Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. MAKAME MBARAWA
amewataka wahandisi na makandarasi nchini kujielimisha vya kutosha
kuhusu mfumo mpya wa ujenzi wa barabara wa mikataba inayopima huduma
zinazopatikana kwenye barabara hizo.
Mfumo huo ambao unaotumiwa na nchi zilizoendelea utawawezesha
makandarasi nchini kujenga barabara kwa mkataba wa muda mrefu wa kupima
huduma ya barabara na mkandarasi atalipwa kulingana na matokeo.
Akifungua semina ya wadau wa barabara kutoka nchi 19 na taasisi 30
duniani inaofanyika jijini Arusha Prof. Mbarawa amesema utaratibu huo
mpya utawawezesha makandarasi kujenga barabara za kiwango cha juu zenye
ubora na usalama na kupunguza utaratibu wa ukarabati wa kila wakati
unaogharimu serikali fedha nyingi.
“Ukijenga barabara kwa viwango vya juu na ukiisimamia mwenyewe kwa muda
mrefu itapunguza gharama za ukarabati wa kila mwaka zinazotolewa na
serikali” amesema Prof. Mbarawa
Profesa Mbarawa amekiri uwepo wa changamoto kubwa kwenye ujenzi na
ukarabati wa barabara za wilaya na kusisitiza kwamba barabara nyingi
zinajengwa chini ya kiwango na hazina uwiano na thamani ya fedha
zilizotumika.
“Serikali inajipanga kuanzisha wakala wa barabara za wilaya
utakaohakikisha unafanya kazi kama ilivyo kwa wakala wa barabara kuu na
za mikoa ili kuongeza ufanisi” amesema Prof. Mbarawa
Profesa Mbarawa amepongeza Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB) kwa kazi
nzuri ya kusambaza fedha za ujenzi wa barabara katika halmashauri zote
kwa wakati na kuwataka viongozi wa halmashauri hizo wazitumie fedha hizo
kwa kazi zilizokusudiwa.
“Atakayecheza na fedha za mfuko wa barabara hatutakuwa na uvumilivu
naye, tunataka fedha hizo zifanye kazi iliyokusudiwa ili adhma ya
kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025 kwa kuwa na miundombinu bora
ifanikiwe” amefafanua Prof. Mbarawa
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, sekta ya
ujenzi Eng. JOSEPH NYAMHANGA amesema semina hiyo ya siku tano inawaleta
wataalam wa barabara nchini kujadili changamoto na mafanikio ya mfumo
mpya ya ujenzi wa barabara na mfumo huo utakapoanza utapunguza gharama
za ujenzi na kuwaongezea nguvu makandarasi wazawa.
Amesema Tanzania ina takribani ya km 87,481 za mtandao wa barabara
ambapo km 35,000 ni barabara kuu na za mikoa, km 52, 581 ni barabara za
wilaya ambapo zote zitanufaika na mfumo huo utakapoanza.
Naye meneja wa bodi ya mfuko wa barabara Joseph Haule amesema
utaratibu huu mpya utakapoanza nchini utapunguza gharama za ujenzi wa
barabara kwa asilimia 30 na utanufaisha wahandisi na makandarasi wengi
nchini kutokana na sera nzuri ya kuwalinda makandarasi wazawa.
Takribani wataalam 200 wa masuala ya barabara kutoka nchi za Afrika,
Ulaya na Amerika wanashiriki katika semina hiyo inayoongozwa na
mwenyekiti wa shirikisho la masuala ya barabara Bw. Kiran Kapila lengo
likiwa ni kubadilishana uzoefu katika masuala ya ujenzi wa barabara bora
kwa gharama nafuu.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni