Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad
BARAZA
Kuu la uongozi la Chama cha Wananchi (CUF) limemchagua kwa kura zote 56
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kuwa mgombea wa nafasi ya
urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama hicho katika uchaguzi mkuu wa
Oktoba mwaka huu.
Akizungumza
na waandishi wa habari hapo katika ofisi ndogo ya CUF Shangani mjini
hapa, Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa chama hicho, Omar Ali Shehe
alisema maalim amepita bila ya mpinzani katika kinyang’anyiro cha nafasi
ya urais wa Zanzibar kutokana na imani kubwa ya wanachama wa chama
hicho dhidi yake.
Alisema
uamuzi huo sasa utamfanya Maalim Seif kumsubiri mgombea kutoka katika
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa ajili ya kinyang’anyiro cha nafasi hiyo.
“Chama
cha CUF kimebadilisha utaratibu zamani jina la mgombea wa nafasi ya
urais linaamuliwa na mkutano mkuu wa chama, lakini tumebadilisha maamuzi
hayo kutokana na gharama kubwa za kuitisha mkutano katika chama
kichanga kama hiki,” alisema.
Mapema
Shehe alitangaza majina ya mwisho ya wagombea wa nafasi ya Uwakilishi na
Ubunge katika chama cha CUF katika majimbo 50 ya Unguja na Pemba.
Katika
majina hayo yanaonesha kwamba Mbunge wa Mkanyageni, Mohamed Habib Mnyaa
ambaye aliangushwa katika kura za maoni amerudishwa kuwania nafasi hiyo
katika jimbo hilo.
Aidha,
Mbunge wa jimbo la Mji Mkongwe kwa tiketi ya CUF, Mohamed Ibrahim Sanya
ameondolewa katika kinyang’anyiro hicho na nafasi yake kuchukuliwa na
mwandishi mkongwe aliyekuwa akifanya kazi katika Shirika la Utangazaji
la Uingereza (BBC), Ali Saleh.
Sanya
aliibuka nafasi ya kwanza katika mchakato wa kura za maoni huku
akimuangusha vibaya kwa kupata kura 21 Ali Saleh ambaye alishika nafasi
ya tatu.
Mkurugenzi
wa Mipango na Uchaguzi alipoulizwa kuhusu maamuzi ya Baraza la Kuu la
Uongozi wa CUF, alisema baadhi ya vigezo muhimu vilipewa kipaumbele cha
kwanza ikiwemo suala zima la matokeo ya kura za maoni kutoka katika
majimbo ya uchaguzi kwa wanachama.
Aidha,
alisema suala la utekelezaji na kukubalika katika jamii ni suala la pili
ambalo lilizingatiwa kwa lengo la kuona mgombea anafanikiwa na
kukivusha chama hadi kupata ushindi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni