Ndugu zangu wana-CCM na Watanzania wenzangu,
Hii ni siku muhimu kwangu na kwa nchi yetu. Leo nimeamua kuwaita
 ili kuwatangazia rasmi Watanzania wenzangu azma yangu ya kutaka kuomba 
ridhaa ya chama chetu, Chama Cha Mapinduzi (CCM), niweze kuteuliwa kuwa 
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Nasema hii ni siku muhimu kwangu kwa sababu naamini historia 
yangu itainakili kama ni siku ambayo kwa mara ya pili katika maisha 
yangu nimejitokeza kuwania kuiongoza nchi yetu kupitia chama chetu. Mara
 ya kwanza ilikuwa ni mwaka 1995 wakati wa uchaguzi wa kwanza wa vyama 
vingi hapa nchini nilipojitokeza nikiwa pamoja na Rais Jakaya Kikwete; 
wakati ule sote tulikuwa wanasiasa vijana. Tulikwenda pamoja kuchukua 
fomu ndani ya Chama na baadaye tukafanya mazungumzo ya pamoja na 
waandishi wa habari. Tulileta hamasa kubwa pale tulipofanya jambo ambalo
 halikuzoeleka kwa Watanzania kwa kutangaza kwamba yeyote atakayepita 
kati ya wawili sisi basi mwenzake ambaye hatafanikiwa angemuunga mkono.
Ningeweza kujitokeza tena mwaka 2005 lakini nikaamua kwa dhati kabisa kumuunga mkono moja kwa moja Rais Jakaya Kikwete.
  Nikiwa Mwenyekiti wa Kampeni niliwaongoza wenzangu kufanikisha
 ushindi mkubwa wa mgombea tuliyemuunga mkono na baadaye ushindi mkubwa 
wa asilimia 80 wa Chama Cha Mapinduzi kwenye uchaguzi mkuu wa 2005.
Nitaeleza kwa nini nimeamua kujitokeza tena mwaka huu na kwa 
nini naamini mimi ndiye mtu sahihi wa kuiongoza nchi yetu wakati huu. 
Mpaka hapa itoshe tu kuwaeleza ni kwa kwa nini naamini leo ni siku 
muhimu kwangu.
Lakini nasema ni siku muhimu kwa nchi yetu pia. Nasema hivyokwa 
sababu naamini inajibu wito wa mahitaji ya sasa ya uongozi wa Taifa letu
 wa kumpata kiongozi imara atakayewaongoza Watanzania kujenga taifa 
imara. Na hili pia nitalieleza kwa kina.
Hali  ya  Nchi  na  Matarajio  ya  Watu:
Miaka 48 iliyopita katika jiji hili la Arusha, Baba wa Taifa, 
Mwalimu Julius Kambarage alianzisha mchakato wa kujenga taifa huru 
kiuchumi na kupiga vita maadui umaskini, ujinga na maradhi kwakutumia 
silaha ya kujitegemea. 
Leo hii, wakati taifa likijiandaa kwa Uchaguzi Mkuu ujao, hatuna
 budi kutafakari tulikotoka, tulipo na tunapotaka kwenda ili tuweze 
kubuni upya mikakati ya kuhitimisha azma aliyo kuwa nayo Mwalimu, ili 
tujenge taifa huru, lenye utulivu, mshikamano, amani na maendeleo.
Nchi yetu hivi sasa inapita katika kipindi kigumu cha mpito 
katika maeneo yote makuu ya maisha yetu – katika siasa, katika uchumi na
 katika maisha ya kijamii.
Kisiasa, tumeshuhudia kuongezeka kwa vuguvugu la mfumo wa vyama 
vingi ambapo ushindani kati ya vyama vya siasa unazidi kuwa mkali na kwa
 bahati mbaya kufikia sura ya kuonekana kama vile ni mapambano ya watu 
binafsi badala ya mapambano ya sera na dira ya kuongoza nchi. 
Tunashuhudia kuongezeka uhasama binafsi kati ya wanasiasa ndani 
ya chama kimoja kimoja na pia kati ya wanasiasa wa chama kimoja dhidi ya
 kingine. Kadiri siku zinavyokwenda, hali inazidi kuzorota na ikiachiwa 
kuendelea nchi yetu inaweza kujikuta mahali pabaya. 
Kukua kwa ushindani ni jambo jema linalokomaza na kurutubisha 
demokrasia yetu na tukiwa na ushindani wenye afya unaweza kuwa chachu ya
 kuleta mabadiliko mema kwa wananchi na kupelekea kuongezeka kwa kasi ya
 maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika nchi yetu. 
Kinyume chake ushindani unaochukua sura ya chuki binafsi au 
kukomoana na hata kulipizana visasi si ushindani wenye tija na tunapaswa
 kuutafutia tiba. 
Tunahitaji uongozi imara kusimamia kipindi cha mpito kutoka 
siasa muflisi za aina hii na kuelekea kwenye siasa mpya zinazoimarisha 
ushindani wenye tija unaojikita katika kushindana katika kuwapatia 
huduma bora Watanzania.
Kiuchumi, tumeshuhudia ukuaji mzuri na kuongezeka kwa mapato ya 
ndani ya Serikali na uimarishaji wa mfumo wa uwajibikaji na ulipaji 
kodi.
  Kwa upande mwengine, Serikali ya Rais BenjaminiMkapa na Rais 
Jakaya Kikwete imefanya kazi kubwa katika uendelezaji wa sekta ya mafuta
 na gesi asilia ambapo kiwango kikubwa cha gesi asilia kimegunduliwa.
  Tanzania sasa imekuwa ni miongoni mwa nchi zinazovutia 
uwekezaji mkubwa katika sekta hiyo ambayo inatajwa kwamba inaweza kuja 
kubadilisha kabisa maisha ya Watanzania. 
Hata hivyo, kipindi hiki cha mpito kuelekea ujenzi wa uchumi wa 
kisasa kimeshuhudia kuongezeka kwa hofu na wasiwasi miongoni mwa 
wananchi kwamba hawatonufaika naukuaji huu wa uchumi na ugunduzi wa 
utajiri mkubwa wa gesi asilia.
  Kwa upande mwingine, vijana wanataka kuona ukuaji wa uchumi na
 ugunduzi wa utajiri huo unakwenda sambamba na uzalishaji wa ajira zenye
 maana ili waweze kukabiliana na changamoto za maisha yao.
  Niliwahi kusema kwamba tatizo la ukosefu wa ajira likiachiwa bila ya kutafutiwa ufumbuzi imara ni bomu linalosubiri kulipuka. 
Vijana wasio na ajira hupoteza matumaini na ni rahisi 
kughilibiwa kuingiza nchi katika machafuko.Tunahitaji uongozi imara 
kuweza kuikabili hali hiyo na kuitafutia suluhisho maridhawa.
Kijamii, kipindi cha karibuni tumeshuhudia mabadiliko makubwa ya
 tabia miongoni mwa raia katika hali ambayo haijawahi kuwa sehemu ya 
utamaduni wa Watanzania.
  Kumekuwa na ongezeko la kutisha la matukio ya uhalifu 
linalokwenda sambamba na wananchi kuonyesha wanapoteza imani na taasisi 
zinazosimamia sheria na usalama na kuamua kujichukulia sheria mikononi 
mwao. 
Kumeripotiwa matukio mengi yakiwemo ya kuvamiwa vituo vya 
polisi, askari kupigwa na kuporwa silaha, matumizi makubwa ya nguvu 
katika utatuzi wa migogoro mbalimbali hasa ile ya kijamii, mathalani 
migogoro ya wakulima na wafugaji, mivutano ya kidini na pia mivutano 
baina ya viongozi wa dini wenyewe kwa wenyewe na baina ya viongozi wa 
dini na wale wa Serikali.
  Matokeo yakemshikamano wa taifa nao unaingia majaribuni. Mara 
nyingine wananchi wanatuuliza viongozi iwapo hii ndiyo nchi tuliyoachiwa
 na waasisi wetu. Tunahitaji uongozi imara wa kukabiliana na changamoto 
hizi na kurudisha mshikamano wa taifa letu na watu wake.
Watanzania  Wanataka  Mabadiliko;
Ndugu zangu, mnaweza kujiuliza kwa nini nimeyaeleza yote hayo na
 yana mahusiano gani na dhamira yangu ya kutangaza nia ya kutaka 
kuiongoza nchi yetu kupitia CCM?
Nimeyaeleza haya kwa sababu haya na matukio mengine yanayoendelea nchini yamepelekea Watanzania kutaka mabadiliko. 
Watanzania wanataka mabadiliko yatakayowawezesha kuzishinda 
changamoto hizi na kuwaongoza kujenga Taifa imara ambalo kila mwananchi 
wake anaishi akiwa na uhakika wa mahitaji yake muhimu na papo hapo 
akijiridhisha kwamba leo yake ni bora kuliko jana yake, na kesho yake 
itakuwa bora zaidi kuliko leo yake.
  Kwa maneno mengine, Watanzania wanahitaji mabadiliko 
yatakayowapa uongozi imara unaoweza kuwaongoza kujenga taifaimara. Hii 
ndio Safari ya Matumaini.
Chama chetu, Chama Cha Mapinduzi (CCM), na watangulizi wake, 
TANU na ASP, kimepata bahati ya kuungwa mkono na Watanzania tokea enzi 
za kupigania uhuru, wakati wa Uhuru wa Tanganyika na Mapinduzi ya 
Zanzibar, na pia miaka yote tokea Uhuru, Mapinduzi na hatimaye Muungano 
wetu. Watanzania hawajawahi kushuhudia chama kingine kikiongoza Serikali
 zetu zaidi ya CCM. Wamekiamini na wanaendelea kukiamini.
  Hata katika yale majimbo machache ya nchi yetu ambayo 
hatukufanya vizuri katika uchaguzi, ukiangalia kwa undani utaona si 
kwamba watu wa maeneo hayo wana matatizo na CCM kama Chama bali wana 
matatizo na baadhi ya viongozi ambao walishindwa kukiwakilisha vyema 
Chama na kutambua matakwa ya wananchi hao.
Mimi naamini kwamba hata katika kipindi hiki ambapo Watanzania 
wanaonekana kutaka mabadiliko bado wanaendelea kuamini kwamba watayapata
 mabadiliko hayo ndani ya CCM. 
Lakini kama alivyotupa wasia Baba wa Taifa, Mwalimu Julius 
Nyerere, mwaka 1995 wakati wa uchaguzi mkuu wa kwanza chini ya mfumo wa 
vyama vingi hapa nchini, Watanzania wasipoyapata mabadiliko hayo ndani 
ya CCM watayatafuta nje ya CCM. 
Mimi naamini kwamba CCM tunao uwezo wa kuwapa Watanzania 
mabadiliko wanayoyataka. Tuwape imani na imani hiyo iwe ni ya dhati na 
ya ukweli kwamba CCM inao uwezo wa kuwapa uongozi imara wanaouhitaji kwa
 ajili ya kujenga taifa imara.
Vyama vya siasa vinajumuisha watu na vinaongozwa na watu. Moja 
ya hulka ya binadamu ni kubadilika kulingana na mahitaji ya mazingira 
anayoishi.
  Kwa maneno mengine, binadamu ni ‘dynamic’. Kwa sababu hiyo basi, hata vyama vya siasa vinapaswa kuwa ‘dynamic’.
  CCM haijapata kuwa na upungufu wa sifa ya ‘dynamism’. Kwa 
zaidi ya miongo mitano sasa, CCM (na kabla yake TANU na ASP) iliweza 
kubadili dira na mwelekeo wake ili kwenda sambamba na mahitaji ya 
Watanzania ya wakati husika. 
Ndiyo maana tumepita katika vipindi tofauti vya mpito kwa mafanikio makubwa licha ya changamoto nyingi zilizotukabili. 
Tanzania imeendelea kuwa nchi ya amani licha ya kubadili mfumo 
wetu wa siasa kutoka ule wa chama kimoja kuja vyama vingi; licha ya 
kubadili mwelekeo wa uchumi wetu kutoka ule wa dola kumiliki njia zote 
kuu za uchumi kuja katika uchumi wa soko unaozingatia ushiriki mpana wa 
Watanzania wa matabaka yote; na hata karibuni kabisa katika mchakato wa 
kuipatia nchi yetu Katiba mpya.
Tanzania tumeweza kufanya mabadiliko ya uongozi mara nne katika 
hali ya amani na maelewano, jambo ambalo nchi nyingi za Afrika 
zimeshindwa.
  Ni imani yangu kwamba tukijikubalisha tunaweza tena kuwapa Watanzania wanachokitaka katika zama hizi za sasa.
  Lakini ni lazima tuoneshe dhamira hiyo kwa dhati ili, kama 
alivyotuasa Mwalimu Nyerere, Watanzania wasiyatafute mabadiliko hayo nje
 ya CCM. 
Nasisitiza tena kwamba CCM inao uwezo wa kuwapa Watanzania 
mabadiliko wanayoyataka, lakini pia wananchi wana hiali kuchagua 
mabadiliko wanayoyataka.
Uongozi  unaohitajika  kuleta  mabadiliko  yanayotakiwa:
Rais Jakaya Kikwete amefanya kazi kubwa katika kipindi chake na 
kama ambavyo amekuwa akisisitiza mara kwa mara katika hotuba zake za 
karibuni ni kwamba yeye ametekeleza wajibu wake kwa kuweka misingi imara
 ya ujenzi wa Taifa la kisasa lenye uchumi madhubuti na unaoweza kukua 
kwa kasi.
  Amesema anamwachia atakayemkabidhi uongozi wa nchi yetu baada ya yeye kumaliza muda wake kuendeleza pale atakapoachia.
Kwa maoni yangu ili kuifanya kazi hiyo na kuzikabili changamoto nilizozieleza, nchi yetu inahitaji uongozi wenye sifa zifuatazo:
–  Uongozi wenye uthubutu, usioogopa kufanya kufanya maamuzi magumu;
–    Uongozi thabiti na usioyumba;
–    Uongozi makini na mahiri;
–    Uongozi wenye ubunifu na wenye upeo mkubwa;
–   Uongozi utakaozikabili changamoto kifua mbele na siyo kuzikimbia;
–    Uongozi unaoamini katika mfumo shirikishi katika ujenzi wa Taifa;
–    Uongozi unaozingatia muda katika kutekeleza majukumu yake.
Naamini pia kwamba wananchi wanataka Rais ajaye wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania awe na sifa kuu zifuatazo:
–    Aweze kuwaunganisha Watanzania (kukabiliana na viashiria vya migawanyiko ya aina mbali mbali inayoinyemelea Tanzania);
–    Aweze kuja na sera na mikakati ya kuinua uchumi wa Tanzania
 na kukuza pato la Mtanzania;ikiwemo kupunguza tofauti ya kipato kati ya
 aliyekuwanacho na wasiokuwanacho;
–     Aweze kuja na sera na mikakati ya kuzalisha ajira kwa vijana wetu;
–     Aweze kutokomeza mianya ya rushwa kwa vitendo;
–    Aweze kuwa mfano wa kuchapa kazi na kuwajibika;
–     Asimamie nidhamu ya matumizi ndani ya Serikali;
–     Aweze kusimamia ukusanyaji wa mapato ya Serikali;
–     Aweze kutumia fursa yetu ya kijiografia kibiashara
Uongozi  Imara,Taifa  Imara
Naamini kwamba uongozi wa juu wa nchi katika nafasi ya Urais si 
kazi ya lelemama na unahitaji utashi. Kabla hata ya kutakiwa na wenzako 
ni lazima kwanza wewe mwenyewe uamini na uwaaminishe wenzio kwamba unao 
uwezo wa kuwaongoza wananchi wenzako. Na katika hilo, rekodi yako ni 
lazima izungumze na kulithibitisha hilo.
Binafsi nina hazina ya uzoefu na rekodi njema ya matokeo ya kazi
 nilizozifanya katika uongozi na utumishi wa umma ndani ya CCM na ndani 
ya Serikali. Nilianza kazi nikiwa Katibu Msaidizi wa CCM katika mikoa ya
 Shinyanga, Arusha na Moshi.
  Nimekuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa na Kamati Kuu ya 
CCM. Niliingia Bungeni mwaka 1985 na baadae mzee wangu, Rais Ali Hassan 
Mwinyi, akaniamini kwa kuniteua kuwa Waziri. 
Nimekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Waziri wa Ardhi, 
Makaazi na Maendeleo ya Miji, Waziri wa Mazingira, Waziri wa Maji na 
hatimaye Waziri Mkuu.
Miongoni mwa mafanikio ninayojivunia katika uongozi na utumishi 
wangu, na ambayo Watanzania wanayatambua na naamini wanayathamini, ni 
pamoja na:
–    Nikiwa Waziri wa Maji chini ya uongozi mahiri wa Rais 
Mkapa,tulithubutu kushawishi na kuongoza hatua za kukataa kufungika na 
makubaliano yaliyowekwa na wakoloni ambayo yalikuwa yanazizuia nchi 
zilizopakana na Ziwa Victoria zisiweze kufaidika ipasavyo na maji ya 
Ziwa hilo. Leo hii ndugu zangu wa Kanda ya Ziwa wanafaidika na ujasiri 
wetu katika kukabiliana na suala hilo zito.
–    Nikiwa Waziri wa Mazingira, tulipanda miti mingi zaidi 
kuliko wakati mwingine wowote tokea Uhuru na pia kuwakabili kikamilifu 
na kuwachukulia hatua waliochafua na kuharibu mazingira.
–    Nikiwa Waziri Mkuu, tulisimamia agizo la Rais Kikwete na 
kufanikisha utekelezaji wake ndani ya miaka miwili kwa kujenga shule 
nyingi za sekondari kuliko wakati mwingine wowote tokea Uhuru.
–    Kipindi hicho hicho, tulisimamia agizo la Rais Kikwete la 
kuanzisha Chuo Kikuu cha Dodoma na kuhakikisha kinakamilishwa kwa 
wakati. Leo hii Chuo Kikuu hicho ni fahari ya Tanzania.
Tunapomtafuta Rais wa Jamhuri ya Muungano ni lazima tukumbuke 
kwamba tunamtafuta mtu ambaye atakuwa pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi
 ya Ulinzi na Usalama katika nchi yetu. Na kwa Chama Cha Mapinduzi 
tunamtafuta mtu ambaye atakuwa pia Mwenyekiti wa Chama chetu.
Naamini kwa vigezo vyote, nina kila sifa ya kubeba dhamana hizo 
nzito. Katika mambo ambayo najivunia na sitoyasahau katika historia 
yangu ni kushiriki kwangu kuilinda nchi yangu pale ilipohitajika. 
Nilishiriki kikamilifu katika Vita vya Kagera nikiwa miongoni 
askari wa mstari wa mbele wa mapambano. Nikiwa Mbunge nilipata heshima 
ya kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama. Naamini Watanzania 
hawatakuwa na wasiwasi wa usalama wao nikiwa Amiri Jeshi Mkuu.
Nimeeleza uzoefu wangu kwenye Chama na huo hauhitaji maelezo 
zaidi. Ninakijua vyema Chama Cha Mapinduzi kiasi cha kutosha kabisa 
kukiongoza kama Mwenyekiti wake pale wakati utakapofika.
  Wana-CCM wanajua nikikabidhiwa uongozi, Chama chetu kitakuwa chini ya nahodha madhubuti, mzoefu na asiyeyumba.
Kutokana na rekodi yangu hii, naamini ninazo sifa za kuwaongoza 
Watanzania wenzangu katika zama mpya za ujenzi wa Taifa la kisasa lenye 
watu wazalendo walioshikamana na lenye uchumi imara unaomnufaisha kila 
Mtanzania. Naamini ninao uwezo wa kuwapa Watanzania Uongozi imara kwa 
ajili ya ujenzi wa Taifa Imara.
Dira  yangu  na  Matarajio  ya  Watanzania
Mfumo tuliojiwekea hapa nchini unaelekeza kila chama cha siasa 
kinachosimamisha mgombea Urais na kinachowania kuongoza nchi yetu kuja 
na Ilani ya Uchaguzi ambayo ndiyo inayoweka misingi ya sera 
zitakazofuatwa na Serikali itakayoongozwa na chama hicho pale kinapopewa
 ridhaa ya kuongoza nchi.
  Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimekuwa ni cha kupigiwa mfano 
katika kutayarisha Ilani bora na ndiyo maana mara zote kimepewa ridhaa 
ya kuongoza nchi yetu. Tumefanya hivyo tokea enzi za mfumo wa chama 
kimoja na tumeendelea kufanya vizuri katika mfumo wa kushindanisha sera 
kupitia vyama vingi. 
Najua kwamba Ilani ya CCM ya mwaka 2015 imo katika hatua za 
mwisho za kukamilishwa na itakapopata baraka za vikao vya Chama itakuwa 
ndiyo msingi wa utendaji wa Serikali ya Awamu ya Tano itakayochaguliwa 
Oktoba mwaka huu. 
Hata hivyo, naamini pia kwamba mgombea mwenyewe anayetaka ridhaa
 ya Chama na ya Watanzania kuongoza nchi naye anapaswa kueleza dira 
yake.
Mimi, baada ya kutafakari kwa kina changamoto tulizo nazo na 
matarajio na matumaini waliyo nayo Watanzania, naamini kwamba Uongozi 
imara unaolenga kujenga Taifa imara unapaswa kuwa na dira yenye malengo 
yafuatayo:
–    Kuimarisha Muungano wetu kwa kuyashughulikia 
yanayotutenganisha na kuyafanyia kazi ili yasivuruge yale 
yanayotuunganisha ambayo ni mengi zaidi na makubwa zaidi.
–    Kushughulikia matumizi mabaya ya siasa za udini na ukabila 
kwa kuimarisha siasa zilizoshiba uzalendo na zenye kutuelekeza kwenye 
Utanzania wetu.
–    Kujenga uchumi imara na wa kisasa, na ambao ni shirikishi 
unaomnufaisha kila Mtanzania aliyeko mjini au kijijini. Tunapaswa 
kubadili hali tuliyo nayo sasa ambapo Kilimo kinaonekana kama 
kimesahauliwa na wakulima wetu wanaonekana wanakata tamaa.
Wafugaji na wavuvi nao wanahisi sekta zao hazijapewa umuhimu 
unaostahiki. Tunahitaji kuondokana na hali iliyopo sasa ya kuwa Taifa 
linalouza malighafi na badala yake kuwa Taifa linalosindika na kusarifu 
mazao na kutengeneza wenyewe bidhaa zitokanazo na malighafi yake. 
Ndani ya miaka mitano ijayo tutahakikishatunaiondolea Tanzania 
sifa ya kusafirisha malighafi na badala yake kusindika mazao 
yanayozalishwa hapa nchini kama pamba, kahawa, chai na korosho na 
kuyaongezea thamani (value addition).Mkakati huu utazalisha ajira nyingi
 na kuongeza mapato ya fedha za kigeni nchini.
  Tunahitaji kujielekeza kwenye kujenga viwanda na kuleta ajira.
 Tuna vivutio vingi sana vya utalii lakini bado Tanzania inapitwa na 
nchi kama Afrika Kusini katika kuingiza idadi kubwa ya watalii.
  Kwa nini nchi kama Dubai iweze kuvutia watalii kwa mamilioni 
na Tanzania tushindwe? Tunapaswa kukabiliana kikamilifu na hisia 
zilizopo miongoni mwa wananchi kwamba Tanzania hainufaiki ipasavyo na 
utajiri wa rasilimali zake nyingi ilizo nazo. 
Tutajipanga zaidi kuhakikisha tunanufaika kama nchi na rasilimali zetu kama madini na gesi asilia. Hii ndio Safari ya Matumaini
–    Kukuza kipato cha wananchi na kunyanyua hali za maisha ya 
watu wetu. Tunapaswa kuhakikisha kuwa ukuaji wa uchumi tunaouzungumzia 
unamnufaisha Mtanzania aliyeko mjini au kijijini na kwamba hali za 
Watanzania wa matabaka yote zinanyanyuka na kwamba wanaridhika na kuuona
 uhalisi wa ukuaji wa maendeleo tunayoyazungumzia.
–    Kuondokana na sifa mbaya ya kuwa Taifa ombaomba. Kwa wingi 
wa rasilimali tulizo nazo na neema ya ardhi, maziwa, mito na bahari 
Tanzania tuna kila sababu ya kuacha kuwa ‘bakuli la ombaomba’ na badala 
yake kuwa ‘mkoba wa neema’ katika Afrika.We can transform our nation from being the begging bowl to become the bread basket of Africa.
– Kujenga mfumo mpya wa elimu unaojielekeza kuwatayarisha vijana
 wetu waweze kuajirika, kujiajiri na kushindana katika soko la ajira. 
Tumepiga hatua kadhaa katika elimu lakini kiwango cha elimu bado
 ni hafifu. Pamoja na kuwa na shahada (degrees), bado wahitimu wetu 
hawawezi kushindana kwenye soko la ajira. 
Wakati tunazungumzia kuunganisha soko la ajira katika Afrika 
Mashariki,hatuna budi kujikita kubadili mfumo wetu wa elimu na 
kuuelekeza kwenye mafunzo ya ufundi na stadi yanayowajenga wahitimu wetu
 kuwa wabunifu na wenye kujiamini katika kukabiliana na changamoto za 
maendeleo duniani.
–    Kuhakikisha tunakabiliana ipasavyo na kulipunguza kwa kiasi
 kikubwa kama si kulimaliza kabisa tatizo la upatikanaji wa maji safi na
 salama. Ni jambo la kusikitisha kwamba tumezungukwa na mito na maziwa 
lakini bado watu wetu hawana maji ya kunywa hata ndani ya Dar es Salaam.
–    Kujenga na kusimamia mfumo imara wa kutekeleza sera na 
sheria tunazozitunga na kuzipitisha kwa lengo la kumtumikia Mtanzania na
 kumjengea uwezo wa kubadili maisha yake ili tuweze kwenda sambamba na 
viwango vya kimataifa. Tanzania imepata sera na sheria nzuri sana lakini
 utekelezaji wake umekuwa hafifu. 
Tumekuwa wepesi wa kutunga sera na sheria lakini wazito mno wa 
kuzitekeleza na kuzisimamia. Uongozi imara wenye kulenga ujenzi wa Taifa
 imara utahakikisha tunakuwa mfano wa utekelezaji wa sera na sheria 
tulizo nazo na mpya zitakazotungwa kukabiliana na malengo tuliyojiwekea.
Mambo haya niliyoyaeleza hapa ndiyo yatakayokuwa msingi mkuu wa 
utendaji wa Serikali nitakayoiongoza pale nitakapopewa ridhaa ya kubeba 
bendera ya CCM katika nafasi ya Urais na pia nitakapopewa ridhaa ya 
kuliongoza Taifa letu kupitia uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Ramani  ya  Uongozi  Imara  Ninaouamini 9 Leadership Roadmap)
Kama nilivyotangulia kusema, kazi ya kuongoza nchi si lelemama 
na hasa unapoongozwa na dhamira ya dhati na msukumo wa ndani ya nafsi 
unaojielekeza kubadilisha maisha ya wananchi wenzako waliokuamini 
uwaongoze. Kwa vyovyote vile, hiyo haiwezi kuwa kazi ya mtu mmoja. Ni 
kazi ya pamoja.
  Lakini ili muweze kufanya kazi kama timu moja iliyojipanga 
kisawasawa kuleta mabadiliko yanayohitajika na ili muweze kweli kutoa 
Uongozi imara unaojikita kujenga Taifa imara hapana budi kiongozi mkuu 
anayeongoza timu hiyo aweke ramani anayokusudia kuifuata katika kutoa 
uongoziimara anaoukusudia yaani ‘Leadership Roadmap’.
Pamoja na kuwa sehemu ya uongozi huko nyuma, kutakuwa na maamuzi
 na matumaini mapya. Ramani ya uongozi imaraninayokusudia kuutoa kwa 
wenzangu na ambayo nitaitumia kuiongoza timu yangu katika kuwatumikia 
Watanzania wenzangu itajikita katika maeneo yafuatayo:
1. Kurejea kwenye Katiba katika kuainisha nia, dhamira na 
malengo yetu ya kujenga jamii inayozingatia misingi ya demokrasia, udugu
 na amani. Muhimu katika hili ni kukemea tabia mbaya zinazochochea 
mfarakano katika jamii kama vile matumizi mabaya ya siasa za udini na 
ukabila.
Aidha moja ya misingi muhimu ya Katiba ni Muungano wetu. Itakuwa
 dhamira yangu kuimarisha misingi ya Muungano pamoja na udugu wa damu 
nahistoria ya ushirikiano iliyojengwa na waasisi wetu, Baba wa Taifa 
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Sheikh Amri Abeid Karume na 
kuyaenzi Mapinduzi matukufu ya Zanzibar.
2. Kujenga fikra mpya za kurejesha kujiamini na kufufua azma ya 
kujitegemea kama Taifa. Ni dhahiri kuwa pamoja na rasilimali zetu, bado 
Tanzania ni taifa tegemezi. Bado tunajidanganya kuwa wafadhili 
watatujengea nchi. Tukumbuke, nchi zinajengwa nawananchi wake. 
Nasi pia lazima tujikomboe kifkra na tuondokane na utamaduni wa 
kuwa tegemezi. Tuanze kwa kujipiga kifua kwa kujiamini kuwa tunaweza 
kujitegemea na kuijenga Tanzania sisi wenyewe.Kujiamini na kujitegemea 
ndio uhuru wa kweli.
3. Kujenga uzalendo, uadilifu ikiwa ni pamoja na kuimarisha 
uwazi katika shughuli zote za serikali na kupambana na rushwa.Watanzania
 tumepoteza uzalendo kwa kiasi kikubwa. Kuna vitendo vinavyoashiria kuwa
 hatuipendi tena nchi yetu. 
Tunashabikia wizi na rushwa. Inabidi turejee kwenye misingi ya 
taifa letu misingi ya uadilifu na uzalendo. Tukumbuke kuwa hatuwezi 
kujenga uchumi wa kisasa kama tutaruhusu rushwa ishamiri.
  Wawekezaji hawataleta mitaji yao kwa wingi kama rushwa 
itaendelea kutawala katika huduma serikali na wananchi hawawezi kupata 
huduma bora kama rushwa itaendelea kutawala. Ni lazima tuipinge rushwa 
kwa vitendo sio maneno.
4. Kujenga Serikali madhubuti, makini na yenye nidhamu 
inayoendeshwa kwa misingi ya sheria, uwazi na uwajibikaji.Maendeleo ya 
watu hayawezekani bila serikali kusimamiautekelezaji sera na miradi na 
kuleta ufanisi katika kutoa huduma na kusimamia maendeleo. Tumekuwa 
wepesi wa kutunga sera lakini wazito wa kuzitekeleza na kuzisimamia.
5. Kuleta msukumo mpya wa ushirikiano kati ya serikali na sekta 
binafsi katika ujenzi wa uchumi wa kisasa na unaojitegemea. Sekta 
binafsi ndiyo nyenzo ya uchumi imara. Inazalisha mali, ajira na 
kuchangia kwa kiasi kikubwa katika pato la taifa kwa kulipa kodi.
  Ilisekta hii itoe mchango unaotakiwa katika maendeleo ni 
lazima ifanye kazi na serikali kwa karibu. Tukumbuke, bila uchumi 
imarahakuna huduma bora!
6. Uwekezaji katika huduma za jamii. Elimu na afya bora, 
mazingira, makazi safi na maji salama ndiyo mihimili ya maendeleo ya 
watu.
  Hii inawezekana tu iwapo serikali itakuwa na sera na utashi wa
 kuutambua uboreshaji wa huduma za jamii kama ndiyo lengo kuu la 
maendeleo ya nchi. Serikali nitayoiongoza itahakikisha kuwa kila 
Mtanzania anapata elimu bora na inayogharamiwa na serikali kama mimi na 
wenzangu tulivyopata. 
Wakatitunazungumzia kuunganisha soko la ajira katika Afrika 
Mashariki, hatuna budi kurekebisha mfumo wetu wa elimu na kuuelekeza 
kwenye mafunzo ya ufundi na ustadi yanayowajenga wahitimu wetu kuwa 
wabunifu, wenye kujiamini, wenye uwezo kushindana katika soko la ajira 
na wa kujiajiri. Napenda kusisitiza kuwa elimu ndiyo muhimili wa 
maendeleo, ndiyo mkombozi wa kweli wa binadamu. Mimi ni mfano hai wa 
ukombozi wa elimu. 
Elimu ndiyoimenivusha kutoka kijijini kwetu Ngarash na kunipa 
upeo wa kitaifa. Mama akiwa na elimu atajua umuhimu wa kumpeleka mwanae 
shule, anapata lishe bora na chanjo stahili na kuwa anaishi katika 
mazingira safi. Elimu ndilo jibu la umaskini, maradhi na ujinga.Taifa lililo elimika ni taifa lenye maendeleo.
7. Kujenga uchumi shirikishi unaolenga kuondoa umaskini.Mkakati 
wa kuondoa umaskini Tanzania lazima ujikite kwenye nguzo za ushiriki wa 
kila Mtanzania katika uchumi wa taifa. 
Kwa misingi hii, tukiweza kupunguza umaskini, tutaweza pia 
kupunguzatofauti za kipato ambazo tukiziacha ziendelee kukua kwa kiasi 
cha sasa, zinaweza kuhatarisha utulivu na amani katika jamii yetu.Uchumi
 shirikishi ndio silaha dhidi ya umaskini.
8. Kuimarisha ulinzi wa nchi na usalama wa raia na ujirani 
mwema.Itakuwa nia yangu kuimarisha misingi iliyojengwa kulinda na 
kudumisha umoja na amani nchini. 
Kadhalika, nitahakikisha kuwa usalama wa mipaka ya Tanzania 
unaimarishwa kwa misingi ya ujirani mwema na kutanzua migogoro na 
matatatizo yoyote na nchi jirani, kwa njia ya diplomasia na mazungumzo.
Hitimisho:
Hii ndiyo misingi na dira ya uongozi wangu. Nachelea kusema kuwa
 haitakuwa kazi rahisi. Lakini kwa ushirikiano wa kila mmoja na maamuzi 
magumu, yote yanawezekana.
  Tumeona nchi nyingi zilizosimamiwa na utawala thabiti wa 
serikali za kimaendeleo zikikabili na kupunguza umaskini katika kizazi 
kimoja. Kama mataifa mengine yamefanikiwa, tena bila raslimali kama 
zetu, kwa nini sisi tushindwe? 
Tuna kila sababu ya kufanya maamuzi magumu sasa ili kuwajengea 
Watanzania matumaini mapya ya maendeleo. Naomba nisisitize kuwa katika 
uongozi wangu hakutakuwa na nafasi ya majungu, na visasi. Hatutaangalia 
nyuma bali tutasonga mbele kwani ndicho Watanzania wanakitarajiakutoka 
kwa uongozi uliojengwa kwenye misingi bora.
Ndugu Watanzania:-
Ni maono yangu kuwa siku si nyingi nchi yetu itaanza safari yenye uelekeo wa matumaini na neema tele kwa wananchi.
Ni maono yangu kuwa siku si nyingi sisi kama Watanzania kwa 
umoja wetu tutajivunia kuishi katika nchi tunayoipenda na inayoendeshwa 
kwa misingi ya utawala bora, chini ya serikali ya kimaendeleo 
iliyojengwa kwenye fikra mpya za uzalendo, uadilifu, utendaji na 
uwajibikaji.
Ni maono yangu kuwa Peke yangu sitaweza, lakini kwa maamuzi 
magumu na ushirikiano wa kila mmoja wetu ikiwa ni pamoja na wagombea 
wenzangu ndani ya CCM, inawezekana kuanza safari hii ya Matumaini Mapya.
Kabla ya kumaliza hotuba yangu hii fupi, kuna mambo matatu ningependa kuyaweka wazi hapa.
La kwanza, linahusu msingi wa uongozi ninaouamini na ambao 
nimeusema mara kadhaa hapa. Msingi huo ni UWAJIBIKAJI.Watanzania 
wananifahamu mimi si mtu wa maneno, ni mtu wa vitendo. Naamini kwa dhati
 kabisa kwamba huwezi kuwa na Uongozi imara utakaoweza kusimamia ujenzi 
wa Taifa imara iwapo huna ujasiri wa kuwajibika. Mimi nimeongoza kwa 
mfano, na pale ilipobidi, nilikubali kuwajibika na kubeba dhamana ya 
uongozinilipojiuzulu nafasi ya Waziri Mkuu.
La pili, mimi si mtu wa visasi. Siamini katika kuangalia ya 
nyuma. Yaliyopita si ndwele, tugange yajayo. Na kwa nini tuangalie nyuma
 wakati kama taifa tuna kazi kubwa sana mbele yetu inayohitaji kufanywa?
 Mimi ni Mkristo; najifunza kutoka kwa Bwana Yesu ambaye alipoulizwa: 
“Nisamehe mara ngapi?” Alijibu, “Samehe mara sabini mara saba”. Nitaenzi
 na kudumisha utamaduni huu wenye sura ya utu na heshima.
La Tatu, natambua kwamba dhamana ya Urais ni shughuli nzito hasa
 kwa taifa ambalo lina changamoto nyingi. Nataka niwahakikishie 
Watanzania wenzangu kwamba afya yangu ni njema kuweza kuwatumikia katika
 jukumu hili zito. Pamoja na vijineno vinavyosemwa pembeni, mimi 
mwenyewe ndiye ninayejijua zaidi. Nawahakikishia kuwa nisingekuja hapa 
leo na kueleza nia yangu hii ingekuwa sina uhakika na afya yangu.
Natoa RAI kwa Chama changu cha CCM, nadhani umefika wakati 
kwamba tutende tofauti na mazoea, watu wote walionyesha nia ya kutaka 
kuongoza, liundwe jopo la madaktari wa ndani na nje ya nchi tupimwe afya
 zetu, kwa hili najitolea kuwa wa KWANZA KUPIMWA afya yangu
Safari tuianze leo, hatuna kesho nyingine.
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni