MAKALA KUHUSU UGONJWA WA KIPINDUPINDU: Tujilaumu Watanzania kwa kuugua Kipindupindu

Kipindupindu ni ugonjwa wa kuharisha na kutapika unaosababishwa na vimelea vya bacteria vinavyoitwa kwa lugha ya kitaalam “vibro cholera”. Chanzo cha kikubwa cha ugonjwa huu huletwa na vimelea vilivyomo kwenye kinyesi na matapishi ya mgonjwa wa kipindupindu.

Kwa miaka mingi sasa wananchi wa Tanzania tumekumbwa na magonjwa ya aina mbalimbali ya mlipuko ukiwemo ugonjwa wa kipindupindu ambao umeenea kwa kasi kubwa sana kutokana na kuwepo kwa mazingira hatarishi yanayochochea mlipuko wa ugonjwa huo.

Kwa mwaka 2015 ugonjwa wa kipindupindu umetikisa nchi yetu kwa kiasi kikubwa na kusababisha watu kupoteza uhai na kupunguza nguvu kazi, watoto kuwa yatima wake kwa waumwe kuwa wajane na wengine kuwapoteza ndugu jamaa na marafiki zao.
Siyo mara ya kwanza kutokea kwa mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu nchini ila imekuwa ni tabia ya watanzania kuchukulia mazoea na kuuona ugonjwa huu kama michezo ya watoto kwenye televisheni       ( TV Game) na huku miaka nenda rudi unazidi kuteketeza watanzania. kwanini watanzania hatulioni hili kuwa ni janga la kitaifa?

Ugonjwa wa kipindupindu ulioanza Agosti 15 2015 katika mkoa wa Dar es salaa na kuenea kwa kasi katika mikoa mingine 20 nchini, kwa mujibu wa taarifa ya tarehe 15 Desemba 2015 kumekuwa na wagonjwa wapya 141 na kufanya jumla ya wagonjwa waliokwa wanaendelea kupatiwa matibabu kwenye vituo vya kutolea huduma katika mikoa yote iliyoathirika kuwa 184 na vifo vipya viwili.

Tangu ugonjwa huu uanze jumla ya watu 11,257 walipata ugonjwa huu na kati yao 177 wamefariki kwa ugonjwa huu ambayo ni sawa na asilimia 1.5 ya waliougua, mpaka sasa kwa wastani ugonjwa huu umepungua katika mikoa ya Dar es salaamna kwa mkoa wa Iringa na mji wa Moshi kwa kiasi kikubwa wamefanikiwa kudhibiti ugonjwa huu.


Katika tamko la Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimua alilolitoa tarehe 16 Desemba 2015 kuhusu mapambano ya ugonjwa wa kipindupindu, Waziri huyo alipiga marufuku uuzaji wa matunda yaliyokatwa na vyakula sehemu za wazi(barabarani) na kutoa amri  watakaokiuka wachukuliwe hatua mara moja.

“ Nahitaji nipatate taarifa ya utekelezaji kila siku kutoka kwa Waganga wa Mikoa na Wilaya na Serikali haitasita kuchukua hatua kwa viongozi ambao watashindwa kudhibiti ugonjwa huu katika maeneo yao” alisema Waziri Ummy katika tamko lake kupitia Vyombo vya Habari. 

Mara baada ya kutolewa kwa tamko hilo siku tatu baadae mwandishi wa makala hii nilifanya ziara ndogo kuzunguka baadhi ya maeneo ya Jiji la Dares salaam hasa katikati ya Jiji na kugundua kuwa bado kuna uuzaji wa matunda yaliyokatwa na vyakula sehemu za wazi(barabarani) unaendelea. Katika kufatilia hilo kujua nini Jijini limefanya hasa Manispaa ya Ilala ambayo ndo muhusika wa maeneo ya katikati ya Jiji niliwasiliana na msemaji wa Manispaa ya Ilala Bw. Daud Langa na kutoa ufafanuzi wa suala hilo.

Msemaji wa Manispaaa ya Ilala alisema katika suala hili watendaji wa kata na mitaa wanahusika moja kwa moja kusimamia na kufatilia kwa karibu operesheni hii na kusisitiza sheria za afya kuzingatiwa na hakutokuwa na huruma kwa yoyote atakayevunja sheria.

“ Kwa mfanyabiashara yoyote tutakayemkamata anauza matunda yaliyokatwa na vyakula maeneo ya wazi tutamkamata na kumfungulia mashtaka ya kuvunja sheria za Afya na adhabu yake ni faini ya Sh 30,000 au kwenda jela miezi mitatu au vyote kwa pamoja” alisema Langa alipokuwa akitoa maelezo hayo.

Nakumbuka Desemba 9 mwaka huu  ilitangazwa kuwa ni siku ya Uhuru na Kazi na Mhe Rais Dkt Jhn Pombe Joseph Magufuli na kuamuriwa iwe siku ya kufanya usafi katika maeneo yetu ikiwa ni mapambano dhidi ya ugonjwa wa kipindupindu ulioenea kwa kasi . katika ziara yangu nilipita maeneo ya kawe sokoni na mto Mbezi ambapo wananchi kushirikiana na watumishi wa taasisi za umma na binafsi walijitokeza kufanya usafi katika maeneo hayo.

Katika maeneo ya Kata ya kawe eneo la mto Mbezi watumishi wa iliyokuwa Wizara ya kazi na Ajira ambayo imehamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu na kuwa Sera, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu walijitokeza kufanya usafi wakishirikiana na wanachi wa maeneo hayo. Cha kushangaza ni pale watumishi hao walipofika na kuanza kufanya usafi na huku wananchi wa pale wakiwaangalia kama wafanya maonesho ya sanaa za maigizo.
Hivi tunasubiri waje watu toka nje ya Tanzania  watusafishie maeneo yetu sisemi watanzania wote ni wavivu hapana ndio wapo wachache waliobarikiwa kwa kuelewa nini wajibu wao katika jamii inayowazunguka lakini wachache pia wanaharibu sifa ya watanzania na kufanya watanzania tuonekane wavivu kazi kutoa lawama hata kwa yale tutanayoweza kuyafanya yaliyo ndani ya uwezo wetu.

Tabia yetu watanzania tulio wengi ni kutupia lawama na malalamiko kwa Serikali hivi kwani Serikali ni nani? Serikali ni mimi na wewe na yule swala sio Serikali imekufanyia nini ila wewe umeifanyia nini nchi yako? Suala la usafi liko chini ya uwezo wetu tulifanye basi kwa bidii na hatuifanyii serikali bali tunaifanyia nchi yetu na vizazi vyetu tukiwa na tabia ya usafi toka tunakoishi mitaani basi itakuwa tabia ya taifa zima kwa ujumla.

Watanzania tujilaumu wenyewe kuugua kipindupindu kwasababu tunaweza kukizuia kwa kuzingatia usafi wa mazingira na usafi wa mipango miji pia kutojenga kwenye mikindo ya maji mito na maziwa na vyanzo vya maji kwani maji ndo chanzo kikubwa cha kipindupindu kwani maji yanatumika kwa asilimia kubwa katika matumizi ya binadamu ya kila siku.

Serikali kwa upande wake inapambana sana na suala hili la kipindupindu kwa kasi kubwa kupitia wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto ikishirikiana na Halmasahuri za Wilaya, Ofisi za Afya za Mikoa na Wilaya na katika kukabilana na ugonjwa huu sekta zote husika zikiwemo Maji, Elimu, Mawasilano, Uchukuzi na Ujenzi hazina budi kushirikiana kwa pamoja ili kutokomeza ugonjwa huu.

Aidha wadau wa maendeleo ya jamii hawakuwa nyuma kusaidia kampeni hii ya kutokomeza kipindupindu nchini, mashirika kama vile shirika la Afya Duniani (WHO), CDC, USAID, MSF, Red Cross na UNICEF kwa kushiriki katika kukabiliana na mlipuko huu. Kwa mujibu wa Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee wadau hawa wamechangia msaada wa fedha na vifaa vyenye thamani ya Tsh 1,884,000,000 na serikali ikatoa Tsh 900,000,000 katika kupambana na ugonjwa huu.

Watanzania tunahamasishwa kupambana na ugonjwa huu kwa kuona kuwa kipindupindu ni aibu kwetu mtu kuugua ugonjwa huu wakati unazuilika kwa kuzingatia usafi tu. Wote kwa pamoja kupitia magazeti Radio, Televisheni mitandao ya Jamii kama Whatsaap, Twitter na Instagram tuelimishane kuhusu usafi wa mazingira ili kutokomeza kpindupindu na kikwa historia nchini.

Kwa taarifa kuhusu ugonjwa wa kindupindu unaweza kuzipata kupitia ujumbe mfupi kwenye simu yako kuandika neon kipindupindu kwenda 15774 na utapata taarifa sahihi juu ya ugonjwa wa kipindupindu na ujembe huu unapatikana bila malipo. Tukumbuke kuwa kinga ni bora kuliko tiba, kuugua Kipindupindu ni aibu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni