Mkuu
wa Kambi ya Wakimbizi Nyarugusu iliyopo wilayani Kasulu, mkoani Kigoma,
Sospeter Christopher Boyo (aliyesimama mwenye shati la kitenge) akisoma
taarifa fupi ya Kambi ya Nyarugusu kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi, Mh. Mathias Chikawe (aliyeketi mwenye suti ya kijivu)
aliyeambatana na Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na
Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Alvaro
Rodriguez mara baada ya kuwasili kwenye kambi hiyo kujionea hali halisi
ya mazingira na changamoto zinazowakabili Waomba hifadhi wa Burundi na
Kongo. (Picha zote na Zainul Mzige wa modewjiblog)
Na Modewjiblog team, Kigoma
WAKATI
dunia kupitia Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanahangika kutanzua
changamoto za wakimbizi Nyarugusu, mkoani Kigoma imeelezwa kuwa idadi
kubwa ya Wakimbizi waliorejeshwa nchini Burundi kutoka kambi ya Mtabila
iliyoko Kigoma iliyofungwa rasmi Desemba, 2012 wameingia tena nchini na
kujazana katika makazi ya muda ya Nyarugusu wakiomba hifadhi.
Kauli
hiyo imetolewa na Mkuu wa Kambi ya Nyarugusu Sospter Christopher wakati
akizungumza na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi aliyekwenda kuangalia
hali halisi ya kambi ya Nyarugusu na Wakimbizi akiambatana na Maofisa wa
Umoja wa Mataifa akiwemo Mratibu wa Mashirika hayo nchini Alvaro
Rodriguez.
Kurejea kwa wingi kwa Wakimbizi
hao ni pigo kisaikolojia kwa watu ambao walirejeshwa nyumbani kwa
kuonekana kwamba hali ni shwari na walikuwa wameanza kuishi maisha ya
kawaida.
Mkuu
huyo wa kambi alisema idadi hiyo ikichanganyika na wengine imafanya
kambi kuhemewa na kuonekana haja ya kutafuta eneo jingine la kupiga
kambi kwa ajili ya Wakimbizi hao ambao mpaka mwishoni mwa wiki iliyopita
walikuwa zaidi ya elfu 51.
“ Kwa sababu tunapokea idadi kubwa
ya waomba hifadhi toka Burundi, tumekuwa tukiongeza idadi ya vituo vya
mapokezi ili kukidhi mahitaji ya kuwapokea wakati tukisubiri maelekezo
toka ngazi za juu za kuwahamishia Migunga Hills eneo linalopendekezwa
kufunguliwa kambi ya Nyarugusu B” alisema Christopher mbele ya Waziri
Chikawe.
Alisema
walianza kupokea waomba hifadhi hapo kambini kuanzia Aprili 29, 2015
kwa idadi ndogo kabisa ya watu 36, lakini idadi hiyo ilianza kuongezeka
siku hadi siku na kufikia Mei 27 mwaka huu idadi yao ilifikia 48,333,
idadi kubwa ikiwa wanawake na watoto.
Wakimbizi hao walikuwa wakipitia vituo vya Kigoma (27,638), Manyovu (4,439), Kilelema (1,603) na Kigadye (1,291).
Kambi hiyo yenye uwezo wa kubeba
watu 50,000 imeelemewa kwa sababu ya ujio mpya uliosababisha kuwepo kwa
Wakimbizi zaidi ya 106,410.
Kuna matatizo zaidi ya milipuko ya
wagonjwa kambi hii imechanganywa na Wakimbizi wa Kongo watu ambao
hawana utamaduni wa pamoja na kuonekana hatari ya kukabiliana kwa
kutosikilizana.
Aidha kambi hiyo pamoja na
kuwahifadhi waburundi wapo pia Wakimbizi kutoka Kongo wapatao 54,706;
Burundi,3261 ; Rwanda 72; Uganda 17; Sudan Kusini wanane; Kenya 7;
Somalia 3; Ethiopia 1; Zimbabwe 1; na Ivory coast 1.
Mkurugenzi
wa Idara ya huduma za Wakimbizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,
Harrison Mseke (wa pili kushoto) akizungumza jambo na Mratibu Mkazi wa
Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo
(UNDP), Alvaro Rodriguez (kushoto) huku Mkuu wa kambi mpya
inayotarajiwa kuanzishwa ya Nyarugusu B, Fredrick Nisajile (wa nne
kulia) akitoa maelezo kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mh. Mathias
Chikawe (wa tatu kushoto) mara tu baada ya kuwasili na kusomewa taarifa
kwenye kambi ya Nyarugusu wilayani Kasulu mkoani Kigoma. Wengine pichani
ni baadhi ya viongozi wa ulinzi na usalama wa wilaya ya Kasulu mkoani
Kigoma.
Akijibu
maswali ya waandishi wa habari walioambatana naye katika ziara hiyo
kuhusu hali ya baadae ya Wakimbizi wa Kongo ambao wapo nchini kwa
takribani miaka 19 sasa, Waziri Chikawe alisema kwamba serikali haina
mpango wa kuwapa uraia kwa sasa ingawa Marekani imesema itawachukua
Wakimbizi elfu 30 kuwapeleka kwao na kwingine duniani.
“hatuna
mpango wa kuwapa uraia kwa sasa…” alisema Chikawe na kusema kwamba kwa
kuondolewa kwa hao wengine kutasaidia kupunguza idadi yao katika kambi
hiyo.
Alisema
kwamba ni lengo la serikali kuhakikisha kwamba kambi hiyo inapunguzwa
ili kuweza kuchangia ipasavyo kwa hali bora ya Wakimbizi na kwamba
mchakato wa kuwaangalia waomba hifadhi kama wanafaa kuwa Wakimbizi
unaendelea.
Akizungumzia malalamiko ya
upatikanaji wa chakula, Waziri Chikawe alisema kwamba si kweli kuwa kuna
watu hawajapata chakula kwa siku saba la sivyo wangelikufa.
Alisema wengi wa Wakimbizi ni
watoto na kwamba wanapoingia nchini wanapewa vyakula vikavu (kama
biskuti) lakini wakishafika kambini wanapewa chakula kilichopikwa na
resheni ya siku 14 .
Alisisitiza kuwa kama kungelikuwa hakuna chakula watoto hao wasingeishi, labda kama wanataka kuongezewa chakula zaidi.
Kuhusu
ujenzi wa kambi mpya Migunga alisema kwamba wataalamu wanaangalia
barabara mbadala kwani iliyopo sasa pamoja na kuhitajika milioni 300
kuitengeneza lakini bado kila mvua itakapokuwa inanyesha itahitaji
kutengenezwa.
Naye
Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mtaifa la Kuhudumia Wakimbizi
(UNHCR), Joyce Mends-Cole katika mahojiano na waandishi wa habari
aliishukuru serikali ya Tanzania kwa kufungua mipaka ili Wakimbizi
waweze kuingia na kutoa eneo kwa ajili ya kambi mpya kutokana na ya sasa
kujaa sana.
Aidha aliishukuru serikali ya
Uingereza kwa kuwa ya kwanza kutoa misaada kwa ajili ya Wakimbizi hao na
kutarajia nchi nyingine kama Marekani itafanya hivyo mapema ili
kuisaidia serikali ya Tanzania katika kuhudumia waomba hifadhi.
Naye Mratibu wa Mashirika ya Umoja
wa Mataifa nchini, Alvaro Rodriguez amesema wanafanya kila
linalowezekana ili kupunguza idadi ya Wakimbizi katika kambi ya
Nyarugusu kwa kuwapatia eneo jingine la kujihifadhi.
Alisema kwa kuwatoa hapo
watasaidia shule zilizofungwa ambazo zinasomesha watoto kutoka kwa
Wakimbizi wa Kongo kurejea madarasani kukamilisha mtaala wao.
Mkuu wa kambi mpya
inayotarajiwa kuanzishwa ya Nyarugusu B, Fredrick Nisajile akifafanua
jambo kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mh. Mathias Chikawe wakati
akitembelea na kukagua maeneo mbalimbali ya Kambi ya Nyarugusu iliyopo
wilayani Kasulu, mkoani Kigoma.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi, Mh. Mathias Chikawe na Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa
Mataifa, Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP),
Alvaro Rodriguez pamoja na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mtaifa la
Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), Joyce Mends-Cole wakikagua sehemu
wanayolala Waomba hifadhi wanaoendelea kuwasili katika kambi ya
Nyarugusu ambayo inaelemewa kutokana na wingi wa Waomba hifadhi hao
wanaoendelea kumiminika mjini Kigoma.
Muonekano wa moja ya chumba
cha kulala familia za waomba hifadhi katika kambi ya Nyarugusu ambapo
kifika muda wa kulala wanatandika mkeka chini katika vumbi hilo jekundu
na kupata usingizi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi, Mh. Mathias Chikawe (mwenye suti ya kijivu), Mratibu Mkazi wa
Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo
(UNDP), Alvaro Rodriguez (wa pili kushoto) pamoja na Mwakilishi wa
Shirika la Umoja wa Mtaifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), Joyce
Mends-Cole (kushoto) wakisikiliza hoja mbalimbali kutoka kwa Waomba
hifadhi wanaohifadhiwa kwenye kambi ya Wakimbizi Nyarugusu iliyopo
wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma walipotembelea kambi hiyo kukagua kambi
hiyo na kuangalia changamoto mbalimbali zinazowakabili na namna ya
kuzitatua.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi, Mh. Mathias Chikawe (mwenye suti ya kijivu) akiteta jambo na
Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika
la Maendeleo (UNDP), Alvaro Rodriguez wakati walipotembelea kambi ya
Wakimbizi ya Nyarugusu iliyopo wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma mwishoni
mwa juma lililopita.
Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mh. Mathias Chikawe akigawa vifaa vya
matumizi ya nyumbani ambavyo ni Blangeti, Mkeka, Kontena la kuhifadhi
chakula na dumu la maji la lita 10 kwa mmoja wa Waomba hifadhi
waliowasili siku ya ziara ya kutembelea kambi ya Nyarugusu mwishoni mwa
juma wilayani Kasulu mkoani Kigoma. Anayeshuhudia tukio hilo ni Mratibu
Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la
Maendeleo (UNDP), Alvaro Rodriguez (mwenye shati jeupe).Kulia ni Mkuu wa
kambi mpya inayotarajiwa kuanzishwa ya Nyarugusu B, Fredrick Nisajile.
Waomba hifadhi na familia zoa wakiwa katika foleni ya kupokea vifaa hivyo.
Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mh. Mathias Chikawe akizungumza na Waomba
hifadhi katika kambi ya Nyarugusu wakati alipofanya ziara ya kutembelea
eneo hilo akiwa ameambatana na Mkuu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa
pamoja na Mwakilishi wa shirika la kuhudumia Wakimbizi nchini (UNHCR).
Mtaalam
wa Mahusiano na Mawasiliano wa Shirika la Umoja wa Mataifa (UN)
Tanzania, Hoyce Temu akizungumza na mmoja wa wakinamama anayeishi kwenye
kambi ya Wakimbizi Nyarugusu wakati wa ziara maalum ya kutembelea
maeneo hayo iliyohusisha Serikali ya Tanzania na Umoja wa Mataifa.
Mratibu
Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la
Maendeleo (UNDP), Alvaro Rodriguez na Mtaalam wa Mahusiano na
Mawasiliano wa Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) Tanzania, Hoyce Temu
wakibadilishana mawazo na mmoja wa wafanyakazi wa Shirika la Kimataifa
Ia Uhamiaji (I.O.M) (katikati) ambaye jina lake halikuweza kupatikana
kiurahisi katika kambi ya Wakimbizi ya Nyarugusu iliyopo wilayani Kasulu
mkoani Kigoma.
Mkurugenzi
wa Idara ya huduma za Wakimbizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,
Harrison Mseke (mwenye suti ya kijivu) akifafanua jambo kwa Mh. Mathias
Chikawe alipotembela katika chumba maalum kichotumika kufanya usajili
kwa Waomba hifadhi na familia zao kwa ajili ya kupewa hati ya kuwa
Wakimbizi kamili kama watatimiza vigezo vinavyohitajika. Aliyeketi kulia
ni Msajili wa Waomba hifadhi, Ndalo Charles Bogohe.
Zoezi la usajili likiendelea kwa familia za waomba hifadhi katika kambi ya Nyarugusu iliyopo wilayani Kasulu mkoani Kigoma.
Wakinamama wakiandaa chakula cha mchana kwa familia zao kama walivyokutwa na kamera ya modewjiblog.
Sehemu ya familia za Waomba
hifadhi katika kambi ya Wakimbizi Nyarugusu, wilayani Kasulu, mkoani
Geita wakiendelea kujipanga baada ya kuwasili kwenye eneo hilo.
Moja ya familia za waomba
hifadhi ikiwa imejipumzisha mara baada ya chakula cha mchana huku nyuso
zao zikionekana kuwa na furaha na matumaini mapya.
Hili ni eneo ambalo Waomba hifadhi kutoka nchini Burundi wa kambi ya Nyarugusu wakiteka maji safi kwa matumizi yao.
Mkurugenzi wa Idara ya huduma
za Wakimbizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Harrison Mseke
(kushoto) akizungumza jambo na Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa
Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP), Alvaro Rodriguez
(wa pili kushoto) wakati wakielekea kukagua vyumba vya madarasa katika
shule ya msingi Mapendo ambayo yamegeuzwa kuwa nyumba za kulala Waomba
hifadhi, kutokana na uhaba wa makazi ya kuishi kwenye maeneo ya kambi ya
Nyarugusu, wilayani Kasulu mkoani Kigoma. Wengine pichani ni baadhi ya
viongozi wa ulinzi na usalama wa wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma katika
msafara huo.
Baadhi ya Waomba hifadhi
katika kambi ya Wakimbizi Nyarugusu wakiwa wamempumzika huku wengine
wakipata chakula cha mchana kama walivyokutwa na kamera ya modewjiblog.
Kinababa nao hushiriki kuandaa chakula cha mchana kwa familia zao kama huyu aliyekutwa na kamera ya modewjiblog.
Eneo
la shule ya msingi Mapendo katika kambi ya Wakimbizi Nyarugusu ambalo
kwa sasa linatumika kuhifadhi Waomba hifadhi wanaoendelea kuwasili
nchini wakitokea Burundi kupitia mji wa Kigoma.
Madawati
ya wanafunzi katika shule ya msingi Mapendo yakiwa nje ya madarasa
yakitumika kuanikiwa nguo na huku wakati wa msimu wa mvua yakinyeshewa.
Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mh. Mathias Chikawe na Mratibu Mkazi wa
Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo
(UNDP), Alvaro Rodriguez wakibadilishana mawazo na wasimizi wa kambi
hizo za Nyarugusu wakati wa ziara ya siku moja wilayani Kasulu, mkoani
Kigoma.
Mratibu Mkazi wa Mashirika ya
Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP), Alvaro
Rodriguez (kushoto) akiwa ameambatana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi, Mh. Mathias Chikawe wakikagua eneo jipya litakaloitwa Nyarugusu B
lililotolewa na serikali kwa ajili ya Waomba hifadhi wanaoendelea
kumiminika mjini Kigoma ambalo liko mbioni kutengenezwa na kukamilika
ndani ya miezi 3 ijayo.
Eneo jipya la kambi ya
Nyarugusu B ambalo limetengwa na serikali ya Jamhuri ya Tanzania kwa
ajili ya makazi ya Waomba hifadhi wanataotenganishwa Burundi na Congo
mara tu baada ya kukamilika.
Muonekano
wa eneo jingine la makazi ya Waombahifadhi ndani ya kambi ya Wakimbizi
Nyarugusu iliyopo wilayani Kasulu, mkoani Kigoma.
Amani
na upendo itawale kati yetu……ndivyo wanavyosema kwa pamoja baadhi ya
watoto waomba hifadhi wakifurahia picha pamoja na Mratibu Mkazi wa
Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo
(UNDP), Alvaro Rodriguez.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni