MWENDA AISA JAMII KUSAIDIA WATOTOTO YATIMA NA WAISHIO KATIKA MAZINGIRA MAGUMU


Meya mstaafu wa Manispaa ya Kinondoni Yusufu Mwenda akigawa chakula kwa watoto  wanaolelewa katika kituo cha Maunga kilichopo Kinondoni Hananasifu Jijini Dar es salaam katika kusherekea sikukuu ya Iddi.
Meya mstaafu wa Manispaa ya Kinondoni Yusufu Mwenda akijumuika pamoja katika chakula cha pamoja na watoto hao wanaolelewa katika kituo cha Maunga kilichopo Kinondoni Hananasifu Jijini Dar es salaam .


ILI watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu waweze kutimiza ndoto zao za kimaisha , Meya mstaafu wa Manispaa ya Kinondoni Yusufu Mwenda ameiasa jamii kujenga utamaduni wa kutembelea vituo vinavyowalea watoto hao sanjari na kutatua changamoto wanazokabiliana nazo hatua itakayowasaidia kufikia malengo hao.
 

Ametoa rai hiyo juzi mara baada ya kujumuika pamoja katika chakula cha pamoja na watoto hao wanaolelewa katika kituo cha Maunga kilichopo Kinondoni Hananasifu Jijini Dar es salaam ambapo pia alitoa misaada mbalimbali ya yakiwemo madaftari, kalamu, sabuni,vyakula na fedha kwa ajili ya kusaidia mahitaji ya kituo hicho.
 

Alisema watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu wanapaswa kupata elimu kama ilivyo kwa watoto wengine wanaoishi na wazazi wao hivyo ni jukumu la kila mwananchi kuona umuhimu wa kutoa chochote alichonacho ili kuwawezesha watoto hao kuipata elimu hiyo kwa ukamilifu.

 

“Tunashukuru kwa sasa Rais John Magufuli ametoa unafuu wa elimu bure kwa watoto katika ngazi ya msingi na Sekondari kwa hiyo kilichopo hapo ni mahitaji madogo madogo ili kumfanya mtoto aweze kufika shuleni na kuudhuria masomo, kama jamii hili ni jambo linalowezekana kabisa tukalitatua kama kila mmoja wetu atakuwa na nia” alisema Mwenda
 

Aidha katika hatua nyingine Mwenda ameahidi kutoa huduma ya mahitaji ya shule kwa watoto wanaosoma darasa la sita hadi sekondari waliopo katika kituo hicho ili kukipunguzia mzigo kituo hicho katika suala linalohusiana na masomo Mbali na hilo pia ameahidi kununua vitanda kwa ajili ya watoto hao na kuvifanyia ukarabati vitanda vilivyoharibika baada ya kuombwa na uongozi wa kituo hicho kutatua tatizo hilo lililodumu kwa muda mrefu kituoni hapo.
 

Kwa upande wake Mlezi wa kituo hicho Zainabu Maunga alisema dhumuni la kuanzishwa kwa kituo hicho chenye jumla ya watoto 50, lilikuwa kutoa msaada wa malezi kwa watoto hao waliopatikana kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya vifo vya wazazi wao.
 

Alisema kituo hicho kinalea watoto hao wakiwemo wavulana 26 na wasichana 24 kwa kutegemea misaada ya watu mbalimbali wanaofika kituoni hapo huku akitaja changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika malezi ya watoto hao.
 

Alizitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na ufinyu wa eneo la kituo, mavazi kwa watoto, chakula pamoja na huduma za afya pale inapotokea mtoto kaugua hatua inayomfanya kupaza sauti yake kwa jamii kila siku akiomba imsaidie kutatua changamoto hiyo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni