Picha na John Stephen, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH)
Na John Stephen
Dar es Salaam, Tanzania. Taasisi
ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI)-Muhimbili LEO imefanya upasuaji mkubwa
wa moyo kwa mtoto, Happiness John Josephat ambaye amepandikizwa
peacemaker (betri ya umeme wa moyo) kwenye mfumo wa moyo wake.
Mmoja wa madaktari wa moyo
walioshiriki kwenye upasuaji huo, Dk Godwin Sharau wa taasisi hiyo
amesema upasuaji huo umechukua saa moja na kwamba mtoto anaendelea
vuzuri.
Dk Sharau amesema mtoto huyo
amepandikizwa peacemaker (betri ya umeme wa moyo) ambayo itasaidia
kuunganisha mishipa ya fahamu ya umeme wa moyo ambayo inaunganisha
vyumba vya moyo vya juu na chini kwenye moyo wa binadamu.
“Upasuaji huu ni wa kwanza
kufanyika Tanzania. Upasuaji kama huu unafanyika kwa watu wazima, lakini
watu wazima hawahitaji upasuaji wa moyo wa kupandikiza. Watoto
wanahitaji upasuaji wa moyo wa kuipandikiza.
“Tatizo la mtoto huyu ni la
kuzaliwa. Na ni nadra kutokea. Inaweza kupita miaka mingi bila watoto
kutokea tatizo kama hilo. Upasuaji umefanywa kwa ushirikiano wa
madaktari wa moyo na madaktari wa matibabu ya moyo nikiwamo mimi (Dk.
Godwin Sharau), Dk Michael Valentine kutoka Marekani, Dk Kisenge na Dk
Sulende Kubhoja, Dk wa usingizi, Dk Anjelan Muhozya na madaktari
wengine ambao wamesaidia katika upasuaji huu,” amesema Dk Godwin Sharau.
Mama wa mtoto huyo, Elitruda Eligi
Malley ambaye ni mkazi wa Sakina-Raskazon mkoani Arusha amewashukuru
madaktari wa Taasisi hiyo kwa kufanya upasuaji huo na mtoto wake kutoka
salama katika chumba cha upasuaji.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni