mail.google.comNyumba ya watumishi wa Kituo cha Afya cha Mkuyuni ambayo imefunguliwa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Ndugu Juma Khatib Chum ili watumishi hao waweze kuishi karibu na Kituo hicho. …………………………………………………… Na. Andrew Tangazo Chimesela (Morogoro) Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, imefanikiwa kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa malaria kwa asilimia 8 ukilinganisha na maambukizi ya ugonjwa huo mwaka 2014. Hayo yamebainishwa hivi karibuni na Dkt. Mwanahamisi Yahya ambaye ni Kaimu mganga wa kituo cha Afya cha Mkuyuni Wilaya ya Morogoro wakati akiwasilisha taarifa ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria kwa kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Ndugu Juma Khatib Chum. Dkt. Mwanahamisi amesema, mapambano dhidi ya malaria Katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro ni moja ya Kipaumbele kinachotiliwa mkazo na Halmashauri hiyo kupitia Idara ya Afya, jitihada zilizoleta matokeo chanya ya kushusha maambukizi ya ugonjwa huo kwa asilimia Nane. “Hali ya maambukizi ya ugonjwa wa malaria katika Halmashauri yetu imeshuka kwa asilimia Nane kutoka asilimia 56 mwaka 2014 hadi asilimia 48 mwaka 2015”, matokeo haya yametokana na jitihada za Halmashauri ikishirikiana na wadau mbalimbali ”.aliongeza Dkt. Yahya. Dkt. Yahya amesema, Kituo cha Afya cha Mkuyuni na Zahanati zilizopo katika Tarafa ya Mkuyuni vimeendeleza mapambano dhidi ya Malaria kwa kutoa Elimu kwa akimama Wajawazito ili kuzuia maambukizi ya malaria kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto. Jitihada nyingine zilizofanywa katika kupunguza mambukizi ya Malaria kushirikiana na Wadau mbalimbali ni pamoja na kuhamasisha jamii kutumia kikamilifu vyandarua vilivyotiwa viwatilifu na kusafisha mazingira ili kuondoa mazalia ya mbu wanaosababisha malaria. Aidha, Dkt. Yahya alitaja lengo la mapambano dhidi ya Malaria kuwa ni kupunguza maambukizi, magonjwa na vifo vitokanavyo na ugonjwa wa malaria katika jamii kwa kutoa Elimu na huduma Bora za Afya kupitia vituo vya Afya na Zahanati. Sambamba na Kiongozi wa Mbio za Mwenge kitaifa Ndugu Juma Khatib Chum kupokea Taarifa hiyo ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria, alifungua nyumba ya mtumishi wa kituo cha Afya cha Mkuyuni iliyojengwa kwa gharama ya shilingi 135,000,000.00. Miradi mingine ya maendeleo iliyopitiwa na mwenge huo ni pamoja na mradi wa utunzaji mazingira Kijiji cha Kiloka, mradi wa maji na usafi wa mazingira wa Kijiji cha Changa na mradi wa Ufugaji bora wa nyuki uliopo kijiji cha Kikundi. Miradi mingine ya maendeleo iliyopitiwa na Mwenge huo ni mradi wa ujenzi wa Ofisi ya Kijiji cha Mtego wa SImba, mradi wa mashamba ya Kikundi cha Vijana wakulima wa mahindi na mradi wa ujenzi wa Ofisi ya Vicoba Kikundi cha Upendo. Mwenge wa uhuru umeingia siku yake ya tatu kukimbizwa katika Mkoa wa Morogoro ambapo leo umekimbizwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro na kupitia miradi saba ya Maendeleo yenye thamani ya shilingi 323,142,000.00.

mail.google.com

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni