Msimamizi
Mkuu wa Mradi wa usafirishaji wa umeme mkubwa, maarufu kama ‘Backbone’,
Mhandisi Khalid James (aliyenyoosha mkono), akitoa maelezo kwa Naibu
Waziri wa Nishati na Madini Dkt Medard Kalemani (wa pili kutoka
kulia-mbele), kuhusu upanuzi wa Kituo cha kupoza umeme cha Iringa ili
kuwezesha Kituo hicho kupokea umeme mkubwa wa Backbone.
Msimamizi
Mkuu wa Kituo cha kupoza umeme cha Iringa, Theopist Semanini akimweleza
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (wa tatu kutoka
kushoto), utendaji kazi wa Kituo hicho, wakati wa ziara yake kukagua
miundombinu ya umeme hivi karibuni.
Ofisa
anayeshughulikia uangalizi wa Gridi katika Kituo cha kupoza umeme cha
Iringa, John Havie, akimwonesha Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt
Medard Kalemani (kulia kwa John) namna anavyoongoza mitambo kupitia
chumba maalum cha uangalizi (control room).
Naibu
Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (kulia) akimweleza
jambo Mbunge wa Jimbo la Kilolo, Venance Mwamoto (kushoto) walipokutana
katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa wakati wa ziara ya Naibu Waziri
kukagua miradi ya umeme mkoani humo hivi karibuni.
Naibu
Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (wa tatu kutoka
kushoto), akitoa maagizo kwa baadhi ya maofisa wa Shirika la Umeme
Tanzania (Tanesco), wanaosimamia Bwawa la Maji la Mtera mkoani Iringa,
alipotembelea Bwawa hilo ambalo maji yake hutumika kuzalisha umeme,
akiwa katika ziara kukagua miradi ya umeme hivi karibuni.
Naibu
Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (mwenye Suti ya Bluu –
Kulia), akizungumza na waandishi wa habari wa Iringa kuhusu
utekelezwaji wa miradi mbalimbali ya umeme mkoani humo, alipopitia
katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo, akiwa katika ziara ya kukagua miradi
mbalimbali ya umeme hivi karibuni.
Na Veronica Simba - Njombe
Serikali
imewataka wakandarasi wanaotekeleza miradi mbalimbali ya umeme hapa
nchini kuachana na visingizio vya uchelewaji wa fedha kutoka kwa
wafadhili na badala yake watumie fedha zao kukamilisha miradi hiyo kwa
wakati.
Naibu
Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani aliyasema hayo hivi
karibuni mkoani Njombe akiwa katika ziara kukagua utekelezaji wa miradi
mbalimbali ya umeme.
Dkt
Kalemani alisema kuwa, kumekuwepo na tabia ya baadhi ya wakandarasi
kuchelewesha utekelezaji wa miradi wanayoisimamia kwa kisingizio kuwa
hawajapokea fedha kutoka kwa wafadhili na hivyo aliwataka kuachana na
tabia hiyo mara moja.
Alisema,
mojawapo ya sifa katika kuchagua Mkandarasi ni pamoja na uwezo wake wa
kifedha katika kutekeleza mradi husika hivyo hakuna sababu ya Mkandarasi
kuchelewesha kazi kwa kisingizio cha fedha.
“Serikali
haitavumilia wakandarasi wanaosuasua katika utekelezaji wa miradi
wanayoisimamia kwa kisingizio cha fedha. Fedha kutoka kwa wafadhili
inapochelewa, wao watumie fedha zao kwani uhakika wa kulipwa upo,”
alisisitiza.
Akizungumza
mara baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa Mradi wa Umeme wa
Makambako – Songea, Dkt Kalemani aliwataka Maofisa wa Shirika la Umeme
Tanzania (Tanesco) wanaosimamia miradi mbalimbali ya umeme nchini
kuhakikisha wanawasimamia wakandarasi ipasavyo ili kukamilisha miradi
husika kwa wakati na viwango vinavyotakiwa.
Alisema,
Mradi wa Makambako – Songea ni mojawapo ya Miradi muhimu kwa Taifa,
hususan kwa wananchi wa maeneo husika hivyo ni lazima ukamilike kwa
wakati uliopangwa ambao siyo zaidi ya mapema 2018.
Naibu
Waziri alisema kuwa, matarajio ya Serikali ni kuhakikisha ifikapo mwaka
2025, vijiji vyote vya Tanzania vinakuwa na umeme hivyo ni lazima
kufanya kazi kwa bidii ili kufikia malengo hayo.
Awali,
akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mradi huo, Meneja wa Mradi
husika, Mhandisi Didas Lyamuya alisema kuwa Mradi wa Makambako – Songea
unatekelezwa chini ya Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results
Now-BRN) na unalenga kuunganisha umeme kutoka makambako hadi songea na
kunufaisha wananchi katika maeneo husika yaani mikoa ya Njombe na
Ruvuma.
Aidha,
Mhandisi Lyamuya aliongeza kuwa, Mradi huo ni wa umeme wa kilovolti 220
kwa umbali wa kilomita 250 na umelenga kuwanufaisha watu 22,700 katika
vijiji 120 vya maeneo husika.
Naibu
Waziri Kalemani yupo katika ziara kukagua utekelezaji wa miradi
mbalimbali ya umeme katika mikoa ya Iringa, Njombe, Katavi na Rukwa.
Ziara hiyo inatarajiwa kuhitimishwa mwishoni mwa mwezi huu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni