Na Richard Mwaikenda
NAIBU Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Mhandisi Edwin Ngonyani, amepiga marufuku kwa Halmashauri
zote nchini, kuwatumia wajenzi wa barabara wasiosajiliwa na Bodi ya
Wahandisi nchini (ERB).
Mhandisi Ngonyaji alichukua hatua hiyo
alipofanya ziara ya kujua utendaji wa Bodi ya Mfuko wa Barabara nchini,
Dar es Salaam juzi, ambapo alielezwa na Meneja wa Bodi hiyo, Joseph
Haule, kuwa barabara nyingi kwenye halmashauri zinajengwa chini ya
viwango kwani wanaopewa tenda hawana utaalam wa ujenzi wa
barabara.
Alisema kuwa, kuanzia sasa halmashauri
ziachane kabisa kuwatumia mafundi wasio na utaalam, bali
wawatumie wahandisi waliosajiliwa na Bodi ya Wahandisi nchini, ili
barabara zijengwe kwa viwango vinavyotakiwa, na watakaokaidi agizo hilo
wanyimwe fedha za mgao kutoka kwenye bodi hiyo.
Pia , Mhandisi Ngonyani, ameitaka bodi
hiyo, kutokutuma fedha za ujenzi wa barabara kwa
halmashauri yoyote ambayo imetumia fedha walizopelekewa na kuzitumia
kinyume cha malengo yaliyokusudiwa.
Amemwagiza Meneja wa Bodi hiyo,
kuzichukulia hatua halmashauri zote ambazo zimetumia fedha hizo tofauti
na malengo yake ikiwa ni pamoja na kutopelekewa fedha hadi
hapo watakapoziresha walizozitumia.
"Ongezeni nguvu zaidi katika kusimamia
matumizi ya fedha za mfuko wa barabara kwa halmashauri ambazo fedha hizo
zinatumiwa kwa shuguli zisizo za barabara", alisisitiza Mhandisi
Ngonyani.
Naye Meneja wa Bodi ya mfuko huo, Joseph
Haule, alielezea mafanikio ya mfuko huo tangu ianzishwe miaka
15 iliyopita kwamba kuwa mapato yameongezeka kutoka sh.
bilioni 73 mwaka 2005 hadi sh bilioni 752.
"Kutokana na kupanda kwa mapato mtandao wa
barabara umeboreshwa kwa kiwango kikubwa kwa kuwa barabara nyingi
zimejengwa kutokana na kipato hicho", alisema Meneja
Haule.
Aidha, Meneja wa Bodi ya mfuko huo, Haule,
alisema kuwa mfuko huo ambao chanzo chake kikubwa ni
ukusanyaji wa fedha kutoka sehemu ya mauzo ya mafuta ya petroli na
dizeli nchini, Bodi italitia mkazo katika ufuatiliaji wa matumizi ya
mfuko kuhakikisha vyanzo vipya vya mapato
vinapatikana.
Alisema kuwa, katika kuhakikisha
ufuatiliaji wa usimamizi wa fedha hizo unatekelezwa, mfuko tayari
umezichukulia hatua halmashauri tatu zikiwemo za Kinondoni, Songea
Vijijini na Bukoba Vijinini ambazo zimetumia fedha za mfuko wa barabara
kinyume na malengo yaliyokusudiwa.
Alisema Bodi ya Mfuko wa Barabara
ilianzishwa kwa lengo la kukusanya mapato, kufuatilia matumizi ya fedha
hizo na kugawa kwenye taasisi ambapo asilimia 63 zinapelekwa Wakala wa
Barabara wa Serikali (Tanroads) kwa ajili ya matengezo barabar kuu na za
mikoa, asilimia 30 katika halmashauri 166 kwa ajili ya ujenzi wa
barabara za halmashauri na asilimia 7 zinapelekwa wizara ya
ujenzi
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni