Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (katikati),
akimwagiza Kaimu Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco),
Mkoa wa Katavi, Wambura Nsiku, kuondoa nyaya za umeme
zilizotelekezwa na Mkandarasi eneo la Wachawaseme, Wilaya ya Mlele
mkoani Katavi, alipokuwa katika ziara ya kazi mkoani humo hivi karibuni.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (Kushoto)
akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mtakuja wilayani Mlele, Mkoa wa
Katavi, aliposimama kuwasalimia akiwa katika ziara ya kazi mkoani humo
hivi karibuni.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani akizungumza na
wananchi wa Inyongi wilayani Mlele, Mkoa wa Katavi, akiwa katika ziara ya
kazi mkoani humo hivi karibuni.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani akifurahia jambo
na wananchi wa Inyongi, Wilaya ya Mlele mkoani Katavi, alipozungumza
nao kuhusu utekelezwaji wa miradi ya umeme vijijini akiwa katika ziara ya
kazi mkoani humo hivi karibuni.
Diwani wa Kata ya Nsenkwa, wilayani Mlele, Mkoa wa Katavi, Eliji Malando
(aliyeinua mkono) akimtambulisha kwa wananchi (hawapo pichani) Naibu
Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (kushoto kwake),
aliposimama kuwasalimu na kuzungumza nao akiwa katika ziara ya kazi
mkoani humo hivi karibuni.
Wananchi mbalimbali wakiuliza maswali kwa Naibu Waziri wa Nishati na
Madini, Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani) kuhusu utekelezaji wa
miradi ya umeme vijijini pamoja na madini, alipozungumza nao akiwa
katika ziara ya kazi wilayani Mlele, Mkoa wa Katavi hivi karibuni.
Na Veronica Simba - Katavi
Serikali imeamua kuchukua na kuikamilisha kazi ya kuwasambazia
wananchi umeme, iliyokuwa ikifanywa na Mkandarasi Lucky Export ya
India, ambaye ameitelekeza na kuahidi kumchukulia hatua za kisheria.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani alitangaza
uamuzi huo kwa wananchi wa Kijiji cha Inyonga, Wilaya ya Mlele mkoani
Katavi, Julai 15 mwaka huu, akiwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji
wa miradi ya umeme wilayani humo.
Akiwa katika ziara hiyo, eneo la Wachawaseme, Naibu Waziri akiwa
amefuatana na uongozi wa Mkoa wa Katavi na Wilaya ya Inyonga, pamoja
na wataalamu kutoka wizarani, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na
Wakala wa Nishati Vijijini (REA), alijionea vifaa mbalimbali vya
kuunganishia umeme vikiwa vimetelekezwa na kutokuwepo na dalili
inayoonesha kazi kuendelea.
Naibu Waziri alisema, kwa kuwa Mkandarasi ameshindwa kufanya kazi
yake ipasavyo, aliyoianza Novemba 2014 na iliyotarajiwa kukamilika Juni
30 mwaka huu na kutoonesha jitihada za kuikamilisha kazi hiyo mapema,
basi ni lazima Serikali iingilie kati ili kuhakikisha wananchi wa eneo hilo
wanapata huduma waliyoitarajia mapema iwezekanavyo.
“Kuanzia sasa, nawaagiza Tanesco kwa kushirikiana na REA, waifanye
kazi iliyosalia wao wenyewe, usiku na mchana na ndani ya siku 15 iwe
imekamilika ili wananchi mpate umeme kama mlivyotarajia.”
Dkt Kalemani alisema, yeye na timu aliyofuatana nayo wamebaini kuwa
kazi iliyosalia ni kusimika nguzo ambazo zimeanguka, kuunganisha nyaya
na kufunga transfoma.
Naibu Waziri pia, alimwagiza Kaimu Meneja wa Tanesco wa Mkoa wa
Katavi, Wambura Nsiku kuhakikisha kwamba Mkandarasi huyo halipwi
fedha iliyokuwa imebaki kwani kazi iliyosalia itafanywa na Serikali.
Aidha, aliongeza kuwa, Serikali itamchukulia Mkandarasi huyo hatua
nyingine zaidi za kimkataba kwa mujibu wa sheria.
Akizungumzia zaidi kuhusu mikakati ya Serikali ya kuwapatia wananchi wa
Mlele umeme, Dkt Kalemani alisema maandalizi ya kuandaa uwanja
ambapo Jenereta kubwa ya kuzalisha umeme itafungwa, yataanza tarehe
moja mwezi Agosti na Septemba 1 mwaka huu, Jenereta husika itafungwa
na kuwaunganishia wananchi umeme.
Alisema kuwa, Vijiji 95 vya Wilaya ya Mlele, ambavyo havikuingia katika
Mpango wa kupatiwa umeme wa REA Awamu ya Pili, vyote vitapatiwa
nishati hiyo katika REA Awamu ya Tatu ambayo utekelezaji wake
umekwishaanza tangu tarehe 1 mwezi huu.
“Vijiji hivyo vitapata umeme kuanzia mwezi Septemba mwaka huu, lakini
tutaendelea kuvisambazia kwa muda wa miaka miwili na nusu hadi mitatu,
hivyo ndani ya muda huo, Mlele nzima itakuwa imepata umeme.”
Vilevile, Naibu Waziri alieleza kuwa, kuanzia Januari mwaka ujao, Serikali
itaanza kutekeleza mradi wa umeme wa maji wa Malagarasi ambao
unatarajiwa kuzalisha megawati 44.8 na kuwezesha kuondokana na
umeme wa jenereta wa kutumia mafuta, badala yake utatumika umeme wa
maji ambao ni wa uhakika zaidi.
Pia, alisema kuwa, upo mradi mkubwa wa kusafirisha umeme wa gridi
unaotoka Mbeya ambao utapita Sumbawanga, Mpanda, Kigoma mpaka
Nyakanazi ambao ni wa kilovolti 400 unaotarajiwa kutatua kabisa matatizo
ya umeme kwa maeneo husika.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri aliwaeleza wananchi wa Mlele kuwa
Serikali imepunguza gharama za umeme.
“Sasa hivi unakwenda kuomba umeme bila kulipia chochote na mtu
asiwadai chochote. Ile gharama ya maombi ya umeme mliyokuwa mnalipia
shilingi 6,000 tumeiondoa. Ukishaomba umeme wa mradi huu wa REA
unalipa shilingi 27,000 tu unaingiziwa umeme nyumbani kwako bila kulipa
hela nyingine yoyote. Hata ile shilingi 5,500 mliyokuwa mkitoa kwa
Tanesco wanapokuja kuwahudumia baada ya kuomba umeme, sasa hivi
hamlipi, mnahudumiwa bure,” alisisitiza.
Naibu Waziri alirejea maagizo ya Serikali kwa Tanesco kuwafuata wateja
mahala walipo badala ya kukaa ofisini kusubiri wateja wawafuate wao.
Aidha, aliwataka wananchi wa Mlele, pindi watakapopata umeme,
wautumie vizuri kwa ajili ya shughuli mbalimbali kwa maendeleo yao.
“Tunataka viwanda vidogovidogo vianze kwa kutumia umeme kwa sababu
tunajenga Taifa la uchumi wa viwanda”.
Naibu Waziri Kalemani yupo katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa
miradi ya umeme ukiwemo mradi mkubwa wa ‘Backbone.’
Amekwishatembelea mikoa ya Dodoma, Iringa, Njombe na Katavi na
anatarajia kutembelea mikoa ya Rukwa, Tabora na Geita.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni