KATIBU MKUU WIZARA YA AFYA AFANYA ZIARA YA KUSHTUKIZA HOSPITALI YA RUFAA KANDA YA MBEYA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na ustawi wa jamii, Dk. Donald Mbando akitembelea miradi katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya akiwa sambamba na Mkurugenzi wa Hospitali hiyo.


 Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na ustawi wa jamii, Dk. Donald Mbando akipokea maelezo kutoka kwa mhandisi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na ustawi wa jamii, Dk. Donald Mbando akipata maelezo juu ya ukamilishwaji wa jengo la vipimo vya uchunguzi katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya.


 Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na ustawi wa jamii, Dk. Donald Mbando akitotoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari mkoani Mbeya
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na ustawi wa jamii, Dk. Donald Mbando akitoa maelezo kuhusu mfumo wa ukusanyaji mapato kwa njia ya Tehama.

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Afya na ustawi wa jamii, Dk. Donald Mbando, ametoa muda wa wiki mbili kwa uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda iliyopo mkoani Mbeya kuhakikisha inakamilisha ukarabati wa maabara ya kupimia magonjwa yanayoambukiza haraka ikiwemo Ebora.
 
Dk. Mbando alitoa maagizo hayo jana alipofanya ziara katika Hospitali hiyo kwa lengo la kufuatilia miradi ya idara ya afya inayotekelezwa ikiwemo Hatua za ukarabati wa maabara, ukarabati wa Wodi za wagonjwa na ujenzi wa jingo la vipimo vya uchunguzi.
 
Akizungumza na uongozi wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, Katibu mkuu alisema lengo la ziara yake ni kukagua na kuangalia miradi ya maendeleo ili kujua hatua ilipofikia katika kipindi ambacho serikali inaenda kuandaa bajeti.
 
Alisema lengo la kutoa wiki mbili kukamilisha ukarabati wa jingo la maabara ili liweze kuanza kutumika kutokana na uwepo wa tishio la ugonjwa wa mafua makali kuikumba dunia hivyo kuokoa gharama za kusafirisha sampuli za wagonjwa kwenda nje ya nchi.
 
Pia Katibu Mkuu aliagiza uongozi wa Hospitali hiyo kuhakikisha ndani ya wiki moja analetewa mchanganuo wa fedha za kumalizia ujenzi wa jingo la vipimo vya uchunguzi ili kuweza kuombea fedha kutoka serikalini kwa mwaka wa fedha 2015/2016 ambapo Milioni 500  zilishatolewa katika ujenzi wa awamu ya kwanza.
 
Alisema jingo hilo likikamilika litasaidia kurahisha upatikanaji wa vipimo kwa wagonjwa kirahisi na kuwapunguzia gharama za kusafiri wananchi kwa ajili ya kufuata vipimo jijini Dar es salaam ili hali uwezekano wa kupata Mbeya upo kutokana nawataalam kuwepo.
 
Alisema kukamilika kwa jengo hilo kutarahisisha kupatikana kwa vipimo aina ya X- ray, ultra sound, ct scan na mashine zingine kwa ajili ya wagonjwa kutoka mikoa saba inayotegemea huduma katika Hospitali ya Kanda ya Mbeya.
 
Katibu mkuu pia aliagiza Hospitali zote nchini kuanzia Hospitali za Wilaya, Hospitali za Mikoa na Hospitali za Rufaa za Mikoa na Kanda  kuhakikisha zinakuwa na mfumo wa Elekitroniki kwa ajili ya ukusanyaji wa mapato ili kupunguza mwanya wa upotevu wa fedha na ubadhilifu.
 
Alisema mfumo huo pia utasaidia kurahisisha mawasiliano baina ya madaktari kwa madaktari au Hospitali moja na nyingine kuhusiana na tatizo la ugonjwa pindi tatizo linapokuwa mkubwa na msaada unahitajika.
 
Aidha aliupongeza uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya kwa kuongeza ukusanyaji wa mapato baada ya kuanzisha mfumo wa TEHAMA ambapo kabla ya mfumo huo walikuwa wakikusanya Milioni 50 kwa mwezi lakini sasa zinakusanywa shilingi Milioni 500.
 
Katika agizo la nne, Katibu Mkuu ameitaka Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya kubuni huduma za miradi ili kuongeza mapato zaidi kama vile kuboresha chumba cha kuhifadhia maiti ili kutoa huduma ya haraka nakiwango cha juu, utengenezaji wa maji ya dawa(IV – Fluids) na vilainishi vya mafuta ya ngozi pamoja na uanzishwaji wa Chuo kikuu kwa ajili ya kuinua elimu za watumishi wa Idara ya afya.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni