Clouds Media International yazindua huduma mpya ya kutafuta na kuunganisha (booking) wasanii kwenye shughuli mbalimbali za burudani.


·        Wasanii kutoka Afrika, Mashariki ya Kati na Asia kunufaika na huduma hii.

Abu Dhabi – Kampuni ya Clouds Media International leo imetangaza kuzindua huduma mpya ya kutafuta na kuwaunganisha wasanii kwenye nafasi za kutoa burudani kwenye matamasha na matukio mbalimbali.

Kazi hiyo ya kuunganisha na kuwatafutia wasanii nafasi ya kutoa burudani itakuwa chini ya Status Bookings ambayo ni kampuni dada ya Clouds Media Group.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Clouds Media, Joseph Kusaga, uzinduzi wa huduma hii ni muendelezo wa kawaida wa kukua kwa kampuni yake.

"Kwa kipindi cha miaka 15 iliyopita tumekuwa tukifanya kazi ya kuwatafuta na kuwapa nafasi ya kutoa burudani wasanii wakubwa kama Jay-Z, T.I., Ludacris, Rick Ross, T-Pain, Shaggy, Wayne Wonder, Fat Joe, Chaka Khan, Ja Rule pamoja na wasanii wakubwa wa Afrika kama P-Square, Iyanya, Diamond Platnumz, Davido, Waje, Vanessa Mdee, 2Face, Ali Kiba, Victoria Kimani, Avril na Patoranking kwa ajili ya tamasha letu la Fiesta, kwahiyo sasa ni wakati muafaka kutumia mahusiano mazuri tuliyonayo na wasanii pamoja na mameneja wao ili tuanzishe huduma hii kwenye maeneo ya masoko tunayoyahudumia," alisema Kusaga.

Tamasha la Fiesta linaloandaliwa na Primetime Promotions ni moja ya tamasha kubwa zaidi Afrika na sasa linaingia mwaka wa 15 likiwa na wahudhuriaji zaidi ya 400,000 kwa mwaka.

Huduma hii ya kutafuta na kuwaunganisha wasanii itakuwa inasimamiwa kutoka makao makuu ya Status Communications yaliyoko Abu Dhabi huku yakipata ushirikiano kutoka ofisi za Status zilizoko Dar es Salaam, Tanzania pamoja na Nairobi, Kenya.

Huduma hii itawapa nafasi waandaji wa shughuli za burudani pamoja na makampuni mbalimbali kuwasiliana na kupata wasanii mbalimbali kutoka chanzo kinachoaminika.


Afsa Mwendeshaji Mkuu wa kampuni ya Status anasema huu ni wakati muafaka wa kuingia kwenye huduma ya kuunganisha na kuwatafuta wasanii nafasi ya kuburudisha.  

"Kwa sasa wasanii wakubwa wa kiafrika wanahitajika sana kwenye sehemu nyingi duniani na sio barani Afrika pekee kwahiyo hii ni nafasi ya muhimu lakini pia kumekuwa na ongezeko la makampuni mengine ambayo sio waaminifu wanaojishughulisha na wasanii ambao huchukua fedha za waandaji wa matamasha bila kuwapa huduma ya wasanii husika," alisema Omari Salisbury.

Salisbury alisema huduma hii itajumuisha wasanii wa kimataifa pamoja na wale wa kiafrika.

“Tuna mahusiano ya moja kwa moja na wasanii mbalimbali kama Ludacris, T.I. na Rick Ross pamoja na wengine kutoka Afrika kama Davido, Wiz Kid, Diamond Platnumz na Victoria Kimani,” alisema Salisbury.

Salisbury pia alisema huduma yao ya kuunganisha na kuwatafutia wasanii nafasi ya kutoa burudani itaenda mbali zaidi kwa kuwapa nafasi hata madijei na waburudishaji wengine wa sanaa za burudani.

“Huduma yetu haitashia tu kwa wasanii bali itagusa pia aina nyingine za sanaa, na kimsingi sisi ndio tunawawakilisha Dijei Pierra wa Kenya pamoja na Dijei Supreme La Rock wa Marekani,” alisema Salisbury.

Kwa wale wanaohitaji huduma za kutafutiwa wasanii wanaombwa kutembelea www.StatusBookings.com au watume barua pepe kwenda Info@StatusBookings.com.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni