ZOEZI LA UANDIKISHAJI WAPIGAKURA KWENYE DAFTARI LA KUDUMU LAWA VITUKO ARUSHA

ZOEZI la kuandikisha wananchi kwenye daftari la kudumu la wapiga kura jijini Arusha, ni sarakasi tupu kutokana na kutawaliwa na vituko vya kila aina vinavyolenga kuvuruga au kuchelewesha zoezi hilo..

Hayo yamebainishwa jana kwenye kikao cha pamoja cha wadau cha kutathimini zoezi hilo ambao ni viongozi wa vyama vya siasa, CCM,Chadema ,TLP, maafisa wakuu waandikishaji , kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa mbele ya waziri wa  nchi ofisi ya waziri mkuu, Sera, Uratibu na bunge, Jenesta Muhagama.

Akichangia ,mwakilishi wa TLP,Michael Kivuyo, amevitaja baadhi ya vituko hivyo kuwa ni pamoja na vijana kutumia zoezi hilo kama sehemu ya kujipatia kipato.

Kivuyo, amesema kuwa   kuna baadhi ya vijana wanajipanga kwenye msitari na  wanashika nafasi zaidi ya moja ambazo huziuza kwa watu wenye haraka kwa shilingi 30,000 walianza kuziuza shilingi  shilingi 5,000 kwa nafasi moja .

Aidha wanawake wanatumia mbinu ya kubeba  watoto wachanga ili iwe ni rahisi kuandikishwa sanjari na kujifunga vitambaa tumboni na kuvalia magauni makubwa ili kuonyesha kuwa ni wajawazito hivyo wapewe kipaumbele katika kuandikishwa.

Kivuyo, amesema katika kata ya Sokon,one na kwenye kituo cha Sinoni,wapo wengine wanalala kituoni kwa siku tatu kwa ajili ya kuweza kuandikishwa kutokana na wingi wa watu na jinsi zoezi linavyoenda kwa kusua sua akaomba siku ziongezwe..

Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Arusha, Godbless Lema,(Chadema)amesema  sasa kuna mtindo umezuka ambapo wanawake na wanaume kwenye mistari wanaweka mawe na kuandika namba wakisubiri kuandikishwa.

Vituko hivyo vinatokana na zoezi kufanyika kwa polepo sana kutokana na uwezo mdogo wa mashine kuandikisha watu 100 kwa siku wakati kituoni kuna watu 500 nae akaomba siku ziongezwe ili kuandkisha wengi.

Karist Lazaro, katibu Chadema, mkoa, amesema  tatizo lingine ni wingi wa watu katika kata ya sokon one ,sinoni, Osunyai  na Mriet.

Amesema kuna vituo  vina watu 2000 hadi 2800  na uwezo wa mashine ni kuandika watu 120 tu hivyo zoezi halitafanikiwa kwa ufanisi mkubwa kutokana na upungufu wa vifaa na wataalamu hali hiyo inawafanya watu walale vituoni .

Lazaro,amesema kuwa baadhi ya polisi wanaosimamia zoezi hilo wanapokea rushwa ya shilingi 5000 ili kuruhusu wananchi kujiandikisha.

Kwa upande wake katibu wa ccm, mkoa, Alphonce Kinamhala,amesema kuwa zoezi hilo lina umuhimu  wake mfumo huo mpya wa uandikishaji unakwamishwa na uchache wa vifaa na ugeni wa teknolojia kwa waandikishaji.

Amesema kuwa zoezi hilo pia linakwamishwa  na hali ya hewa kuwepo kwa mawingu kutokana vinatumia mwanga wa jua wakati kwa sasa Arusha hakuna jua  la kutosha anga limezingirwa na mawingu kwa muda mrefu hivyo jua linaonekana kwa nadra .

Ametolea mfano kuwa jimbo la Arumeru, mashariki alikuta mashine zimezimika kutokana na hali ya hewa kuwa ya mawingu na hivyo kukosekana kwa jua kuanzia June 17 hadi 19 hivyo zoezi lilishindikana.

Kinamhala, amebainisha Katika kata ya King’ori ni vituo kumi tu kati ya 25 ndivyo vinaandikisha huku vingine vikishindwa kutekeleza zoezi hilo.

Amesema kituo cha Sinoni cha jijini Arusha wazee wamekata tama ya kuandikishwa kutokana na zoezi kusua sua.

Hivyo akaomba siku zaidi ziongezwe ili kuwezesha wananchi wote wenye sifa wanaandikishwa .

Kwa upande wake Mkurugenzi wa jiji Idd Juma, ambae ni afisa mwandikishaji mkuu amesema katika kukabiliana na wingi wa watu kwenye vituo, halmashauri June 19 imepokea mashine za BVR 90,toka tume ya taifa ya uchaguzi ambazo zitapelekwa kwenye vituo ambavyo vina watu wengi ili kuondoa msongamani.

Amesema vifaa hivyo vimepatikana kutokana na halmashauri kupeleleka maombi tume ya kuongezewa vifaa hivyo .

Kwa upande wake Waziri ameruka viunzi alipotakiwa atangaze nyongeza ya siku za kuandikisha ,badala yake akaagiza maafisa wakuu waandikishaji na vyama vya siasa kukaa pamoja na kutathimnini zoezi hilo na ndipo watoe ombi kwa tume kuongezewa siku

Pia alikataa asipangiwe ratiba ya kutembelea vituo ili akashuhudie zoezi hilo badala yake alisema ataenda kwenye vituo ambavyo ataona vinafaa lakini sio ratiba ya kupangiwa.

Waziri, ameagiza mkurugenzi wa jiji kuwa na vikao vya mara kwa mara na wadau wa zoezi hilo ambao ni vyama vya siasa  na kufanya tathimini ya zoezi hilo na iwapo kama kuna kero ambazo hawaziwezi kuzitatua wawasiliane na tume pamoja na kumpatia waziri taarifa.
‘’Katika zoezi hili kila mwananchi mwenye sifa ataandikishwa hakuna atakae achwa ‘’Waziri alisisitiza .

Waziri akatumia fursa hiyo kumuagiza mkurugenzi wa jiji kuondoa waandikishaji wasio na tija kwa kuwa ni mzigo, na na wanaofanya vizuri wahamishiwe kwenye vituo vyenye watu wengi.

Amevitaka vyama vya siasa kutokuendesha mapambano ambayo yatasababisha kukwamisha zoezi hilo bali washirikiane kutatua changamoto zilizopo kwenye zoezi hilo.
 
 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni