaji Fahad Juma Khamis ambae alishinda kwenye
mashindano ya Kitaifa yaliyofanyika Mkoani Pwani Tanzania Bara.
Mchezaji
Huzaima Haji Ali wa Timu ya Mchezo wa Watu wenye ulemavu wa Akili
Zanzibar akivishwa Medali na Balozi Seif baada ya kushinda mashindano ya
Kibaha Tanzania Bara.
Baadhi
ya wachezaji wa Timu ya Mchezo wa Watu wenye ulemavu wa Akili Zanzibar
wakifuatilia hotuba ya Balozi Seif ambaye hayupo pichani wakati
akiwapongeza baada ya kufanya vizuri kwenye mashindano yao.
Wa kwanza kutoka kulia ni mchezaji wa soka Mbarak Awesu Moh’d wa
Zanzibar aliyebahatika kuwa miongoni mwa Wachezaji wa Tanzania
watakaokwenda Nchini Marekani kushiriki mashindano ya Kimataifa.
Balozi
Seif akiwa katika picha ya pamoja na wachezaji wa Timu ya Mchezo wa
Watu wenye ulemavu wa Akili Zanzibar baada ya kuwapongeza kwa kuja na
ushindi Zanzibar.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameupongeza Uongozi wa
Chama cha Michezo cha Watu wenye ulemavu wa Akili Zanzibar {Special
Olympic} kwa jitihada uliochukuwa kwa kuiwezesha Timu ya Zanzibar
kurejea na ushindi mkubwa kwenye mashindano ya Taifa yaliyofanyika
Kibaha Tanzania.
Alisema
jina la Zanzibar tayari linaanza kuibika tena kwenye medani ya Michezo
katika Nyanja ya Kimataifa baada ya kufifia katika miaka ya nyuma
kutokana na kukosa kutoa wachezaji wenye kiwango kinachokubalika
Kimataifa.
Balozi
Seif Ali Iddi alitoa Pongezi hizo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar
baada ya kupokea Medani 32 ambazo kati ya hizo 17 za dhahabu, Tano za
Fedha na 10 za Shaba walizopata wachezaji wa Zanzibar kwenye mashindano
hayo.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar amefarajika kutokana na ushindi huo na
kushawishika kuwavisha nishani hizo baadhi ya wachezaji hao akiwemo
Mbarak Awesu Moh’d aliyefanikiwa kuchaguliwa katika Timu ya Taifa ya
Tanzania inayotarajiwa kushiriki mashindano ya Kimataifa ya Special
Olympic Nchini Marekani Mwezi uajo wa Julai mwaka huu.
Balozi
Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Ilani ya Chama
cha mwaka 2010 iliyotilia Mkazo Michezo itajitahidi kutoa msukumo katika
kuunga mkono michezo hasaya wachezaji vijana wenye mahitaji maalum.
Katika
kuunga mkono jitihada za Viongozi na wachezaji hao wa Special Olympic
Balozi Seif alitoa ahadi kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
itagharamia Tiketi kwa Mchezaji Mbarak Awesu Moh’d wa Zanzibar
aliyebahatika kuwa miongoni mwa Wachezaji wa Tanzania watakaokwenda
Nchini Marekani.
Akisoma
Risala ya wanamichezo hao Mwalimu wa Timu ya Mchezo wa Watu wenye
ulemavu wa Akili Zanzibar {Special Olympic} Maalim Amour Ali Khamis
alisema chama cha Mchezo huo kimesajiliwa Tarehe 12 Oktoba mwaka 2009
kwa lengo la kuendeleza michezo kwa watu wenye akili pungufu.
Maalim
Amour alisema ufinyu wa fedha unaokikabili chama cha mchezo huo
Zanzibar umechangia kukosa ushiriki sahihi wa wachezaji wa mchezo huo
kwa pande zote mbili za Zanzibar katika mashindano ya Kitaifa.
Mwalimu
huyo wa Timu ya Mchezo wa Watu wenye ulemavu wa Akili Zanzibar
{Special Olympic} kwa niaba ya Viongozi na wachezaji waliochini ya Chama
hicho ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa uamuzi wake wa
kuunga Mkono timu yao.
Alisema
jitihada hizo za Serikali kwa kushirikiana na wafadhili tofauti kutoka
Taasisi za Umma na Watu Binafsi zimewawezesha Vijana hao wa Zanzibar
kushiriki michezo mbali mbali ya Kitaifa na Kimataifa.
Akimkabidhi
Medali hizo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi,
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Michezo cha Watu wenye ulemavu wa Akili
Zanzibar Bibi Saada Hamad Ali alisema vitendo vya udhalilishaji
wanavyofanyiwa watoto wenye ulemavu wa akili hivi sasa vimekithiri mno.
Bibi
Saada alisema inasikitisha kuona baadhi ya wasimamizi wa sheria
wanakataa ushahidi unaotolewa na wazazi au walezi wa watoto wenye
ulemavu wa akili kwa kisingizio kwamba ushahidi kamili haujakamilika.
Alisema
jamii inaendelea kushuhudia udhalilishaji huo kwa kuwapa nguvu watu
waovu kuendeleza vitendo viovu kutokana na kuelewa kuwa wanaotendewa
vitendo hivyo kati yao wanashindwa kujieleza mahakamani kutokana na
ulemavu wao.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni