POLISI WAJIPANGA RASMI KUPAMBANA NA UHALIFU



MKUU WAPOLISI  WILAYA YA ARUSHA( SSP)EMMANUEL TILLE AKIZUNGUMZA NA VIONGOZI WA KATA YA MOIVARO TARAFA YA SUYE NA PAMOJA NA ASKARI WA ULINZI SHIRIKISHI WAKATI WA UZINDUZI WA VIKUNDI VINNE VYA KATA HIYO.
 Jeshi la Polisi linaendeleza harakati za kupambana na uhalifu ili kupunguza matukio ya namna hiyo, wananchi wa kata ya Moivaro tarafa ya Suye halmashauri ya jiji la Arusha hawapo mbali na jitihada hizo hivyo kuamua kujitokeza kwa moyo mmoja kupinga uhalifu kwa kuanzisha vikundi vinne vya ulinzi shirikishi kutoka mitaa ya Ngurumausi, Oldonyommasi, Moivaro Kati na Shangarao.

Akizindua vikundi hivyo ambavyo vimewezeshwa na wadau walioongozwa na Jeff Mligha ambao walijitolea vifaa mbalimbali vya ulinzi zikiwemo tochi, Mkuu wa Polisi wilaya ya Arusha Mratibu Mwandamizi wa Polisi Emmanuel Tille kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha alisema kwamba matarajio ya wananchi katika kata hiyo ya Moivaro ni makubwa na ana imani watakuwa wanalala na kuamka salama hivyo kuwataka walinzi hao wawe na nidhamu kwenye kazi yao.

“Kazi ya ulinzi ina miiko yake; kitu cha kwanza ni nidhamu ya hali ya juu. Mimi mwenyewe mpaka nafikia hatua hii ni kwa sababu ya nidhamu na nawataka ninyi muige mfano wangu, ninachosema hapa ni pamoja na kuwahi kazini, kutunza siri pasipo kuwazunguka wenzako pamoja na kufuata maelekezo ya wakubwa wa vikundi vyenu” Alisisitiza Tille.

Amesema japokuwa askari hao wapatao 42 wamepewa mafunzo lakini kupitia Wakaguzi wa Polisi wa Tarafa na askari kata wataendelea kuwapa mafunzo mara kwa mara ili waweze kufanya kazi zao kwa mujibu wa sheria, huku akiwaonya wasijichukulie sheria mkononi.

Amewataka wananchi wanapopata taarifa watoe kwa viongozi wa Polisi mara moja ili ziweze kufanyiwa kazi kwa haraka na hatimaye kufikia malengo ya kupunguza uhalifu ndani ya jiji la Arusha, huku akiwataka watendaji wa kata na Wakaguzi wa tarafa wahakikishe askari wa kata wanakuwa katika maeneo yao kila siku hali ambayo itawasaidia kubaini maeneo tete.

Akizungumza katika uzinduzi huo Diwani wa kata hiyo Rick Moiro alivitaka vikundi hivyo kufuata taratibu za kazi na kupambana na uhalifu hasa vijana wanaojihusisha na madawa ya kulevya aina ya bangi huku akiomba Jeshi la Polisi litoe ushirikiano wa karibu na vikundi hivyo pindi tu wanapoomba msaada.

 Afisa Mtendaji wa kata hiyo Bi. Editha Kisangia alisema kwamba mbali na hali ya uhalifu kuwa ya kawaida katika eneo hilo lakini hatarajii kutokea kwa changamoto kutoka kwa baadhi ya wananchi kushindwa kuchangia vikundi hivyo kwani faida wataiona baada ya kuanza kufanya kazi.

Wakaguzi wa Polisi wanaoongoza tarafa tatu za halmashauri ya jiji la Arusha toka mwaka 2013 ni pamoja na Frimina Massao tarafa ya Suye, Winibrita Moshi tarafa Elerai na Shabani Shabani tarafa ya Themi.
 

MKUU WA POLISI WILAYA YA ARUSHA( SSP) EMMANUEL TILLE AKIWAKAGUA ASKARI WA VIKUNDI VYA  ULINZI SHIRIKISHI KUTOKA MITAA YA NGURUMAUSI,OLDONYOMMASI,MOIVARO KATI NA SHANGARAO.
DIWANI WA KATA YA MOIVARO RICK MOIRO AKIZUNGUMZA NA VIKUNDI VYA ASKARI WA ULINZI SHIRIKISHI WALIOTOKA KWENYE BAADHI YA MITAA YA KATA YAKE BAADA YA UZINDUZI WA VIKUNDI HIVYO.
MMOJA WA WAHITIMU WA MAFUNZO WA VIKUNDI VYAASKARI WABULINZI SHIRIKISHI  AKIKABIDHIWA KITAMBULISHO CHA KAZI NA MKUU WA POLISI WILAYA (SSP)EMMANUEL TILLE.
BAADHI YA VIONGOZI WA KATA YA MOIVARO PAMOJA NA VIKUNDI VIPYA VYA  ASKARI WA ULINZI SHIRIKISHI WAKIMSIKILIZA MKUU WA POLISI WILAYA YA ARUSHA (SSP)EMMANUEL TILLE.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni