NHC ARUSHA YAKARIBISHA WAWEKEZAJI KUWEKEZA MRADI WA SAFARI CITY

Na Mahmoud Ahmad Arusha
Shirika la nyumba la Taifa limeanza ujenzi wa nyumba za mfano kwa ajili ya uwekezaji wa pamoja na wananchi katika kata ya Olmort jijini hapa mradi utakaojulikana kama Safari city huku likikaribisha wananchi kuja kuwekeza kwenye mradi huo.

Akizungumza na vyombo vya habari Meneja wa shirika hilo mkoani hapa James Kisarika alisema kuwa mji huo unajengwa kwa awamu na utakuwa na vitu vyote jamii inavyohitaji ikiwemo maji, umeme na mtambo wa kuchakata maji taka.

Alisema kuwa kila kiwanja kitakuwa na huduma za bomba la maji,utengenezaji wa barabara,uandaji wa hati miliki pamoja na michoro huku katika awamu ya kwanza shirika likitoa haki za uendelezaji wa viwanja vyenye ukubwa wa mita za mraba 200-600 na yatapatikana kwa shilingi 35,000 tu kwa mita moja ya mraba.

“Mji huu ni miongoni mwa miji ya kisasa hapa nchini na utaweza kusaidia watu wa kada mbali mbali kupata kumiliki nyumba na kujenga sisi tutakuwa wasimamizi wa mradi huu”alisema kisarika

Alisema kuwa ili kuwa mmoja wa wawekezaji katika mradi huo unapaswa kufuata utaratibu kwa kuchukuwa fomu ambayo ni bure na inatolewa na shirika hilo popote hapa nchini au tembelea tovuti yao www.thesafaricity.com na utalipia asilimia 25% ya thamani ya kiwanja unachotarajia kununua.
Aidha shirika la nyumba la taifa kupitia mradi huo linatoa fursa kwa makundi mbali mbali ya wawekezaji wenye mahitaji ya uendelezaji wa nyumba za makazi kwa vipato tofauti(chini,kati,na juu) majengo ya ofisi na biashara,maduka makubwa(Shoping mall)pamoja na madogo,maeneo ya biashara,maendeleo ya viwanda vidogo vidogo,burudani na utalii,Hospital.uwanda wa elimu,sanjari na huduma zote za kijamii.
Baada ya maelezo hayo wanahabari walipata fursa ya kutembelea eneo hilo na kujionea ujenzi wa nyumba za mfano za mradi huo ikiwemo nyumba za makazi nafuu ambazo zitakuwa za mfano kwa nyumba za makazi ambazo wawekezaji hao watatakiwa kujenga kwa mfano huo.
Kutakuwepo na eneo la msitu pamoja na mashine maalumu ya kuchakata maji taka ambayo baada ya kuyachakata maji hayo yatatumika tena kwa ajili ya umwagiliaji kwenye mradi huo.
Mwisho.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni