Mbunge David Kafulila amepata mpinzani katika jimbo la Kigoma kusini
WAKATI
mchakato wa kutangaza nia ukiendelea kwa wagombea wa nafasi ya urais
nchini, Mwanasheria wa Halmashauri ya wilaya ya Kigoma mkoani Kigoma
Iddi Ndabhona ametangaza nia kuwania ubunge katika jimbo la Kigoma
Kusini wakati wa uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Akizungumza
alipopewa nafasi ya kusalimia wakati wa mkutano mkuu wa wakulima wa
tumbaku mkoani Kigoma, Ndabhona amesema kuwa anayo nafasi na uwezo wa
kuwatumikia wananchi wa jimbo la Kigoma Kusini na kuwaletea maendeleo.
Kwa sasa
jimbo hilo liko chini ya mbunge, David Kafulila kupitia chama cha NCCR –
Mageuzi ambaye ameonesha nia ya kugombea tena na mtangaza nia huyo
ametangaza kugombea kupitia Chama Cha Mapinduzi. Mwanasheria huyo ambaye
ni Mkurugenzi wa kampuni ya uwakili ya Lake Tanganyika Attorney and Law
Chambers alisema kuwa iwapo chama chake cha CCM kitampitishia kupitia
vikao rasmi ataweza kulirudisha jimbo hilo CCM. Wakati akitangaza nia ya
kugombea ubunge katika jimbo la Kigoma Kusini, tayari kamati ya ushauri
ya mkoa Kigoma imepitisha azimio la kuligawa jimbo hilo na kupata
majimbo mawili ya Buhingu na Uvinza. Kutokana na hali hiyo mwanasheria
huyo alisema kuwa iwapo tume ya Taifa ya uchaguzi itaridhia mapendekezo
ya kamati ya ushauri ya mkoa Kigoma kuhusu mgawanyo wa majimbo mkoani
Kigoma na majimbo hayo kugawanya atagombea kwa jimbo la Uvinza.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni