Mahmoud Ahmad Monduli
Monduli,Uongozi
wa halmashauri ya wilaya ya Monduli mkoani Arusha umeingia lawamani
mara baada ya wakazi wa kijiji cha Engeruka kuushutumu ya kwamba umekuwa
ukikusanya mapato ya vivutio vya utalii ndani ya kijiji hicho bila kuwapa gawio lolote pamoja na wao kuwa
walinzi wa rasilimali hiyo.
Mapato hayo yanatokana
na vivutio vya kihistoria vya magofu ya
Engaruka ambayo yanasadikika kuwa ni mabaki ya makazi ya watu wa zamani ambao
waliishi eneo hilo miaka 500 iliyopita.
Akizungumza kwa niaba
ya kijiji hicho mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Engaruka Juu,Mohammed
Yusuph alisema kwamba pamoja na halmashauri ya Monduli kukusanya mapato
mbalimbali kupitia vivutio hivyo lakini kijiji chao hakinufaiki na rasilimali
hiyo.
“Tumeshalipigia kelele
sana suala hili lakini sisi kama kijiji pamoja na kutunza vivutio hivyo lakini hatunufaiki
na chochote “alisema Yusuph
Hatahivyo,alisisitiza
kwamba wameshachukua hatua mbalimbali za kufika mbele ya halmashauri hiyo kujua
namna watakavyonufaiki na rasilimali
hiyo lakini hadi sasa hakuna majibu ya uhakika.
Hatahivyo,msimamizi
mkuu wa eneo hilo la kihistoria,Israel Mollel alisema kwamba uongozi wa halmashauri
hiyo uliweka uzio na kutoza kila mtalii kiasi cha $10 sawa na sh,13000 katika
maneo ya Engaruka,Gilai na Engaresero kama ada ya kiingilio lakini wao kama
wasimamizi hawaambulii chochote.
Alisema
kwambatangu utaratibu huo uanzishwe
umechangia kushuka kwa idadi ya watalii wanaotembelea eneo hilo ambapo miaka ya
nyuma walikuwa wakipokea watalii 50 kwa siku lakini kwa sasa hupokea watalii 10
kwa siku.
Akijibu malalamiko hayo
mwenyekiti wa halmashauri ya Monduli,Isaack Joseph maarufu kama Kadogoo alisema
kwamba hana taarifa kuhusu suala hilo lakini uongozi wake utafuatilia ili kujua
kama hawapokei gawio lolote.
Alifafanua kwamba
halmashauri yake ilitoa kiasi cha sh,2 milioni kwa kila kata mwaka jana kama
gawio la fedha za makusanyo ya vivutio mbalimbali vya utalii na watafuatilia
kujua kama fedha hizo zilifika au la.
Hatahivyo,alisema kwamba
halmashauri yao kwa kushirikiana na halmashauri za wilaya ya Karatu,Longido na Ngorongoro
wameweka utaratibu wa ukusanyaji wa mapato ya vivutio vyote vya utalii
vilivyomo ndani ya wilaya hizo ambapo mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro(NCAA)
itakuwa ikikusanya mapato hayo kwa utaratibu waliojipangia ili kudhibiti mapato
hayo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni