Matayarisho
ya awali ya maandalizi ya ujenzi wa Kiwanja cha Michezo cha Mao Tse tung
kiliopo Mperani Kikwajuni Mjini Zanzibar yameanza rasmi kwa hatua ya utafiti wa
uchunguzi wa udongo wa eneo hilo.
Mhandisi wa
Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Ali Mbarouk alieleza hayo wakati
akimpatia ufafanuzi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
aliyefanya ziara fupi ya kuangalia matayarisho hayo.
Mhandisi Ali
Mbaouk alimueleza Balozi Seif kwamba utafiti huo wa udongo unaofanywa kwa
kuchukuwa aina tofauti za udongo kwenye vishimo 34 vinavyochimbwa ndani ya eneo la uwanja huo unatarajiwa
kuchukuwa muda wa siku 20.
Alisema
udongo huo utafanyia utafiti wa kina na wataalamu waliobobea ambao kukamilikwa
kwake watatoa ripoti kamili itakayofuatiwa na utangazaji wa tenda kwa Makampuni
yatayokuwa tayari kujenga uwanja huo.
Alifahamisha
kwamba ujenzi kamili wa uwanja wa Mao Tse Tung unatarajiwa kuanza rasmi mwezi
wa Febuari mwaka 2016 chini ya ufadhili wa Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa
China.
Akitoa
ufafanuzi wa Ramani ya ujenzi wa uwanja huo Mhandisi Ali Barouk alimueleza
Balozi Seif kwamba uwanja huo utakapomalizika utakuwa na Viwanja viwili vya
mchezo wa soka, kimoja kitakachokidhi michezo ya Pete pamoja na Kikapu.
Alieleza
kwamba lipo eneo litakalotengwa maalum kwa michezo mbali mbali ya ndani { INDO
GAMES }, Majukwaa ya watazamaji eneo la watu Maarufu { VIP } pamoja na ofisi za
watendaji wa uwanja huo.
Akielezea
furaha yake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema
kukamilika kwa uwanja wa huo wa Mao Tse Tung kutasaidia kuupunguzia mzigo
mkubwa uwanja wa michezo wa Amani.
Balozi Seif
alisema uwanja wa Amani kwa sasa ndio pekee unaobeba michezo yote ya Kimataifa
na Kitaifa ,Sherehe tofauti ikiwemo ile kubwa ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja
na matamasha mbali mbali.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kati kati akisalimiana na wataalamu wa
Kichina wanaosimamia utafiti wa udongo katika uwanja wa Mao Tse Tung katika matayarisho ya awali na
maandalizi ya ujenzi wake.
Eneo la Uwanja wa Michezo wa Mao Tse Tung likionekana kuwa katika
maandalizi ya awali ya matayarisho ya ujenzi mpya unaotarajiwa kugharamiwa na
Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China.
Gari ya Kijiko likiwa katika harakati za uwekaji sawa eneo la
Uwanja wa Mao Tse Tung ili kupatana udongo kwa ajili ya kufanyiwa utafiti wa
kina kabla ya kuanza rasmi ujenzi wake.
Mhandisi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Ali
Mbarouk aliyepo kati kati akimuonyesha Balozi Seif ramani ya uwanja wa
Mao
utakavyokuwa baada ya kukamilika ujenzi.
Picha na –
OPMR – ZNZ.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni