TUME ya Taifa ya
 Uchaguzi (NEC) imesema watu 152 watafikishwa mahakamani mkoani Njombe 
kutokana na kujiandikisha mara mbili katika Daftari la Kudumu la 
Wapigakura kwa mfumo mpya wa ‘Biometric Voter Registration Kit’ (BVR).
Aidha, imeeleza 
kuwa kata 130 zimeongezeka kutokana na Tawala za Mikoa na Serikali za 
Mitaa (TAMISEMI) kufanya mabadiliko ya kiutawala katika kata, 
vijiji,vitongoji na Mitaa hivyo kulazimu NEC kuhairisha kwa wiki moja 
uandikishaji wa daftari uliokuwa ukianza jana kwa baadhi ya mikoa.
Kaimu Mkurugenzi
 wa Uchaguzi NEC, Dk Sisti Cariah alisema hayo jana wakati akielezea 
kuahirishwa kwa wiki moja uandikishaji hadi Juni 16 mwaka huu kwa mikoa 
ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara na Mara.
Akizungumzia 
suala la watu kujiandikisha mara mbili, alisema katika mkoa wa Njombe 
ambao Daftari hilo liko tayari na wiki ijayo litawekwa wazi kwa siku 
tano na kisha kufanyiwa marekebisho kwa siku moja na wamebaini watu 152 
waliojiandikisha mara mbili.
Alisema watu hao
 wametenda kosa la jinai na watashtakiwa, huku akitoa onyo kwa watu 
kuacha kufanya hivyo kwani mashine za BVR zinagundua wanaojiandikisha 
zaidi ya mara moja.
Alisema wataweka wazi baadhi ya watu waliojiandikisha mara mbili kwenye mikoa yote, ambayo iko tayari.
Alisema mpaka 
sasa tayari wamepokea madaftari yaliyokamilika ya uandikishaji kwa mikoa
 ya Lindi, Mtwara na Ruvuma huku uandikishaji huo ukiwa umekamilika kwa 
asilimia 50 na wanatarajia kukamilisha uandikishaji mwezi Julai.
Akizungumzia 
suala la mipaka ya kiutawala, yaliyofanywa na Tamisemi, Cariah alisema 
ilifanyika wiki mbili zilizopita katika mikoa mbalimbali, jambo 
lililosababisha kusitisha uandikishaji katika mikoa hiyo huku mikoa 
ambayo tayari uandikishaji umefanyika watarekebisha wakati wa kuweka 
wazi daftari.
“Katika kupiga 
kura lazima kitambulisho kioneshe kata anayokaa mtu kwa mabadiliko haya 
yamefanya kata kubadilika na kuongezeka 130 hivyo kufanya madiwani 
watakaopigiwa kura kuongezeka hivyo kata kuendana na kitambulisho,” 
alisema.
Alisisitiza kuwa
 kutokana na changamoto hiyo mikoa hiyo mitano, itaanza uandikishaji 
pamoja na mikoa ya Tanga na Morogoro Juni 16 mwaka huu na baadaye Juni 
25,mwaka huu wataanza uandikishaji katika mkoa wa Pwani.
Alisema sasa wanatumia Mashine za BVR 8,000 walizokuwa wanahitaji pamoja na vipuri vyake vyote ziliwasili yangu mwezi uliopita.
Alisema katika 
mkoa wa Dar es Salaam uandikishaji utaanza Julai2 mwaka huu kwa kutumia 
BVR zaidi ya 3,000, ambazo kila moja ina uwezo wa kuandikisha watu 120 
na hiyo itatokana na kuwa mikoa nane, uandikishaji utakuwa umemalizika 
na zote kutumika katika mikoa ya Pwani na Dar es Salaam.
“Jijini Dar es 
Salaam sehemu zenye watu wengi kutakuwa na mashine hizo nyingi huku 
vituo vyote, vikifunguliwa kwa mara moja ikifuatiwa na Zanzibar, ambapo 
wataandikisha waliokosa sifa za kuandikishwa katika Daftari la ukaazi 
kwa ajili ya kupiga kura ya kumchagua Rais wa Muungano”alisema.
Akizungumzia 
changamoto ya watu kusubiri kwa muda mrefu katika vituo vya 
kujiandikisha, alisema hiyo inatokana na kuwa Printa za kusafisha picha 
zinatakiwa kubadilishwa kila baada ya wapigakura 400 kutokana na vumbi 
na muda huo wtau uona kama mashine zimeharibika lakini ni utaratibu wa 
kawaida.
Cariah alisema 
uandikishaji umekamilika kw amikoa mitano ya Njombe, Lindi, Mtwara, 
Ruvuma na Iringa na imefanikiwa kwa kiasi kikubwa na wanaendelea katika 
mikoa 12 sasa ambayo ni Katavi, Rukwa, Mbeya, Dodoma, Singida, Kigoma, 
Kagera, Simiyu, Mwanza, Geita na Shinyanga.
Akizungumzia 
mafanikio ya mikoa hiyo kuwa takwimu ilikuwa kuandikisha wapigakura 
518,230 na waliandikisha watu 529,224, Mtwara walitakiwa 732,465 
waliandikisha 727,565, Ruvuma wapigakura 783,296 waliandikishwa 826,779 
na Iringa wapigakura 524,390 waliandikishwa 526,006.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni