Rais Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na viongozi wa jumuiya ya watanzania waishio nchini Sweden jijini Helsinki.
Rais mpya
 ajaye nchini Tanzania anakabiliwa na changamoto kubwa ya kuhakikisha 
Tanzania itaendelea kubakia kuwa moja kwa kudumisha Umoja wetu na Amani 
kwani Tanzania inatokana na muungano wa nchi mbili.
Rais 
Jakaya Kikwete ameyasema hayo jijini Stockholm – Sweden ambapo alikuwa 
akiongea na watanzania waishio Sweden mara baada ya kuwasili na kuanza 
ziara ya kikazi ya siku 3, kuanzia tarehe 3 – 5 Juni,2015.
“Hapa 
tulipofikia lazima kuhakikisha Taifa linakuwa moja, kuna vyama, na 
makabila mbalimbali, lazima uhakikishe Nchi inabaki moja”. Rais 
amesisitiza.
Watanzania
 mbalimbali walioko nchini Sweden kwa ajili ya shughuli za kikazi, 
kimasomo na ambao wanaishi nchini Sweden, walifika kumpokea na 
kumsalimia Rais Kikwete ambapo pia wamemsomea risala ambayo pamoja na 
vitu vingine wametaka kujua kuhusu haki yao ya kupiga kura katika 
uchaguzi Mkuu ujao.
“Swala 
hili linategemea Tume ya Uchaguzi, likiwekewa utaratibu linawezekana. 
Taratibu zake hazijawekwa, lakini ninaamini kuwa uchaguzi ujao unakuwa 
uchaguzi wa mwisho ambao watanzania wanaoishi nje hawapigi kura”. Rais 
amesema.
Rais 
Kikwete pia ameelezea matumaini yake kuwa Tanzania itapata kiongozi 
mzuri na kuelezea mafanikio ambayo serikali yake imeyapata na kutumaini 
kuwa yatadumishwa na kuendelezwa na Rais ajaye.
Mapema 
akisoma risala ya watanzania, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watanzania Nchini
 Sweden Bw. Tengo Kilumanga, amempongeza Rais Kikwete kwa kuridhia na 
kuonesha nia ya dhati ya kumaliza kipindi cha uongozi wake na kuwa mfano
 bora katika ukanda wa Afrika Mashariki.
“Tunakupongeza
 mheshimiwa Rais, viongozi wengi katika Bara la Afrika huwa hawaagi, 
umefanya kitendo cha kishujaa sana. Viongozi wa Afrika huwa hawaagi kwa 
sababu siku ya kuondoka madarakani huwa haijulikani”. Amesema Bwana 
Kilumanga. “Hii inaonesha wewe sio Mtu wa kupenda madaraka”. Ameongeza.
Hii ni 
ziara ya kwanza ya Rais Kikwete ya kuaga Nchi wahisani na wenza katika 
maendeleo na Rais ameanzia Nchi za Nordic kwa sababu ya historia na 
uhusiano wa Nchi hizi kwa Tanzania tangu kupata Uhuru wake.
Rais 
Kikwete anaendelea na ziara yake nchini Sweden ambapo anatarajia kufanya
 mazungumzo na wafanyabiashara na wawekezaji mbalimbali kwa lengo la 
kuwahamasisha kuja kuwekeza nchini Tanzania.
Imetolewa na;
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
Stockholm – Sweden
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni